Thursday, February 27

DC Mjaja: SItoivumilia familia yeyote itakayohusika na kusuluhisha kesi za udhalilishaji.

 

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

MKUU wa Wilaya Mkoani Khatib Juma Mjaja amesema, hatoivumilia familia yeyote itakayohusika na kusuluhisha kesi za udhalilishaji zinazotokea kwenye jamii.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mkuu huyo alisema, zipo baadhi ya familia hukimbilia kusuluhisha kesi mara tu baada ya mtoto wa kufanyiwa udhalilishaji, jambo ambalo sio sahihi, kwani linachangia kuongezeka kwa vitendo hivyo.
Alisema kuwa, watakapoibaini familia yeyote ambayo mtoto wao amebakwa na kisuluhisha watawapeleka kwenye vyombo vya Sheria kwa hatua zaidi.
“Kwa kweli familia zinazosuluhisha kesi za udhalilishaji zinarudisha nyuma juhudi zinazofanywa na Serikali pamoja na taasisi binafsi katika kupiga vita vitendo hivyo, lakini sasa tutapambana vikali kuhakikisha tunadhibiti”, alisema Mkuu huyo.
Alieleza kuwa, kati ya vipao mbele vya Wilaya yao ya Mkoani ni kuhakikisha wanapiga vita vitendo vya ukatili na udhalilishaji sambamba na kuwachukulia hatua za kisheria wanaohisika kufanya matendo hayo.
“Hatuna muhali kwa hili, tunapopata taarifa ya mtoto ama mtu kufanyiwa udhalilishaji, tunasimamia kuhakikisha Sheria inachukua nafasi yake”, alieleza.
Mjaja aliwataka waananchi kuondosha muhali kwani ndio unaosababisha kuongeza udhalilishaji na kupelekea kuvunja ustawi, heshima na utu wa mtoto ama mtu aliefanyiwa kitendo hicho.
Aidha aliwataka wanaojihusisha na vitendo vya udhalilishaji kuacha mara moja, kwani Serikali ya Wilaya inashirikiana na vyombo vya Sheria katika kukomesha matendo hayo ambayo ni jinamizi linalowakumba watoto na kusababisha kukosa haki zao stahiki.
“Hatuwezi kukubali watu wawafanyie udhalilishaji wanawake na watoto alafu tuwaache, hii tabia tunataka ikome mara moja”, alieleza Mjaja.
Hata hivyo aliwataka vijana kukaa pamoja na kuanzisha vikundi vya ujasiriamali, jambo ambalo litasaidia kujiepushakufanya mambo maovu, kwani muda wote watakuwa na kazi za kufanya.