ABDI SULEIMAN
KAIMU Mratib wa Tume ya Ukimwi Pemba Ali Mbarouk Omar, amesema kuwa suala la unyanyapaa kwa watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi, limepungua kwa kiasi kikubwa na watu hao wanaishi na familia zao na kwa amani.NA ABDI SULEIMAN
Alisema watu hao wanapata huduma zinazoendana na afya zao, pamoja na kushirikiana na jamii kama ilivyo kwa watu wengine, kwani elimu iliyotolewa imeweza kuwawasaidia sana wananchi kupata elimu hiyo.
Mratib huyo aliyaeleza hayo wakati alipokua akizungumza na vijana kutoka taasisi mbali mbali zinazofanya kazi na Vijana Kisiwani Pemba, huko katika ukumbi wa Tume ya Ukimwi Chake Chake Pemba.
Akizungumzia suala la Vijana, aliitaka jamii kutoa elimu sahihi ya ukimwi na stadi za maisha na elimu ya afya ya uzazi, pamoja na kutambua viashiria hatari vinavyowakumba vijana.
Wakiwasilisha taarifa za baadhi ya vijana, wamesema kuwa wamekuwa wakitoa elimu kwa vijana juu ya kujikinga na maambukizi mapya ya VVU kupitia njia mbali mbali.
Ali Hamad khatib kutoka chama cha uzazi na malezi bora Tanzania (UMATI), alisema waliweza kutoa elimu na huduma juu ya maambukizi ya UKIMWI, magonjwa ya ngono, afya ya uzazi na stadi za maisha, kwa kuwafikia vijana 600 wakiume na 700 wa kike.
Naye mratib wa vijana kutoka PIRO Asha Nassor Ali, alisema wameweza kuwafikia vijana 150 kwa kuwapatia elimu ya stadi za maisha ili waweze kujitambua afya zao.
Aidha aliitaka ZAC kuziangalia kwa jicho la huruma taasisi za vijana zinazofanya kazi ya kuelimisha vijana juu ya masuala ya ukimwi.
Kwa upande wake mwakilishi kutoka JUKAMKUM Maira Ismail Rashid, alisema waraibu wengi wamepata mwamko wa kujali afya zao, kupunguza tabia hatarishi na wanatoa ushirikiano kupima afya zao.