Monday, November 25

WAANDISHI andikeni habari zianzohusu mazingira

NA HANIFA SALIM, PEMBA.

WANDISHI wa habari nchini wametakiwa kujikita zaidi katika kuandika habari zinazohusiana na athari za uhalifu wa mazingira ili jamii ijue umuhimu wa kuyatunza mazingira yaliyowazunguka.

Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa habari wa kupinga vita matumizi ya madawa ya kulevya na uhalifu (ODAJACT) Tanzania Edwin Soko’o aliyasema hayo alipokua akizungumza katika mkutano wa kujadili mazingira uliowashirikisha wandishi wa habari uliofanyika kwa njia ya mtandao (Zoom Metting).

Alieleza, bado vyombo vya habari havijajikita katika kuandika habari juu ya uhalifu wa mazingira, kuelimisha jamii na kuonesha athari za kuwauwa wanyama wa asili ambao wanaishi kwenye mapori.

Alisema, mwandishi wa habari anapotaka kuandika habari hizo lazima afanye uchunguzi (I.J) kwa kusoma sheria ili atambue namna ya hifadhi ya mapori yanasimamiwa na nani na kwa sheria zipi na binaadamu anaposogea katika eneo lililotengwa kwa ajili ya wanyama sheria gani inachukuliwa.

“Lazima tufanye uchunguzi wa kina katika kuandika habari za uharibifu wa mazingira, kuna haja ya kufahamu kwa nini wanyama wanavamia maeneo wanaoishi watu, inamaana watu wamekaribia makaazi hayo kwa hiyo sasa watu wanazidi kuingia kwenye mapori ambayo wanyama walikua wanafugwa”, alisema.

Aidha alisema, umuhimu wa utunzaji wa mazingira hususani katika misitu waandishi wanapaswa kupiga vita vya hali ya juu kwa kiwango kinachoweza kuripotiwa katika mazingira ya usahihi kabisa.

Nae Mkufunzi wa wafunzo hayo Lucyphine Kilanga alisema, suala la
kufanyiwa mafunzo ya usalama wa waandishi wa habari juu ya uandishi wa habari za uhalifu wa mazingira ni jambo la msingi ili kuweza kujikinga kwenye kazi zao.

Nao waandishi wa habari walioshiriki mafunzo hayo waliishauri OJATACT kuandaa mafunzo kwa ambao watajikita kuandika habari za mazingira kwani walisema, masuala hayo yanahitaji umakini, usiri na kuchukua tahadhari juu ya maisha yao.

Walisema, wengi wanaohusika na uhalifu wa mazingira au kufanya uhalifu huo ni watu wenye uwezo mkubwa hivyo walisema, lazima mwandishi ajue tahadhari za kuchukua juu ya usalama wao kazini.

“Tukiangalia Dar-es-salaam pekee kwa mujibu wa wakala wa misitu kwa mwaka wanatumia zaidi ya tani 500,000 na ukweli ni kwamba mikaa hii inatoka kwenye misitu”, alisema.

Hata hivyo walisema, uchafuzi wa mazingira wa aina yoyote waathirika wake wakubwa ni wanawake na watoto hivyo ni vyema jamii iweze kuwalinda watu hao katika ustawi wake wa kimaisha.

MWISHO