NA ABDI SULEIMAN.
WADAU wa Habari Kisiwani Pemba, wamewataka waandishi wa habari kuwa wabunifu katika kuandika habari zao na sio kuandika habari za kundi moja.
Wadau hao wamesema mwandishi wa habari ni yule anayeandika habari mchanganyiko, na sio kundi moja jambo ambalo linafanya bahari nyingi kutokupata waandishi.
Hayo yalielezwa na wanakongamano la kujadili uhuru wa kujieleza, uhuru wa habari na maadili kwa waandishi wa habari, kwenye kongamano lililoandaliwa na klabu ya waandishi wa habari Pemba (PPC), kupitia Umoja wa vilabu vya waandishi wa habari Tanzania (UTPC) mkongamano lililofanyika mjini Chake Chake.
Dk.Amour Rashid alisema waandishi wanapaswa kuzingatia mavazi na utamaduni wa wazanzibar, wakati wanapokuwa kazini sambamba na kuwashauri kujiendeleza kielimu ili kuweza kujuwa lugha mbali mbali.
“Vizuri katika habari zenu mukajuwa hata sheria mbali mbali na katiba zetu za nchi, licha ya changamoto munazokumbana nazo wakati wa upatikanaji wa habari”alisema Dk Amour.
Naye Said Mohamed Ali alisema umuhimu wa habari upo lakini hatuutumii ipasavyo na kubaki kuwaonea wasio kuwa na sauti, kwa kushindwa kuwasemea changamoto zao.
Msaidizi katibu wa Mufti Zanzibar Shekhe Said Ahmad Mohamed, alisema imekuwa ni biashara kwa sasa kwani huwezi kumwita mwandishi bila ya kuwa na malipo.
Aidha alisema fani hiyo kwa sasa imevamiwa kila mtu ni mwandishi wa habari akeshamiliki kamera hufanya kazi hiyo, bila ya kuwa na elimu au ruhusa kutoka taasisi husika.
Naye meneja wa Jamii Tv Ali Massoud Kombo, alisema ipo haja kwa wateuliwa wa Rais Kisiwani Pemba, kuacha kuwaharasi waandishi wa habari wakati wanapokuwa katika majukumu yao.
Mapema akifungua kongamano hilo, kaimu Mrajisi wa NGOs Pemba Ashrak Hamad Ali, aliwataka waandishi kuendelea kuandika habari za maendeleo, ili kuwasaidia wananchi kwani tanznaia uhuru wa habari upo mkubwa sana.
Alisema wanahabari ni watu muhimu sana katika sehemu yoyote ile, hivyo wanapaswa kuelimisha jamii juu ya suala la uchumi wa buluu, sense ya watu na makaazi.
Akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo, Katibu mkuu wa ‘PPC’ Ali Mbarouk Omar, alisema moja ya jukumu la mwandishi wa habari, ni kuelimisha na kukosoa.
“Kwenye kukosoa, haina maana kuwa uandae migogoro baina ya waandishi na mamlaka husika, bali iwe ni kukosoa kwa aili ya kujenga jamii,’’alieleza.
Hata hivyo aliwataka waandishi wa habari kufuata maadili ya habari wakati wote wanapokuwa akatika kazi zao, sambamba na kuandika habari zinazogusa jamii moja kwa moja.
MWISHO