Thursday, January 16

DAKTARI MWENGINE CHAKE CHAKE KULA SIKUKUU POLISI, NI KWA TUHUMA ZA KUMBAKA MGONJWA WAKE

NA WAANDISHI WETU, PEMBA.
DAKTARI anaetoa huduma kwa wagonjwa kituo cha afya cha serikali cha  Gombani wilaya ya Chake Chake Pemba, Is-haka Rashid Hadid, anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa kaskazini Pemba, akituhumiwa kumtorosha na kisha kumbaka mtoto wa mwenye umri wa miaka 16, mkaazi wa Gombani.
Daktari huyo miaka 35 ni mkaazi wa Kangagani Wilaya ya Wete mkoani humo, ambapo anadaiwa alimchukua mtoto huyo kutoka kwa rafiki yake, na kumpeleka kwenye nyumba anayoishi eneo la Kangagani.
Mtoto aliefanyiwa kitendo hicho alisema kuwa, April 21 mwaka huu alikwenda kituo cha afya Gombani, kwa ajili ya matibabu na baada ya kupatiwa huduma na daktari huyo, alimuomba nambari yake ya simu.
Alisema ilipofika usiku, walikuwa wanawasiliana kupitia ujumbe mfupi (sms) kwa lengo la kwenda kuchukua dawa nyingine ambazo kwa mchana huo alizikosa hospitalini hapo.
“Nilikwenda hospitali kutibiwa, baada ya kufanya mapele katika sehemu zangu za siri, lakini akaniambia mpaka aje daktari fulani, kwa hiyo kesho (siku ya pili yake), atakuja kunichukua ili ukanipe dawa nyingine”, alisema mtoto.
Alisema kuwa, siku ya pili wakati yupo skuli, daktari huyo alimpigia simu na kumeleza kuwa, akirudi skuli amsubiri kwa rafiki yake, mpaka atakapotoka kazini daktari huyo, ili akamchukue kwa ajili ya kumpatia dawa nyingine,
‘’Alikuja kunichukua nikijua naenda kupewa dawa nyingine, kumbe alinipeleka hadi nyumbani kwake Kangangani, ingawa nilipomuuliza, alijibu hana mke,’’alisimulia mtoto huyo.
Mtoto huyo alieleza kuwa, walipofika kwenye nyumba hiyo, waliwakuta vijana wawili, na kumtambulisha kuwa ni ndugu zake, na kisha kabla ya kumbaka alimfanyia uchunguuzi wa virusi vya Ukiwmi.
‘’Usiwe na wasi wasi wowote wewe uko salama na mimi niko salama, hatuna maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, na kisha aliniletea futari na kuanza kupiga,’’alifafanua.
Alifahamisha kuwa, aliishi hapo kwa muda wa siku tano huku akiwa anafanyiwa kitendo cha ubakaji na mtuhumiwa huyo.
“Aliniambia simu niizime, lakini siku ya tano baada ya kuwasha simu alinipigia shoga yangu na kuniambia kwamba wazazi wangu wananitafuta, ndipo nilipompigia simu Is-hak (mtuhumiwa) na kumweleleza”, alisema.
Aidha mtoto huyo alieleza kuwa, daktari huyo (mtuhumiwa) anapokwenda kazini, alikuwa anamfungia mlango, ingawa kwa siku ya tano alimtoa na kuandoka eneo hilo.
Mama mzazi wa mtoto huyo alieleza kuwa, mwanawe aliondoka kwenda skuli, ingawa alikuja kupata wasiwasi kuona ilipofika saa 9:00 jioni, kuwa hajarudi na kuanza kupiga simu kwa ndugu na jamaa wa karibu.
Alisema kuwa, aliporudi mumewe (baba mzazi) akamwambia kwamba mtoto wao hajarudi na ndipo walipochukua uamuzi wa kwenda kituo cha Polisi Chake Chake kutoa taarifa.
“Ilipofika siku ya tano nilimpigia simu nikampata, nikamnasihi arudi nyumbani, aliporudi kabla ya chochote tulirudi tena kituo cha Polisi Chake chake, ambapo awali walipeleka malalamiko,’’alieleza mama huyo.
Alisema kuwa, wakati anamuhoji mwanawe alimwelezea kuwa amechukuliwa na kijana na kumpeleka kwenye nyumba anayoishi katika shehia ya Kangagani na kusema kuwa tayari ameshamuharibu.
Mratibu wa wanawake na watoto shehia hiyo Awena Salim Kombo, alisema kuwa amepokea taarifa ya tukio hilo na kusema kwamba tayari askari wameshakwenda kufanya uchunguzi wa tukio hilo.
“Nilipomuuliza mtoto aliniambia kuwa, daktari huyo alikwenda kumchukua kwa rafiki yake, kwa lengo la kuja kumpa dawa, lakini alipofika ndio alimuweka ndani”, alisema.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Juma Sadi Khamis, alithibitisha kupokea kwa taarifa hizo, na kusema kwamba upelelezi utakapokamilika atatoa taarifa rasmi.
‘’Mtuhumiwa tuna echini ya ulinzi, ambapo tulimpokea akitokea Mkoa wa kusini Pemba, na anaendelea kuhojiwa, baadae taarifa rasmi zitatolewa kwa kina,’’alisema Kamanda.
Tukio linalofafana hili, liliwahi kutokea Novemba 21, mwaka 2019, katika hospitali ya Chake chake, baada ya daktari wa kitengo cha Atrasaund, kudaiwa kuomba rushwa ya ngono kwa mjamzito, kama sharti la kumpa huduma.
Aidha Disemba 18, mwaka mwaka 2019, TBC 1, iliripoti Afisa Muuguzi msaidizi wa kituo cha Afya Mamba mkoani Katavi kushikiliwa na Jeshi la Polisi, kwa tuhuma za kumbaka mjamzito, wakati alipokuwa akimsaidia kujifungua.