Thursday, January 16

WATOTO 89499 kupatiwa matone ya polio Pemba nzima

NA ABDI SULEIMAN.

KITENGO cha Chanjo Pemba, kimesema kuwa lengo la kampeni ya kitaifa ya kutoa matone dhidi ya polio, ni kuhakikisha wanazuia uingizwaji wa ugonjwa wa polio nchini, kulingana na mlipuko uliotokea nchini  Malawi.

Alisema ili kufanikisha lengo hilo ni muhimu kutoa kinga ya polio, kwa watoto wote nchini walio katika umri chini ya miaka mitano (5) ili kuzuwia mlipoko wa Polio.

Akiwasilisha mada kampeni ya utoaji wa matone dhidi ya ugonjwa wa Polio, katika mkutano wa waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali vya habari Pemba, mkutano uliofanyika ukumbi wa Makonyo Chake Chake.

Afisa Chanjo Wilaya ya Chake Chake Fihim Abdalla Mohamed, alisema Kampeni hii ina lengo la kuongeza kinga kwa watoto wote, kwa kuwapatia chanjo ya matone ya polio hata kama wameshapata chanjo hiyo awali.

Alisema tageti yao ni kuwafikia watoto 89499 kwa Pemba, Mkoani watoto 20484, Micheweni watoto 22761, Wete watoto 24018 na Chake Chake ni watoto 22236.

“Ugonjwa wa Polio umekuwa tishio kwa miaka mingi, katika nchi nyingi duniani ikiwemo nchi ya Tanzania, kwa mara ya mwisho Tanzania ilipata mgonjwa Polio mwezi Julai 1996,”alisema.

Aidha alifahamisha kutokana na mwingiliano wa wananchi baina ya Tanzania na Malawi, na tathmini iliyofanywa na Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani (WHO), Tanzania imeonekana ni miongoni mwa nchi zilizo katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa polio endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa,”alisema.

Hata hivyo alisema Ugonjwa huo wa Polio hauna tiba, lakini unaweza kuzuiliwa tu kwa kupata chanjo ya matone au ya sindano na sio dawa nyengine.

Kwa upande wake meneja wa Chanjo Wizara ya Afya Zanzibar Abdullhamid Ameir Saleh, alisema madhumuni makubwa ni kuwapatia kinga watoto wote nchini, kwani kampeni hiyo sio Tanzania tu bali nchi zote zilizozunguka nchi ya Malawi zitafanya kampeni hiyo.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Chanjo Pemba Bakari Hamad Bakari, aliwataka waandishi wa habari Pemba kuhakikisha wanatumia taaluma zao kuelelezea jamii juu ya umuhimu wa chanjo kwa watoto.

Alisema waandishi wanajukumu kubwa la kuelimisha jamii, na jamii ikafahamu umuhimu wake siku itakapofika kuwapelekea watoto wao kupata matonye hayo kwa waliokuwa wahawajazidi miaka mitano.

Alifahamisha katika kutokomeza mripuko wa polio lazima wato matonye ya polio kwa 100% na sio 80, kutokana na hali ya mripuko ilivyo baada ya kuripotiwa kwa mmojwa Malawi.

MWISHO