NA ABDI SULEIMAN.
WANANCHI wa Vijiji vya Chaoni, Gongoni na Hemani shehia ya Wesha Wilaya ya Chake Chake, wamekabidhiwa sadaka ya futari na skukuu ya Eid El Fitr kutoka kwa uongozi wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB).
Waliopatiwa futari hiyo ni wanawake 110 kutoka katika vijiji hivyo vitatu, wamekabidhiwa Sukari, Mafuta ya kula, mchezo na unga wa Ngano.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi futari hiyo, kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Yusuph Juma Mwenda, aliwataka wananchi hao kuhamasiha kudai risiti wakati wanapofanya manunuzi kwa wafanya biashara.
Aidha aliwasihi wananchi hao kuhakikisha wafanyabiashara wanawapatia risiti za kieletorini, kufanya hivyo serikali inapata kodi zake ambazo huzitumia kwa kurudisha kwa wananchi na kutumika kwa shuhuli mbali mbali za maendeleo.
“ZRB hulazimika kurudisha kwa wananchi kile ambacho inakikusanya kutoka kwa wafanya biashara, ili wananchi watambue thamani ya fedha zao zinazokusanywa”alisema.
Hata hivyo Kamishna huyo aliwataka wananchi hao, kupokea sadaka hiyo japo kuwa ni ndogo kwani inaweza kuwasaidia katika kipindi hiki na skukuu kwa ujumla.
Makamishna huyo aliwaomba wananchi wa Kisiwa cha Pemba kuchangia kwa kulipa kodi, ili maendeleo ambayo Rais wa Zanzibar anayokusudia kuyatekeleza kwa wananchi wa Unguja na Pemba yaweze kufanikiwa.
Kwa Upande Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashidi Ali, alimpongeza Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi na Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), kuwasaidia wananchi wasiojiweka kwa kuwapatia sadaka ya Futari katika kipindi hiki cha Mawezi Mtukufu wa Ramadhani.
Alisema kuna wananchi wengi ambao hali zao ni duni na wanahitaji misaada mbali mbali, katika kipindi hiki cha Ramadhani na kuelekea skukuu ya Eid el Fitri.
“Sadaka hii tuliopatiwa leo na wenzetu ZRB ni kurudisha kwa wananchi kile wanachokikusanya, nyinyi mumekuwa taasisi ya kwanza kuwakumbuka wananchi wa vijiji hivi”alisema.
Hata hivyo aliwataka wananchi kuhakikisha wanahamasishana kudai risiti za kieletroniki, baada ya kufanya malipo yoyote kwa wafanyabiashara, kwani kodi inayopatikana hutumika kwa ajili ya maendeleo.
Naye Sheha wa Shehia ya Wete Mohamed Haji Ali, alisema wanawake ndio kundi kubwa linalohitajika kupatiwa misaada mbali mbali katika kipindi hiki cha Ramadhani na Skukuu, kwani ndio walezi wa familia muda wote.
Aidha alishukuru ZRB kwa msaada huo waliowapatia, huku akiahidi kuukabidhi kwa walengwa waliokusudiwa na kuoyomba ZRB kutokuchoka kuwasaidia kila wanapopata muda.
Kwa upande wake Ruksam Rajab Haji aliishukuru ZRB kwa kutoa msaada huo, huku akiwataka wanafanyabiashara kutoa risiti za kieletroniki, pamoja na kutumia mashine za kisasa za utoaji wa risiti hizo.
MWISHO