NA ZUHURA JUMA, PEMBA
UKODISHWAJI wa visiwa vidogo vidogo utasaidia upatikanaji wa soko la uhakika kwa bidhaa wanazozalisha wajasiriamali kisiwani Pemba.
Wakizungumza na Zanzibarleo wananchi mbali mbali kisiwani Pemba walisema kuwa, visiwa vidogo vodogo vitakapokodishwa yatajengwa mahoteli ambapo wamiliki watahitaji bidhaa mbali mbali kutoka kwa wajasiriamali.
Walieleza, yatakapojengwa mahoteli katika visiwa hivyo wanaamini kuwa bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali zitapata soko kutokana na wamiliki wa mahoteli watahitaji bidhaa mbali mbali huku watalii wanapotembea pia watanunua bidhaa hizo.
Mmoja wa wakaazi wa Micheweni Pemba Hadia Hamad Shehe alieleza, Serikali na taasisi binafsi zinaimarisha vikundi vya wanawake na vijana katika shughuli za ujasiriamali, ingawa wanakosa soko la uhakika.
Alifahamisha kuwa, uwekezaji huo utasaidia upatikaji wa soko la uhakika, kwani watalii wataingia kisiwani Pemba kwa wingi kutembea katika visiwa hivyo na nje ya visiwa.
“Wavuvi wanapewa boti lakini hawana sehemu ya kuuzia samaki wao, lakini zitakapojengwa hoteli za kitalii watauza huko, wajasiriamali watauza mikoba, mboga, matunda na bidhaa nyengine”, alieleza
Kwa upande wake mkaazi wa Jadida Wete Halima Mzee Khamis alisema, miradi hiyo itaimarisha kipato cha mwananchi mmoja mmoja, jamii na Taifa kwa ujumla.
Alisema uwekezaji huo unaweza kuipa nchi umaarufu kutokana na watalii wanaoingia, wataitangaza na kuongeza urafiki na mataifa makubwa ambayo yataweza kutoa misaada ya moja kwa moja.
“Hapa wazawa watapata fursa ya kuuza bidhaa tofauti, ikiwemo za vyakula, mikoba, mafuta na dawa zinazotengenezewa karafuu, mkaratusi, mwani”, alifahamisha Mohamed Khamis Shehe mkaazi wa Uweleni Mkoani.
Mratibu wa Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale Pemba Khamis Ali Juma alieleza, mwekezaji hawezi kuimarika kwenye shughuli zake ikiwa hakuwategemea wajasiriamali, kwani wageni watakaofika lazima watahitaji vitu.
“Wajasiriamali watapata tija na manufaa kwa sababu kuna wanaolima bidhaa tofauti, pia wavuvi watauza samaki kwa wawekezaji hao”, alieleza.
Mjasiriamali wa ushonaji wa makawa ya kindu mzima, Khadija Sleyum mkaazi wa Tumbe alisema, watanufaika sana kwani watalii wataingia kwa wingi na watanunua bidhaa zao kwa vile ni za kipekee.
“Makawa, vipepeo na mikoba tunayotengeza inawavutia sana watalii na ni mambo ya utamaduni, hivyo soko litakuwa na sisi tujikwamua kiuchumi”, alisema Khadija.
“Wananchi wawe makini na hili, kwa mfano mwekezaji anahitaji tani moja ya tungule kila siku, ikiwa wananchi watajikubalisha kulima, kutakuwa na soko la kudumu”, anasema Mkuu wa Wilaya ya Wete Dk, Hamad Omar Bakar.
Mratibu wa TAMWA PEMBA Fat-hiya Mussa Said alisema, watalii wanapoongezeka nchini na wajasiriamali wataongeza soko la bidhaa zao ndani na nje ya nchi.
“Mtalii anapoona bidhaa ni mzuri, anaweza kununua na kusafirisha kwenye nchi yao, hivyo soko la wajasiriamali litaimarika na wananchi watanufaika kwa ujumla”, alisema.
Mratibu Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Pemba Haji Khamis Haji alifahamisha kuwa, watahakikisha wajasiriamali wanakidhi vigezo vya kupata mikopo ili waongeze mtaji utakaowasaidia kuzalisha bidhaa nyingi na zenye ubora.
“Mikopo itawasaidia kuzalisha bidhaa nyingi, hivyo wawekezaji watazipata za kutosha, hii itawainua sana wajasiriamali wetu”, anasema.
Mkurugezi dhamana Taasisi ya Viwango (ZBS) Pemba Salim Said Salim aliwataka wajasiriamali kuzalisha bidhaa zenye ubora ambazo zitawapatia alama ya ubora, ili watalii wanunue kwa haraka.
Hata hivyo alisema alama ya ubora ni muhimu sana katika bidhaa zinazozalishwa, kwani wageni wakiziona itakuwa hawana wasiwasi wa kutumia, hivyo ni vyema wazingatie vigezo vyote vinavyotakiwa.
MWISHO.