Thursday, January 16

Mapape wajipanga kufikia malengo.

 

NA ABDI SULEIMAN.

KIKUNDI cha Mapape Cooperative Society kilichopo Mapape Chambani, kimesema kimedhamiria kuongeza ufugaji wa Majongoo bahari na kaa, ili kufikia Majongoo bahari 20,000 na kaa Elfu 8000 hadi elfu 10,000 ifikapo 2025.

Aidha uongozi wa kikundi hicho, umefahamisha kwa sasa wamejipanga kuona malengo yao yanafikiwa, katika kuongeza ufugaji wa Majongoo bahari na kaa, kwani ufugaji huo umekua na soko kubwa kimataifa.

Akizungumza na wamandishi wa habari hizi, katibu wa Kikundi hicho Juma Saidi Ali, alisema ili kufikia malengo na mikakati yao ni kuhakikisha kila mwanachama amekuwa tayari kuona ufugaji huo unaimarika na kuhamisika zaidi.

Katibu Juma alisema mikakati ni kuongeza uzalishaji na kufikia kiwango cha juu, ili kuendana na soko la bidhaa hiyo katika soko la Asia, kwani tani 10 zinahitajika lakini hakuna.

“Hapa kwetu Zanzibar uzalishaji wake umekua ni mdogo sana wafugaji hatuwezi kufikia kiwango kinachihitajika, sisi tumeamua kuongeza uzalishaji hata hivyo pia bado haukidhi,”alisema.

Aidha alisema ufagaji huo unafaida kubwa kijamii, kiafya na hata kiuchumi, ambapo ushirika huo umeamua kuunga mkono juhudi za Serikali katika sekta ya uchumi wa buluu.

“Sababu kubwa iliyopeleka mpaka tukaamua kuanzisha ufugaji huu, kujikwamua na hali ngumu za kiuchumi kwa wananchi na wanachama wetu,”alisema.

Akizungumzia suala la uhifadhi wa Mazingira, alisema kikundi chao kimeamua kupanda miti ya mikoko na ufugaji wa nyuki kwa ajili ya kuhifadhi mazingira ya bahari.

Aidha Juma alisema hilo wameamua baada ya kuona eneo kubwa la bahari limekua ni jangwa, huku maji chumvi yakienda kuathiri maeneo mengi hali iliyowalazimu kupanda miti hiyo.

Akizungumzia changamoto, alisema ni ukosefu wa vifaa vya kutumia kufanya doria na ulinzi katika mashamba yao, suala la wizi wa majongoo na kaa wao, unaofanywa na baadhi ya watu kwa tamaa za haraka.

Omar Khamis Juam mmoja ya wanaushirika, alisema niwakati sasa kwa serikali kuwaangalia kwa jicho la huruka kuwasaidia vifaa vya kisasa, ili kuweza kufanya doria za mara kwa mara katika mashamba yao.

“Sisi tukipatiwa boti moja aina ya faiba na mashine yake imetutosha, tutaweza kufanya ulinzi muda wote hata wakati mwengine kulala huko mashambani,”alisema.

Khakim Haji Mussa alisema kwa sasa mikakati yao ni kuhakikisha wanazungushia uzio kwa kujenga miti katika shamba zima, yote ni kuwalinda majongoo hao.

Naye Maryamu Issa mwanachama wa ushirika huo, aliyomba serikali kuhakikisha wanawapatia vifaranga vya majongoo muda wa kutoa utakapofika katika hachari yake iliyopo beitras mjini Unguja.

Kikundi cha mapape Cooperative Society kilianzishwa mwaka 2021 kina wanachama 30 wanaume 15 na wanawake 15, hadi sasa kina majongoo bahari 60.

MWISHO