Wednesday, January 15

PPC kuadhimisha uhuru wa habaru kwa usafi wa fukwe

NA HANIFA SALIM.

KLABU ya waandishi wa habari wa Pemba (PPC), katika kuelekea maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari, kwa mara ya mwanzo imeamua kufanya usafi katika fukwe za hoteli za kitalii.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mwenyekiti wa klabu hiyo Bakar Mussa Juma alisema, wameazimia kufanya shughuli za kijamii ikiwemo kufanya usafi huo, ili kwenda sababa na adham ya serikali ya mapinduzi ya Zanzibar katika uchumi wa buluu.

Alisema, wameamua kufanya shughuli hizo kutokana na kuiunga mkono harakati za serikali katika sekta ya utalii, ambayo ni nguzo inayosaidia Zanzibar kuingiza pato kubwa la fedha za kigeni kwa zaidi ya asilimia 85%.

“PPC kwa mwaka huu itafanya shughuli zake kwenye fukwe za mahoteli kama vile Ayyana na Mantarif, kwa kuwashirikisha wadau mbali mbali ikiwemo wa uchumi wa buluu, utalii, wizara ya habari, na wakuu wa Wilaya,”alisema.

Alieleza, pia vikundi vya mazoezi vitashiriki kutoka wilaya ya Chake chake na waandishi wa habari watapata fursa ya kufanya mahojiano na maafisa mbali mbali, wakiwemo wa utalii na mambo ya kale uchumi wa buluu na wengineo.

Alifahamisha, fursa hiyo ni ya kipekee kwa waandishi wa habari kupata maoni ya wadau hao juu ya umuhimu wa vyombo vya habari na maendeleo ndani ya nchi yao ya Tanzania.

“Ni hivi karibuni tumeona Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluh Hassan ameitangaza nchi yetu kupitia filamu ya Royal Tour na kwenye eneo moja wapo ni hili ambalo tutalifikia kufanya usafi,” alisema.

Aidha aliwataka wadau ambao wamepata mualiko kuungana nao katika shughuli hiyo muhimu ambayo inaadhimiwa kufanywa na kutangazwa kupitia vyombo mbali mbali vya Zanzibar na Tanzania Bara.

Mratibu wa Klabu ya (PPC) Mgeni Kombo Khamis amesema, wameamua kufanya shughuli usafi kwenye maeneo hayo ili kuunga kono sekta hiyo kwani watu wengi wanapofanya maadhimisho huelekea hospitali na majengo mengine ya taasisi.

Alisema, ni mara ya kwanza kwa makundi ya habari kufanya usafi katika fukwe za mahoteli ya kitalii hivyo, aliwataka viongozi na wasimamizi wa taasisi nyengine kuiunga mkono sekta ya utalii ili iweze kukua na kuleta maendeleo zaidi ndani ya nchi yao.

Maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari huadhimishwa kila ifikapo mwezi mei ya kila mwaka, kauli mbiu ya mwaka huu ikiwa ni “Uwandishi wa habari na changamoto za kidigitali”.

                                      MWISHO.