NA MWANDISHI WETU-PEMBA.
Ofisa Mdhamini wa Wizara ya habari, Vijana , Utamaduni na Michezo Pemba, Mfamau Lali Mfamau amewataka waandishi wa habari kijendeleza kitaaluma za teknolojia mpya ya habari ili kwenda na wakati kwani Dunia inaenda kwa kasi sana , hivyo hawana budi kubadilika ili kuendana kasi hiyo ya kidunia.
Alisema uandishi wa habari unaozingatia takwimu ( Dijital) ni muhimu zaidi kwa ulimwengu wa sasa kwani utaibuwa mambo mpya ambayo yatawavutia wasomaji , wasikilizaji na watazamaji wa vyombo hivyo.
Hayo aliyaeleza huko katika Ukumbi wa Samael Gombani Pemba, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi na wadau wa habari katika maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya habari yaliofanywa kwa ushirikiano wa PPC na Shirika la habari la Internews .
Mfamau alisema kuwa katika uandishi wa habari wa Kidijtal ( Takwimu) ni lazima waandishi kuwa makini katika kuandika habari zao ili kukwepa upotoshaji wa kitakwimu ambao unaweza kuleta migangano isiyokuwa ya lazima.
Alifahamisha kuwa kazi ya uandishi wa habari inathaminiwa sana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani ni muhimu kwa ustawi wa maendeleo ya jamii hakuna mtu atakae juwa mambo mbali mbali yanayotokea Duniani iwe ya kijamii, kisiasa , kiuchumi na kiutamduni ambayo yote ni muhimu .
“ Bila ya nyinyi waandishi wa habari kukamata kalamu zenu , mukaandika habari za matukio mbali mbali yanayotokea Duniani iwe ya aina tafauti tafauti hayawezi kuwafikia wananchi , hivyo ni muhimu kwenu kufanya kazi hii kwa vile mumepewa uwezo kwa mujibu wa katiba”, alisema.
Alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Dk, Hussein Ali Mwinyi imejiweka kuwa ni Serikali ya Uwazi na uwajibikaji jambo ambalo ni fursa kubwa kwa waandishi wa habari kuandika habari zenye maudhui hayo .
Alifahamisha katika hotuba za Rais wa Zanzibar Dk, Mwinyi alikuwa anawakumbusha viongozi aliowateuwa kuwa waadilifu, waaminifu na wawajibikaji hivyo kazi hiyo haiwezi kufanyika kwa ufanisi bila ya ushiriki wa wanahabari na waandishi wa habari kwani wananchi wanataka kusikia habari zinazoelelekeza mipango , maendeleo na vipao mbele vya Serikali .
Aliwataka kutekeleza jukumu lao kwa ufanisi zaidi la kuwahabarisha, kuwaburudisha wananchi na aliwasihi watumie fursa hizo kwa kutekeleza majukumu yao kwa kufuata misingi, kanuni na uhuru walionao kwa kuelekeza mbinu za ujairiamali, ubunifu , fursa za kiuchumi na stadi mbali mbali kupitia vyombo vyao vya habari.
Alilipongeza Shirika la habari la Internews kwa uamuzi wao wa kushirikiana na kuiwezesha Klabu ya Waandishi wa habari Pemba (PPC) kufanya maadhimisho hao kwa kutambua Pemba ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzani.
“ Nilipongeze Shirika la habari la Internews kwa kuamuwa kuiwezesha Klabu ya waandishi wa habari Pemba (PPC) kufanya maadhimisho haya kwani na Pemba ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia wako waandishi wa habari,”alieleza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari Pemba, Bakar Mussa Juma aliwataka waandishi wa habari kuweka mbele Uzalendo pale wanapotekeleza majukumu yao kwa kuyatangaza yale mema yanayofanywa na Serikali inayoongozwa na Dk, Hussein Ali Mwinyi hususan katika maendeleo ya wananchi .
Alisema ni wajibu wa waandishi wa habari kufanya utafiti wa kina kwa kufuata misingi ya uandishi wa habari za kitakwimu ili wanapoandika habari zao wawe na uhakika na kile wanachowalisha wananchi kwenye taarifa zao.
Alifahamisha uandishi wa habari unaendana na takwimu unamvutia msomaji ama msikilizaji kwani unaleta uhalisia wa kile kinachoandikwa hivyo ni jambo muhimu sana kwa waandishi kujikita zaidi katika uandishi huo kwa kujiendeleza kielimu.
“ Ndugu waandishi wa habari kujiendeleza sio tu kwa kukaa darasani bali hata kwenye mitandao , mwandishi anaweza kuibuwa mambo mbali mbali yanayoweza kumsaidia katika kazi zake na pale inapotokea fursa ya kujiendeleza anaweza kupatiwa kuongeza ujuzi zaidi”, alisema.
Mwenyekiti huyo alilipongeza Shirika la Internews kwa kuziwezesha Klabu za waandishi wa habari wakiwe na waandishi mmoja mmoja kuwapatia taaluma mbali mbali zinazowasaidia katika kazi zao za kila siku jambo ambalo limeweza kuwabadilisha kiutendaji.
Hata hivyo alisema Klabu za Waandishi wa habari zitakwenda sambamba kiutekelezaji kwa kufuata ujumbe wa Kidunia wa “ Waandishi wa habari na Changamoto ya kidijital” kwa kuwatafutia mbinu za kujiendeleza katika uandishi huo ili kwenda sambamba na mabadiliko ya kasi ya kidunia.
MWISHO.