Thursday, January 16

HABARI KAMILI YA DAKTARI ALIYEKAMATWA TENA NA POLISI PEMBA HII HAPA

NA HAJI NASSOR, PEMBA

BAADA ya Jeshi la Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, kumuachia kwa dhamana, daktari Is-haka Rashid Hadid wa kituo cha afya Gombani Chake chake, anayetuhumiwa kumbaka mgonjwa wake ambae ni mtoto, hatimea mtuhumiwa huyo amekamatwa tena.

Taarifa zinaeleza kuwa, daktari huyo aliachiwa kwa dhamana ya Polisi baina ya Mei 5 na Mei 6 mwaka huu, na baadhi ya wanaharakati wa haki za wanawake na watoto kulitupia lawama nzito Jeshi hilo.

Walidai kuwa, lililofanyika ni uzembe ndani ya Jeshi la Polisi, hata kama ikiwa mtoto, aliyebakwa na daktari huyo aliwataja watuhumiwa wawili tofauti.

Walisema wanavyofahamu wao, yapo makosa yalioorodheshwa kwenye sheria, kuwa hayana dhamana likiwemo la ubakaji, ingawa Polisi kaskazini Pemba, wanadai walipingana na sheria hiyo.

Kwa wakati huo, wanaharakati hao akiwemo Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii wilaya ya Wete, Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA- Zanzibar walishangaazwa na kitendo cha daktari huyo, kupewa dhamana.

Kamanda wa Polisi Mkoani humo Juma Saadi Khamis, alithibitisha kuwa, wamemkamata tena mtuhumiwa huyo, na wanaendelea na taratibu za kumfikisha mahamamani.

Alisema, ni kweli mtuhumiwa huyo ambae ni daktari, walilazimika kumuachia kwa dhamana ya kipolisi, kutokana na mtoto kuwachanganya, juu ya idadi ya watuhumiwa aliodai kumbaka.

‘’Ni kweli yule daktari ambae tulimuachia kwa dhamana wiki iliyopita, sasa tumeshamkamata tena na wakati wowote atafikishwa mahakamani, kujibu tuhuma zinazomkabili,’’alieleza.

Kamanda huyo alisema, tayari wameshakamilisha hatua za kumuhoji na wakati wowote, jalada lake litafikishwa kwa Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, kwa hatua nyingine.

‘’Kwa wakati ule ni kweli, tulimpa dhamana kwa sababu maalum, na tulimueleza kuwa tukimuhitaji tutamuita na wakati huo umefika na sasa, tunae kwa ajili ya kumfikisha mahakamani,’’alifafanua.

  Kuanzia Mei 1 mwaka huu, Jeshi la Polisi Mkoa wa kaskazini Pemba, lililazimika kumshikilia daktari huyo, kwa tuhuma za kumbaka mgonjwa wake ambae ni mtoto.

Kisha baina ya Mei 5 na Mei 6 mwaka huu, mtuhumiwa alipata dhamana ya polisi, kwa madai ya mtoto huyo, kutaja watu wawili tofauti.

Ambapo Kamanda wa Polisi, alisema walilazimika kumpa dhamana daktari huyo, hadi hapo atakapopatikana mtuhumiwa mwengine.

Awali mtoto huyo aliyefanyiwa kitendo hicho alidai kuwa, Aprili 21 mwaka huu, alikwenda kituo cha afya Gombani, kwa ajili ya matibabu, na baada ya kupatiwa huduma na daktari huyo, alimuomba nambari yake ya simu.

Alisema ilipofika usiku, walikuwa wanawasiliana kupitia ujumbe mfupi (sms), kwa lengo la kwenda kuchukua dawa nyingine ambazo kwa mchana huo, alizikosa hospitalini hapo.

“Nilikwenda hospitali kutibiwa, baada ya kufanya mapele sehemu zangu za siri, lakini akaniambia mpaka aje daktari mwengine, kwa hiyo kesho (siku ya pili yake), atakuja kunichukua, ili ukanipe dawa nyingine”, alisema mtoto.

Alidai kuwa, kisha alimchukua hadi kijiji cha Kangagani wilaya ya Wete, na kumfungia kwa siku tano, na kabla ya kumbaka alimchunguza virusi vya Ukimwi.

Tukio linalofafana na hilo, liliwahi kutokea Novemba 21, mwaka 2019, hospitali ya Chake chake, baada ya daktari wa kitengo cha Atrasaund, kudaiwa kuomba rushwa ya ngono kwa mjamzito, kama sharti la kumpa huduma.

Aidha Disemba 18, mwaka mwaka 2019, TBC 1, iliripoti Afisa Muuguzi msaidizi wa kituo cha Afya Mamba mkoani Katavi kushikiliwa na Jeshi la Polisi, kwa tuhuma za kumbaka mjamzito, wakati alipokuwa akimsaidia kujifungua.

                   Mwisho