NA ABDI SULEIMAN.
MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, amesema kada ya sheria ni muhimu sana katika nchi, kwa kulitambua hilo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, iliamua kutunga sheria mahusisi ya msaada wa kisheria na kuanzishwa idara ya masada wa kisheria chini ya Wizara ya Ofisi ya Rais katiba sheria utumishi na utawala bora.
Alisema idara hiyo imekua ikifanya kazi kubwa katika masuala mbali mbali ya msada wa kisheria Zanzibar, ili kuona wananchi wasio na uwezo wanapata haki zao za kisheria.
Mkuu huyo alisema kada ya wasaidizi wa sheria, inasaidia kwa kiasi kikubwa sana kuwafahamisha wananchi hususan wa ngazi za chini katika jamii, juu ya haki zao za kisheria na namna ya kufuatilia na kuyatafutia ufumbuzi matatizo mbali mbali ya kisheria.
Aidha aliyasema hayo wakati alipokua akifungua mafunzo ya wasaidizi wa sheria Kisiwani Pemba, yaliyofanyika mjini Chake Chake na kuandaliwa na idara ya katiba na msaada wa kisheria Zanzibar.
“Mafunzo haya ni muhimu kwenu washiriki, ili mukitoka hapa muweze kwenda kutekeleza majukumu yenu kwa uweledi na malengo yaliokusudiwa, hizi sheria mutakazofundishwa mukazifanyie kazi kwa vitendo ili kusaidia jamii iliyotuzunguka,”alisema.
Alisema jamii imekua ikikumbana na changamoto mbali mbali, ikiwemo suala la ukosefu wa haki za watu, eneo la ardhi limekua na migogoro mingi sana, ni wakati wasaidizi wa sheria kusaidia na kuelekeza nguvu zaidi katika kuzuwia hii migogoro na sio kutatua.
Akizungumzia sheria ya haki ya mtoto, alisema kwa sasa kumekua na janga katili na hali sio nzuri, matukio mengi na ipo haja kuelekeza nguvu hapo, wadau wananafasi katika mapambano dhidi ya kutokemeza vitendo hivyo.
Kwa upande wa Rushwa alisema matukio mengi yanafanywa katika jamii, wanaoathirika ni wananchi hivyo wasaidizi wa sheria wanapaswa kwenda kuwafahamisha juu ya suala hilo.
Hata hivyo alisema serikali imeweka matarajio makubwa kwa wasaidizi wa sheria, katika kusaidia upatikanaji wa haki kwa wananchi bila ya kujali kipato chao, wadau na wateja wanaokwenda kufanya kazi ni wananchi wa chini wengi wao ni maskini, hivyo wananafasi ya kwenda kuwasaidia wananchi hao.
Mkuu huyo aliipongeza Idara ya katiba na msaada wa kisheria Zanzibar, skuli ya sheria ya Zanzibar kwani kuwepo kwa skuli hiyo ni faraja kwenye kada ya sheria nchini.
Kwa upande wake afisa mdhamini Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais katiba sheria utumishi na Utawala bora Pemba Halima Khamis Ali, alisema idara ya katiba na msaada wa kisheria Zanzibar inajukumu la kusimamia masuala ya kisheria, hivyo wasaidizi hao wamechaguliwa kwa mahitaji ya jamii juu ya masuala ya kisheria.
Alisema uwepo wa wasaidizi hao katika jamii ni msaada mkubwa, kwani jamii inahitaji kusaidiwa kwa hali na mali katika masuala mbali mbali ya kisheria.
Mapema mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria zanizbar Hanifa Ramadhan Said, aliishukuru shirika la LSF kwa kuendela kuwaunga mkono katika masuala mbali mbali ya kisheria.
Alisema mchakato wa kuwapata wasaidizi hao, ulikuwa mkubwa Unguja maombi yalikua zaidi ya 400 na wanaohitajika ni wasaidizi 32, Pemba maombi yalikuwa zaidi ya 200 wasaidizi wanaohitajika ni 18, hivyo wasaidizi hao wanapaswa kuthamini nafasi waliopatiwa.
Aidha alisema licha ya kupatikana kwa wasaidizi 32 unguja na Pemba 18, lakini bado kunahitajika wasaidizi wa sheria wengi ili kufikia shehia zote za Zanzibar.
“Kwa sasa tuna shehia 888 ila wasaidizi wa sheria tulionao ni 205 Zanzibar nzima, tuna shehia 141 hazina wasaidizi wa kisheria Unguja 106 na Pemba 35,”alisema.
Naibu Mkuu wa skuli Taaluma Msemo Mavare, aliwataka wasaidizi hao wa Sheria kuyafanyia kazi kwa vitendo mafunzo hayo, ili jamii iweze kunufaika juu ya uwepo wao.
Akitoa neno la shukurani Mwanasheria kutoka Idara ya Katiba na msaada wa kisheria Zanzibar Ali Haji, alisema mafunzo hayo ni muhimu sana, kwani jamii iliyokubwa inachangamoto nyingi juu ya masuala ya kisheria.
MWISHO