NA HAJI NASSOR, PEMBA
WASAIDIZI wa sheria tarajali kisiwani Pemba, wameelezwa kuwa, moja ya jambo linalowaondoa kwenye usaidizi wa sheria, ni kujiingiza kwenye siasa za wazi wazi.
Hayo yameelezwa na Afisa sheria kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar, Ali Haji kwenye mafunzo yanayoendelea ya siku 15, yanayofanyika Chakechake.
Alisema kila mtu kikatiba yuko huru kuamini dini na hata imani ya chama cha siasa akipendacho, ingawa kwa wasaidizi wa sheria, lazima wajiwekee mipaka.
‘’Ni haki ya kikatiba kushiriki katika masuala ya siasa na hasa kuchagua na kuchaguliwa, ingawa kwenu wasaidizi wa sheria muwe makini na ushabiki wa kupindukia,’’alieleza.
Kwa upande wake Naibu Mkuu wa skuli ya sheria Zanzibar kitengo cha taaluma, Msemo Mavare alisema suala la kuthibitisha jambo mahakamani, lina njia zake kadhaa.
Alisema mfano ni kukiri jambo ‘confession’ pasi na kutenzwa nguvu, kuahidiwa jambo, sambamba na njia ya kuwa na mashahidi.
Hivyo amewashauri wasaidizi hao wa sheria tarajali, kuisoma kwa kina sheria ya ushahidi, ili kuwasidia wananchi wanaowafikia kutaka msaada na ushauri wa kisheria.
“Sheria hii ya ushahidi ni kubwa, lakini hamna budi kuipitia na kuisoma vile vifungu muhimu, kikiwemo cha nani shahidi, aina ya ushahidi pamoja na njia za kutoa ushahidi,” alisema.
Akiwasilisha mada ya njia za unasihi kwa wahanga wa matukio ya udhalilishaji, Afisa Idara ya ustawi wa jamii Pemba Fatma Abdalla, alisema ni eneo linalohitaji ujuzi wa hali ya juu.
Alifahamisha kuwa, shurti moja wapo kwa mtoa ushauri nasihi ni kumjua kwa kina mteja wake, aina ya udhalilishaji aliyofanyiwa na athari.
“Huwezi kuwa mshauri nasihi mzuri, ikiwa hawezi kujenga masuali yanayoweza kukupa taarifa, pamoja na ujuzi wa uchaguzi wa lugha,”alifahamisha.
Mapema wakili wa serikali Seif Mohamed Khamis, aliwataka washiriki hao, kuhakikisha wanaielewa katiba hasa vile vipengele muhimu zaidi.
‘’Kwa mfano Katiba ya Zanzibar yam waka 1984, kuanzia kifungu cha 11 hadi cha 25 kinachoeleezea haki za binadamu, muhakikisha mnavipitia mara kwa mara,’’alishauri.
Baadhi wa washiriki, walisema elimu hiyo ni nzuri ingawa changamoto iliyobakia ni jamii kubadili mtazamo kuwa hilo ni jukumu la serikali pekee.
Mshiriki Juma Seif kutoka jimbo la Chonga, Wahida Kombo Khamis wa jimbo la Chake chake na Fatma Hamad Faki wa jimbo la Wingwi wameahidi kuifikisha elimu hiyo kwa jamii.