Monday, November 25

Hakuna pingamizi yeyote ya kumiliki ardhi, ni kufuata utaratibu, Sheria-DC Abdalla

 

NA SAID ABRAHMAN.

 

MKUU wa Wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Ali, amewataka wananchi hasa wanawake kutambua kuwa hakuna pingamizi yeyote ya kumiliki ardhi, kwa Nchi hii zaidi ni kufuata utaratibu, Sheria na miongozi iliyowekwa.

 

Mkuu huyo wa Wilaya aliyasema hayo mjini Chake Chake, wakati akifungua mafunzo ya Siku moja juu ya umiliki wa ardhi Kwa wanawake yaliyoandaliwa na jumuia ya PECEO, kwa Ufadhili wa The Foundation for civil society.

 

Alisema wanawake wana nafasi nzuri ya kumiliki ardhi, ukilinganisha na takwimu mbali mbali zilizofanywa na ndio wanaopambana katika uzalishaji katika maeneo mbali mbali.

 

“Nimefarajika sana kusikia katika mafunzo yenu haya wapo wenzetu wa Kamisheni ya ardhi, wenzetu wa Wakfu na mali Amana, hawa ndio hasa wanaosimamia masuala yote ya ardhi,” alisema.

 

Aidha alifahamisha kuwa Zanzibar ina usawa katika kumiliki ardhi, anaepaswa kumiliki ardhi ni lazima kufuatwa utaratibu uliopo wa kiserikali, hata wa kidini kwani miongozi ipo ya kupatikana ardhi.

 

“Kwa upande wa dini tunayo mamlaka ya Wakfu na mali Amana, ndio inayosimamia mirathi, pia ipo kamisheni ya ardhi ambayo huwa nayo inasimamia Kiserikali,”alisema.

 

Hata hivyo Mkuu huyo alifahamisha kuwa Serikali imekuwa ikiwasaidia sana, kupunguza migogoro ya ardhi kwa kuweka utaratibu wa kusajili ardhi.

 

“Niwaombe akina mama tuendelee kutafuta ardhi, kwani ndio chanzo Cha shughuli zote za kiuchumi, kijamii na kimaendeleo yoyote ambayo yanafanywa, hakuna maendeleo ambayo yanafanyika juu ya anga,” alisema Abdalla.

 

Alisema hapendi kuona wananchi wanakimbilia mahakamani katika kusuluhishana masuala ya migogoro ya ardhi, badala yake ofisi yake hulazimika kuzisuluhusha pande zilizozozana.

 

“Kwa muda huu tunamaliza migogoro ya ardhi ya miaka iliyopita nyuma na hatupendi kuona Kuna migogoro mipya,”alisema Mkuu wa Wilaya.

 

Hata hivyo Mkuu huyo aliipongeza jumuia ya PECEO Kwa kutoa elimu kwa wanawake, na kuwataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa makini na kufuatilia Kwa Yale yote ambayo watasomeshwa.

 

Akiwakilisha mada katika mafunzo hayo, Yussuf Hamad Kombo kutoka Ofisi ya Mrajisi wa ardhi Pemba, alieleza kuwa tatizo kubwa ambalo linafanywa na wanawake wengi kukosa kumiliki ardhi ni kutokana na uelewa mdogo juu ya umuhimu wa umiliki wa ardhi.

 

Aidha Yussuf alisema kuwa sababu nyengine, inayowafanya kutomiliki ardhi ni kutokana na kiuchumi, kwani wanawake wengi wamekuwa ni tegemezi, pamoja na mfumo dume.

 

Akizungumzia taratibu za kupelekea kumiliki wa ardhi, ni pamoja na kununua na mnunuzi lazima apitie katika bodi ya uhaulishaji wa ardhi na kupatiwa hati, kuruthi na kupewa kama zawadi.

 

Sambamba na hilo,lakini pia njia nyengine ambayo itamfanya mtu aweze kumiliki ardhi ni kurithi ardhi ambapo jukumu la kurithisha limepewa mamlaka ya Wakfu na mali Amana.

 

Nae Massoud Ali Massoud kutoka Kamisheni ya Wakfu na mali Amana Pemba, alisema kuwa hivi Sasa mambo ya urithi wanawake sio sahihi kuwachia wanaume.

 

“Bado wanawake wanahaki ya kurithi na hii haikuanza leo, umeanza tokea kuanza kwa Uislamu, hivyo msikae nyuma na badalaya mudai haki zenu,” alisema Massoud.

 

Nao washiriki wa mafunzo hayo walisema kuwa elimu waliopata wataweza kuitumia ipasavyo na kuitaka PECEO kuendelea kutoa elimu hiyo Kwa wanawake.

 

MWISHO.