SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema pamoja na mafanikio kadhaa yaliyofikiwa katika usawa wa kijinsia na kuongeza idadi ya viongozi wanawake bado nguvu za ziada zinahitajika ili kufikia malengo ya kimataifa na kitaifa katika kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake nchini.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Riziki Pembe Juma aliyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya uongozi wa kimabadiliko kwa makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika katika hoteli ya Marijani Pwani Mchangani.
Alisema Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi wameonesha mfano katika kuleta usawa, kuwawezesha wanawake na kupambana na aina mbalimbali za udhalilishaji sambamba na nchi ya Tanzania kuridhia mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa.
“Uwepo wa utashi wa kisiasa kupitia viongozi wetu wa juu umechochea mafanikio katika kuleta usawa wa kijinsia na uwezeshaji kwa wanawake,” alisema.
Alisema Zanzibar imekuwa na sera inayotoa miongozo ya uzingatiaji wa masuala ya jinsia na uwezeshaji wa wanawake tangu 2001 na hivi sasa kuna sera ya jinsia ya mwaka 2016 ambayo serikali Ina mpango wa kuzifanyia mapitio ili iende Sambamba na mabadiliko ya sera na sheria nyengine.
Akiyataja mafanikio mengine yaliyochangiwa na utekelezaji wa sera hiyo alisema ni kukuza uzingatiaji wa masuala ya kijinsia katika sera na mipango ya kimaendeleo ya kitaifa na kisekta pamoja na kuanzishwa na kuimarishwa kwa program zinazowalenga wanawake.
Mafanikio mengine alisema ni kufanyika kwa mabadiliko ya sheria hususan zinazohusu masuala ya kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia zikiwemo sheria ya jinai namba 6 ya mwaka 2018, sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai namba 7 ya mwaka 2018 na sheria ya mahakama ya kadhi namba 9 ya mwaka 2017 ili kuimarisha upatikanaji wa Haki kwa washirika wa vitendo hivyo ambavyo ninawatokea zaidi wanawake na watoto.
Alisema Zanzibar ikiwa ni sehemu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imeridhia mikataba na maazimio mbalimbali ya kitaifa na kikanda inayolekga katika kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika ngazi zote.
Alisema masuala ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake yamepewa kipaumbele kutokana na umuhimu na mchango wake katika kuondoa umasikini wa kipato na usiokuwa na kipato.
Waziri Riziki alibainisha kuwa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ndio msingi Mkuu wa uzingatiaji wa masuala ya kijinsia na uwezeshaji wa wanawake Zanzibar ambayo imeeleza wazi juu ya haki na fursa sawa kwa wananchi wote.
Aidha alibainisha kuwa baadhi ya mikataba na maazimio hayo ni pamoja na azimio la Haki za binaadamu ya mwaka 1948, mkataba wa kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake (CEDAW 1979), mkataba wa Haki za mtoto (CRC 1989), azimio la Beijing 1995 na azimio jengine muhimu ni la SADC la Jinsia na maendeleo 1997 ambalo linazitaka nchi wanachama kuwa na usawa wa kijinsia na kukuza ushiriki wa wanawake katika masuala ya uongozi na siasa.
Hata hivyo katika kuyafanyia kazi masuala ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake mipango ya kitaifa ya maendeleo ya muda mrefu na muda mfupi kama vile dira ya 2020 ya Zanzibar, Dira ya 2050, MKUZA 1, 11,111 zote zilikuwa na mikakati na viashiria vya usawa wa kijinsia.
Waziri Riziki, alisema ni matarajio yake kwamba washiriki wa Mkutano huo wataweza kuboresha mazingira katika tasisi zao yatakayowezesha matokeo ya usawa wa kijinsia ndani ya sekta hizo pamoja na kuimarisha mashirikiano yatakayopelekea matokeo endelevu.
Sambamba na hayo aliwasisitiza viongozi hao kuhakikisha wanazingatia suala la kujitathimini katika masuala ya uongozi na mifumo iliyokuwepo kwa kutafakari na kuhakikisha kuwa wanazingatiaje masuala ya uongozi na usawa wa kijinsia.
“Nyinyi ndio watendaji wakuu katika mawizara na ipo changamoto ya ubaguzi hivyo ni matarajio yangu kuwa mtakuwa mnasimamia masuala ya kijinsia kwa nguvu zote”, alishauri.
Alisema hatua hiyo italeta Mapinduzi ya uongozi na usawa wa kijinsia hasa kwa wanawake na wanaumme kwani wao ni sehemu ya mabadiliko hayo kwa wanawake na uongozi.
Mapema Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Abeda Rashid Abdalla alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa maslahi ya taifa na jamii kwa ujumla.
Naye Naibu Mwakilishi Mkaazi wa UN Women nchini Tanzania, Julia Broussard, alisema Tanzania bara na Zanzibar imepiga hatua kubwa katika kuimarisha usawa wa kijinsia na kuimarisha uongozi kwa wanawake hasa baadaNaye Naibu Mwakilishi Mkaazi wa UN Women nchini Tanzania, Julia Broussard, alisema Tanzania bara na Zanzibar imepiga hatua kubwa katika kuimarisha usawa wa kijinsia na kuimarisha uongozi kwa wanawake hasa baada ya Rais Samia kuonesha jitihada za kufika kwa lengo hilo na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi kuwa kinara katika kuunga mkono maendeleo ya wanawake.
Alisema UN Women itaendelea kushirikiana na serikali zote mbili katika jitihada za kuishajihisha usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake kufikia maendeleo yanayohitajika hasa katika kupambana na umasikini.
Alisema ni matumaini yake kwamba mkutano huo ambao unajumuisha makatibu wakuu na manaibu utakuja na mikakati imara ya kufikia usawa wa kijinsia na kutatua changamoto zinazojitokeza kwa upande wa wanawake na watoto ikiwemo udhalilishaji na kuongeza idadi ya wanawake katika vyombo vya maamuzi.
Mafunzo hayo ya siku moja yameandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na UN Women.
Imeandaliwa na kitengo cha Habari Wizara Ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto.
|
|
|