Friday, November 15

Milele Zanzibar Foundation yasaidia wanafunzi 44 wa Chuo cha ufundi Kengeja.

NA HANIFA SALIM-PEMBA.

SERIKALI imesema, itaendelea kushirikiana na wanafunzi ambao wamepatwa
na janga la moto katika Chuo cha ufundi Kengeja ili waweze kuendelea
na masomo yao kama awali.

Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Khatib Juma Mjaja aliyasema hayo huko katika
Chuo cha ufundi Kengeja alipokuwa akiwakabidhi vifaa wanafunzi 44 wa
kike, ambao walipatwa na maafa ya kuunguliwa na  moto katika nyumba
wanayolala (Dakhalia) siku ya Mei 16 mwaka huu, vilivyotolewa na
taasisi ya Milele Zanzibar Foundation.

Mjaja alisema, wanafunzi hao ni sehemu ya Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar, hivyo wafahamu kwamba Serikali yao inawajali na kuwaunga
mkono kwa kila hatua ili kuhakikisha wanaendelea na masomo yao na
kubaki salama.

“Janga hili ni Mwenyeezi Mungu mwenyewe ameandika kinachotakiwa ni
kushukuru, mimi naipongeza na naishukuru taasisi ya milele kwa msaada
wake huu ambao una manufaa na nafasi kubwa kwetu,” alisema.

Aidha aliwataka walimu wa saikolojia wa Chuo hicho kuwa karibu na
wanafunzi hao kwani alisema, bado wanahitaji ukaribu mkubwa katika
kipindi hicho kigumu kwao.

Hata hivyo Mjaja aliwataka wanafunzi hao kuwa na subira sambamba na
kushirikiana na walimu wao, wasome kwa bidii ili waweze kutimiza
malengo yao waliojiwekea.

Meneja wa Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation Pemba Abdalla Said
Abdalla alisema, janga hilo si dogo na linamuhusu kila mmoja kwenye
jamii na Serikali hivyo aliwataka wanafunzi hao kurudisha morali ya
masomo yao kwani Serikali ipo pamoja katika kuwasaidia.

“Thamani ya msaada huu ni zaidi ya shilingi milioni 10 bajeti yake ni
ya haraka vifaa nitofauti ikiwemo, mabuku, kalkuleta, kampasi,
vitambaa vya sare na shamba dressing, mikoba, vifaa vya kuchorea
(drowing board) na fedha shilingi 20,000/= kwa kila mwanafunzi kwa
ajili ya kushonea sare zao,” alisema.

Ofisa Mdhamini Wizara ya elimu na mafunzo ya amali Pemba Mohamed
Nassor Salim alisema, msaada huo utaongeza nguvu na kurejesha
uimarishaji wa wanafunzi katika masomo ya wanafunzi hao.

“Wizara ya elimu tunaishukuru milele kwa niaba ya Serikali yetu
imekuwa ikituunga mkono kwa njia mbali mbali asanteni sana,
kilichopungua Ofisi ya Makamu wa Pili kupitia kamisheni ya maafa
imeshatukabidhi fedha kwa ajili ya kukamilisha kilichokosekana,’’
alisema.

Nae Mkurugenzi wa ndani na uratibu wa kamisheni ya kukabiliana na
maafa Pemba Khamis Arazak Khamis alisema, baada ya kutokea janga hilo
kamisheni ilishirikiana na wizara ya elimu ili kuona namna ya kufanya
tathmini juu ya hasara iliyotokea na kinachohitajika.

Alifahamisha, kwa baadhi ya vifaa milele wamejitolea kuwasaidia vyenye
thamani ya shilingi Milioni 10, lakini kwa ambavyo hawajavipata
Serikali kupitia kamisheni imeshakabidhi fedha kwa wizara ya elimu kwa
ajili ya vifaa ambavyo vimebakia.

Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya wanafunzi wenzake mwanafunzi wa
Chuo hicho Sahiba Amour Suleiman aliishukuru Serikali na taasisi ya
milele kwa kushirikiana nao kwa kila hali ili kuhakikisha wanarudi
kuendelea na masomo yao kama awali.

Hili ni tukio la tatu la kuungua moto kwa nyumba za kulalia wanafunzi
(Dahalia) kwa mwaka huu ambapo kwa mara ya kwanza wanafunzi 210
walinusurika kufariki  katika skuli ya Utaani, Madungu na Chuo cha
ufundi Kengeja chenye waafunzi 97.