Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na watoto Mhe Ana Athanas Paul amesema mafanikio makubwa yamepatikana kutokana utekelezaji wa sera ya jinsia ya mwaka 2016 ambayo inatarajiwa kufanyiwa mapitio ili kuleta maendeleo zaidi.
Ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa siku moja kwa Watendaji Wakuu, kuhusu uongozi wa mabadiliko katika ukumbi wa ZURA maisara MjiniUnguja.
Mhe Anna ameyataja mafanikio hayo ni pamoja na kukuza uzingatiaji wa masuala ya kijinsia katika sera na mipango ya kimaendeleo ya kitaifa na kisekta pamoja na kuanzishwa na kuimarishwa kwa programu zinazowalenga wanawake.
Pia mafanikio mengine ni pamoja na kufanyika kwa mabadiliko ya sheria hasa zinazohusiana na masuala ya kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji ikiwemo sheria namba 6 ya mwaka 2018,sheria ya mwendendo wa makosa ya jinai namba 7 ya mwaka 2018 na sheria ya mahakama ya kadhi namba 9 ya mwaka 2017 ili kuimarisha upatikanaji wa haki kwa waathirika wa vitendo vya udhalilishaji ambao zaidi ni wanawake na watoto.
Nae Naibu wa Shirika la Umoja wa Kimataifa linaloshughulika na masuala ya usawa wa kijinsia na wanawake bi Julia Broussard amesema uongozi na mabadiliko ya kimapinduzi yanakuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake pamoja na kumpongeza mama Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake katika kumkomboa mwanamke.
Akiwasilisha maada juu ya Mabadiliko ya Uongozi, Makamu Mkuu wa Chuo Utafiti katika Chuo Kukuu cha Dar es Salaam Profesa Benadeta Killian amesema kiongozi lazima ajitambue na ili awe bora anatakiwa kuongoza kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa wa kijinsia pamoja na kuwashirikisha anaowaongoza katika masuala mbalimbali katika kuleta mabadiliko na maendeleo katika sekta yake.
Imeandaliwa na kitengo cha Habari Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto.