NA ABDI SULEIMAN.
BAADHI ya wakulima wa zao la Mwani katika shamba la Tangini (baharini), kijiji cha Tumbe Wilaya ya Micheweni wamesema kuwa zao hilo limeweza kubadilisha maisha yao, kwa kiasi kikubwa tafauti na miaka ya 1995 walipokuwa wanaaza kulima.
Wamesema kwa sasa hali za maisha yao yamebadilika, kwani wanamiliki nyumba za makaazi walizojenga kupitia kilimo hicho cha mwani ambacho ndio tegemeo kubwa kwao.
Wakizungumza na Timu ya waandishi wa habari, katika ziara iliyoandaliwa na chama cha waandishi wa habari za Mazingira Tanzania (JET), kupitia mradi wa Tuhifadhi maliasili Tanzania unafadhiliwa na USAID, huko katika shamba la Tangini maji makubwa Tumbe.
Fatma Hamad Omar (55) alisema kwa sasa anamiliki nyumba yake ya kukaa, huku akiendelea kuwasomesha watoto wake kupitia fedha anazozipata kutoka katika kilimo cha mwani.
Alisema alikotoka alikuwa hawezi hata kusomesha watoto wake, huku makaazi wakikaa katika nyumba ya familia na sasa mafanikio ameanza kuyapata.
“Mimi nilianza kulima mwani tokea kilo shiriki 20, hadi sasa naendelea na kilimo hichi huku nikiwa na watoto 10, nimewasomesha kupitia kilimo hichi hichi wapo ambao wako JKU na wengine wanaendelea na kusoma,”alisema.
Aidha alisema kilimo hicho kimepelekea mpaka nyumba yake kutia Umeme, huku akisikitishwa na bei ya mwani kwa sasa bado kilo ni shilingi 600.
Akizungumzia Changamoto alisema mwani kwa sasa wanalima mbali, huku wakikosa vyombo vya kisasa vya kuwapeleka maji makubwa ambako ndiko wanakolima.
Naye Mariyam Said Sharif 45, alisema wamelazimika kuitikia wito wa serikali kulima kina kirefu cha mwani, huku wakiwaomba kuwapatia usafiri wa uhakika wakuwafikisha maji makubwa ambayo sasa wamelazimika kulima huko.
Alisema msimu wa bamvua la mwani unapomalizika hufika kupata hadi tani moja, huku akiomba serikali kuongeza bei hadi kufikia shilingi elfu 2000/= kwa kilo moja.
“Hakuna kazi nyengine ya kufanya na sisi hii imekua ndio ajira yetu, kwa kweli tunahatarisha hata maisha yetu hebu tizama nyinyi mumetembea dakika 10 mwa mashine sisi tunaotumia kafi na usafiri huu sio hatari hii,”alisema.
Hata hivyo alisema bado wanahitaji vitendea kazi ikiwemo usafiri, majaketi, viatu, kamba, viboya pamoja na vifaa vypte vinavyohitajika katika kilimo cha mwani.
Kwa upande wake Kombo Subira Kombo, mkulima wa mwani, alisema kila miezi minne huvuna Tania moja ya mwani, huku wakiomba boti za mashine kwa ajili ya kuvulia.
“Kipindi cha upepo huwa ni mtihani kwa wakulima wa mwani, tayari alishatokea mtu kuzama baada ya chombo chake kupakia mwani, kwa kutokua na usafiri wa uhakika,”alisema.
Hata hivyo alisema kwa sasa wamelazimika kulima kina kirefu cha maji, kutokana na maji madogo mwani kuwa na topetope na mwani kuharibika na kutumia muda mrefu kuvuna.
Naye fatma machano Ali alisema kilimo cha mwani kimepelekea kununua charahani kwa kushona nguo, huku wakiumizwa na bei ndogo ya kilo ya mwani.
“Mtu anafanya kazi muda mwingi huku bei ya kilo ikiwa ni ndogo sana, huku wakijitegemea kwa kununua vitu vya aina mbali mbali na manufaa ni ya wote,”alisema.
Msimamizi wa mashamba ya Mwani kituo cha Tumbe, kutoka kampuni ya Sea Wed Cooperation LTd Bosco Huruma Kimambo, alisema suala la bei bado ni changamoto kubwa kwa wakulima mpaka sasa, kwani walaji wakuba wa zao hilo liko nje ya Tanzania.
Alisema katika kipindi cha COVIDI 19 walikuwa na mwani zaidi ya Bilioni moja wameuhifadhi stoo, kwani mwani hauna muda maalumu huku wakiwawezesha wakulima kulima mwani wa kisasa zaidi.
Alisema siku bei ikipanda mkulima atapata mavuno mengi, suala la bei ni kero ya muda mrefu, kwani wapo watu wananunua mwani kilo mia 700 lakini hamsaidizi mkulima kitu chochote.
Kwa upande wake mkuu wa Mwani Pemba kutoka Idara ya maendeleo ya Uvuvi Pemba Asha Khamis Sultani, alisema wakulima wanajitahidi kulima na asilimia kubwa ni wanawake, huku Micheweni ikiwa ni wilaya inayozalisha mwani asilimia 75% kwa zanzibar.
Alisema kwa sasa wakulima wa mwani wanahifadhi mazingira, kwani wameachana na kutumia chupa ambazo ni hatari kwa samaki, huku wakilima mwani kina kirefu na unasaidia kukua vizuri na kuepukana na maradhi.
MWISHO