Monday, November 25

WANANCHI tuendelee kuhifadhi na kulinda mazingira-Mkurugenzi

NA ABDI SULEIMAN.

MKURUGENZI wa Idara ya Mazingira Zanzibar Farhat Ali Mbarouk, amewataka wananchi kuendelea kushajihishika katika suala la uhifadhi wa mazingira, ili dhana ya uchumi wa buluu iweze kueleweka.

Alisema bila ya kuwa na mazingira mazuri ya fukwe za bahari uchumi wa buluu hauwezi kueleweka, hivyo wananchi wanapaswa kuachana na tabia ya kutupa takataka za plastiki katika fukwe.

Aidha mkurugenzi huyo, alisikitishwa na hali ya utupaji wa chupa za plastic katika eneo la bahari ya kivunge, hali inayohatarisha maisha ya viumbe wa baharini ikiwemno samaki.

Hayo aliyaeleza wakati alipokua akizungumza na mwandishi wa habari njia ya simu, kuelekea siku ya mazingira duniani ambayo huadhimisha kila ifikapo Juni 5 ya kila mwaka.

“Hivi karibuni nilifanya ziara ya kuelekea eneo la kivunge, nilisikitishwa na chupa nyingi zimetapakaa, ikizingatiwa wataalamu wamesema ifikapo 2050 kutakua na taka nyingi baharini kuliko samaki, hili ni janga linakuja,”alisema.

Mkurugenzi Farhat alisema hali halisi bado Zanzibar wananchi wanaendelea kuharibu mazingira, ikiwemo uchimbaji mchanga kiholelea, uchafuzi mkubwa wa ukataji wa miti licha ya elimu kuendelea kutolewa.

Alisema uwepo wa miradi mbadala ambayo wananchi watapatiwa, basi wataweza kuachana na uharibifu wa mazingira ikiwemo wavuvi, kuvua kina kirefu cha bahari, baada ya kupatiwa vifaa vya kisasa na kupata cha kujikimu.

Akizungumzia athari za mabadiliko ya tabianchi, alisema zaidi ya maeneo 148 yameathiriwa na mabadiliko hayo, ikiwemo mashamba kuingia maji chumvi, visima kuwa na maji chumvi, matumbawe baharini kuharibika kutokana na joto kuwa kali, ambapo nchi za visiwa ndio waathirika wakubwa wa mabadiliko hayo.

Alisema serikali imekua ikichukua juhudi mbali mbali kwa kujenga tuta eneo la tovuni, msuka bandarini ili kusaidia maji kutokuingia katika maeneo ya kilimo na kufanya shuhuli zao mbali mbali, huku wananchi wakiendelea kushajihisho kupanda miti kwa wingi.

Naye mkurugenzi taasisi ya HUDEFO Tanzania Sarah Pima, alisema jamii kwa ujumla ni wahusika wakuu katika suala la utunzaji wa mazingira, kwani wanapaswa kuyafanya mazingira kuwa salama.

Alisema suala la mazingira sio suala la mtu mmoja, hivyo asasi zisizo za kiserikali bado zinapaswa kuendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya suala la mazingira.

“Upo mkaa mbadala ambapo tunaweza kutumia, ili kulinda miti na kutumia majiko banifu, yataweza kusaidia sana kuhifadhi mazingira,”alisema.

Alisema mpaka asasa wameweza kwuafikia wananchi 42000, kutoa elimu mbali mbali juu ya suala la utunzaji wa mazingira, uhifadhi wa bahari, upandaji wa miti.

MWISHO