NA ABDI SULEIMAN.
WAFANYAKAZI na Viongozi wa Benk ya Watu wa Zanzibar (PBZ) Pemba, wameungana na wananchi duniani katika kuadhimisha siku ya Mzingira duniani, kwa kufanya usafi katika barabara ya Hospitali ya Chake Chake hadi soko la matunda Tibirinzi.
Usafi huo uliwashirikisha pia wafanyakazi kutoka baraza la Mji Chake Chake, kwa lengo la kuweka mazingira safi na salama ya mji wa Chake Chake.
Akizungumza mara baada ya kuamilizika kwa zoezi hilo, meneja wa PBZ Tawi la Gombani Mohamed Mussa Ali, alisema katika kuelekea maadhimisho ya miaka 56 ya kuasisiwa PBZ wamelazimika kurudi kwa jamii kwa kufanya usafi wa mazingira.
“Tumekua tukifanya hivi kwa kurudisha kwa jamii kile ambacho tunakipata, kwa kufanya shuhuli mbali mbali ikiwemo kusaidia vifaa katika hospitali, huduma za kijamii na usafi wa mazingira,”alisema.
Akizunguzmia suala mafanikio, alisema PBZ imepata mafanikio makubwa ikiwemo kufungua matawi katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar na Tananzia bara, pamoja na kuongeza idadi ya mawakala kutoka 500 hadi kufikia 1000 mwisho wa mwaka huu.
Kwa upande wa ATM Mashine, alisema sasa wanamashine hizo 35 huku matarajio yao ni kuongeza hadi kufikia mwisho wa mwaka kuwa na masihne 55, kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi kwa wakati mmoja.
Aidha meneja huyo alisema mawakala wa PBZ, wamekuwa na mchango mkubwa katika kutoa huduma bora kwa wateja wao, hali iliyopelekea kuanzisha shindano kwa mteja atakaefanya miamala mingi kupatiwa zawadi ya bodaboda.
“Siku ya Mazingira duniani imekwenda sambamaba na miaka 56 ya PBZ, ndio maana leo tumeamua kufanya usafi katika maeneo yetu yaliyotuzunguka,”alisema.
Naye meneja wa Islamik Bank Pemba Said Saleh Rashid, alisema Islamiki benk imetimiza miaka 10 tokea kuanzishwa kwakwe, huku ikiwa imepiga hatua kubwa kimaendeleo.
“Benk hii imekua ikifanya kazi zake kwa umakini mkubwa sana, imekua ikipinga suala la riba katika utoaji wake wa mikopo, wananchi wamehamasika kuitumia benk hiyo,”alisema.
Hata hivyo aliwataka wananchi na wazanzibari kuendelea kuiyamini benk yao ya watu wa Zanzibar, kutokana na utoaji wake huduma bora kwa wateja.
Kwa upande msimamizi wa usafi mji wa Chake Chake Masoud Ali Omar, alisema suala la usafi wa mazingira sio la baraza la mji pekee, bali ni la kila mtu kwani anawajibu wa kulinda, kutunza na kusafisha mazingira yaliyozunguka.
Aliwataka wananchi walioko majumbani kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri ya miji yao safi na salama, huku akiushukuru uongozi wa PBZ kwa maamuzi yao ya kufanya usafi katika eneo la mji huo.
Benk ya watu wa Zanzibar imo katika maadhimisho ya miaka 56 tokea kuanzishwa kwake, ambapo kilele chake ni Juni 30 mwaka huu 2022.
MWISHO