NA MWANDISHI WETU.
Wazazi wa Shehia ya Mwembe mchomeke wamesema vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia baadhi yao vinachangiwa na wazazi wenyewe kutokuwa karibu na watoto wao na kutowafuatilia myenendo yao.
Hayo wameyasema wakati wakitoa maoni yao juu ya tatizo la ukatili na udhalilishaji wa kijinsia baada ya kupatiwa elimu juu ya masuala hayo na Maafisa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii jinsia wazee na watoto ikiwa ni muendelezo wa utoaji wa Elimu hiyo katika kila Wilaya.
Wamesema kuna baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwaachia watoto kuangalia TV huku wao wenyewe wakishughulikia masuala mengine hali ambayo mtoto anaweza kuangalia picha mbaya na hatimae kuiga.
Pia wamesema tatizo la mavazi na utandawazi nao umekuwa ukiathiri na kuchangia kuwepo mporomoko wa maadili kwani baadhi yao huiga mambo mbalimbali wanayoyaona na hivyo kupelekea kutokea vitendo hivyo vya udhalilishaji.
Aidha wameshauri kila mzazi kuhakikisha anadhibiti mwenyewe familia yake kwa kuwafuatilia kwa karibu watoto wao na kufuata misingi ya dini inavyoelekeza pamoja na kurudisha malezi ya pamoja ili kupunguza vitendo hivyo.
Pia wameishauri Serikali kuweka adhabu sawa sawa kwa vijana wanaotenda vitendo hivyo kwani wamedai kuwa baadhi yao wanakubaliana wenyewe kufanya vitendo hivyo, huku wanaowadhililisha watoto nao kushauri wafungwe kifungo cha maisha.
Mapema Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Magharibi A, bi Zuhura Abdallah Ali akitoa Elimu ya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia amesema baadhi ya udhalilishaji unatoka ndani ya nyumba zao kwa kuwaita watoto majina mabaya, kuwapiga kipigo cha kupindukia, kuwachoma moto na kuwapa kazi ngumu kinyume na uwezo wao jambo ambalo linawaharibu watoto kisaikolojia.
Pia amesema kuna baadhi ya wazazi wa kiume wamekuwa wakiwatelekeza watoto wao kwa kumuachia mama bila ya kuwahudumia kwa kisingizio cha kumpa talaka hali ambayo inawapa mzigo mzigo mkubwa kina mama juu ya ulezi na kuchangia kuwepo kwa vitendo hivyo vya udhalilishaji.
Imeandaliwa na kitengo cha habari na Mawasiliano Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto.