Saturday, March 15

NA ABDI SULEIMAN.

WASARIFU wa bidhaa zinazotokana na zao la Mwani Kisiwani Pemba, Wametakiwa kuzidisha juhudi, mbinu na bidii katika kuzalisha bidhaa bora zitakazoweza kuingia katika ushindani wa masoko.

Wito huo umetolewa na Afisa Mdhamini Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvivu Pemba Dkt.Salim Mohamed Hamza, wakati alipokua akizungumza na wasarifu wa bidhaa za mawani Kisiwani Pemba.

Alisema dunia hivi sasa imebadilika katika suala la biashara, hivyo wasarifu hao wanapaswa kuzalisha bidhaa zilizokua na ubora ambazo zitaweza kuingia katika ushindano wa masoko huria.

Aliwasihi wajasiriamali hao wa mwani, kuzitumia taasisi za viwango vilivyopo zanzibar ili kuweza kuzalisha bidhaa bora, itakazoweza kutambulika na kupatiwa nembo na taasisi husika.

“Wajasiriamali wengi wanafeli katika kuzalisha bidhaa zenye ubora, kutokana na kutokua na uroho sasa ni vizuri kuwa na uroho wakujifunza zaidi ili kuzalisha bidhaa zitakazoweza kushindana na masoko ya kimataifa,”alisema.

Alisema hivi sasa soko limekua huria, kila mtu analeta bidhaa zake baada ya kufuata sheria na taratibu zilizopo katika nchi husika, hivyo lazima wafanyabiashara wa mwani kujipanga kikamilifu katika kuzalisha bidhaa zao.

Hata hivyo aliwataka wasarifu hao, kuifikisha elimu hiyo kwa wananchi wenzao, kwani bahati walioipata wao ni vizuri kuieneza kwa wananchi wengine.

Naye mratibu wa masuala la Mwani kutoka Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation Pemba Mhando Waziri alisema jumla ya wasarifu wa mwani 50 kutoka Wilaya nne za Pemba wanapatiwa mafunzo ya usarifu bidhaa hizo kisasa zaidi, ili waweze kukidhi ushindani wa soko huria.

Alisema wasarifu hao ni kutoka vikundi 10 vya mwani Pemba, kwani shuhuli wanazozifanya ni muhimu sana ndio maana Milele imeamua kuwapatia elimu hiyo wakulima hao.

Hata hgivyo aliwataka wadau hao, kuhakikisha wanapotoka hapo wataweza kuzalisha bidhaa zilizobora na zinazoendana na makoso ya kisasa.

Kwa upande wao wadau hao wa mwani, wameahidi kuyatumia mafunzo hayo ya usarifu wa mwani, kuwabadilisha katika ufanyaji wa bidhaa zao ili kuendana na ushindani wa masoko hivi sasa.

Wamesema masoko yamekua na ushindani mkubwa katika bidhaa za mwani, kwani zipo nchini nje ya zanzibar nazo zinasarifu bidhaa hizo, hivyo ni wakati kwa wasarifu hao kubadilika katika utekelezaji wa bidhaa hizo.

Katika mafunzo hayo, pia washiriki waliweza kupatiwa vifaa vya kusarifu zao hilo la mwani kisasa zaidi.

MWISHO