Friday, November 15

KILIMO cha vanila kinavyohifadhi mazingira katika maeneo husika

 

                                                                                                                                                                                                     NA ABDI SULEIMAN.

WAKULIMA wa Viungo katika kijiji cha Daya shehia ya Mtambwe Kusini Wilaya ya Wete, wamesema kuwa wataendelea kutumia kilimo hai kwa ajili ya kuhifadhi mazingira katika mashamba yao.

Wamesema bidhaa za viungo wanavyolima lazima viwe katika hali ya mazingira mazuri, hivyo suala la uharibifu wa mazingira katika mashamba yao ni marufuku kufanyika.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika ziara maalumu, iliyoandaliwa na Chama cha waandishi wa habari za Mazingira Tanzania (JET), chini ya mradi wa Tuhifadhi Maliasili Tanzania kutoka shirika la misaada la watu wa Marekani (USAID).

Wamesema biashara za viungo kama vile Vanila, Hiliki, Mdalasini, Mchaichai, Pilipili Manga na karafuu zinahitaji mazingira mazuri, muda wote vinapokuwa shambani.

Mkulima wa michaichai na mdalasini Daya Mtambwe, Amina Ali Mmanga, alisema kuwa wageni wangi wanaofika katika mashamba yao, huvutiwa na mazingira mazuri ambayo yanapatikana katika mashamba yao.

Alisema wamekuwa wakali pale wanapoona wananchi wanaharibu mazingira, kwani mazingira mazuri ya misitu yanapelekea hata vilimo vyao kunawiri ipasavyo.

“kilimo hiki kimetusaidia sana katika kuhudumia familia zetu, yapo mambo mengi tunahudumia familia na wala hatuwaombi pesa waume zetu, ikiwemo baadhi ya vitu vya skuli kwa watoto,”alisema.

Naye Safia Ali Mmanga alisema kabla ya kuingia katika kilimo cha viungo hali za maisha zilikua ngumu, lakini sasa riski yake anapata na kuhudumia watoto wake.

Alisema kwa sasa anatengeneza madogo ya karafuu kwa ajili ya kusafirishia mwili, sabuni za karafuu, kwa upande wa viungo vyengine hulazimika kuvisaga na kuvichanganya pamoja kama viungo.

Kwa upande mwengine aliyomba serikali kuwawekea viwanda vya kusarifu biashaa zao, ikiwemo vanilla na karafuu kwani wanaweza kutengeneza vitu vingi kwa ajili ya jamii.

Naye Fatma Yussuf Said mkulima wa viungo Mtambwe, alisema karafuu inafaida nyingi sana mwilini mwa mwanaadamu, licha ya kutumia katika chai, dawa ya kunywa, pamoja na kuchuliwa mwilini.

Aliyomba serikali kutokuwaacha nyuma wanawake waliojikita katika kilimo cha viungo, kwa kuwawezea kuwapatia mikopo isiyokuwa na riba.

“Tutakapo wezeshwa kwa kupatiwa mikopo na masoko, basi kilimo cha vanilla, mdalasini na michaichai wataweza kuisarifu ipasavyo na kuongeza kipato chao,”alisema.

Hata hivyo aliyomba serikali kuwapatiwa viwanda ili bidhaaa zao za viungo waweze kuzisarifu wenyewe, pamoja na kuongeza thamani kupitia bidhaa zao.

Kwa upande wake Mkulima viungo, na katibu wa kikundi cha Daya Cooperative Society Mohamed Ali Mmanga, alisema kilimo hicho walianza mwaka 1992 hadi sasa bado wanaendelea na kilimo hicho.

Alisema kilimo cha vanilia kina faida kubwa kuanzia mti, mazao wenyewe na mpaka mbegu zake zote kwao ni biashara, kwani kilo moja ya vanilla kavua ni shilling Milioni 1 hadi laki 900,000/=, huku wakiomba serikali kuwapatia soko la uhakika la kilimo hicho.

Alisema kilimo hicho hadi sasa bado wanaendelea kutumia kilimo hai, ambacho hakiharibu mazingira kwa ajili ya kulinda mazingira yaliyozunguka vilimo vyao.

“Sisi hapa miti muda wote ipo katika hali nzuri, kilimo hichi cha viunguo kinahitaji mazingira ya ubaridi baridi na kuvutia ndio maana hapa watalii wakija huvutiwa na mazingira husika,”alisema.

Hata hivyo alisema kilimo chao ni kilimo msitu kwani hawawezi kukata miti, kutokana na vanilla na mikarafuu huhitaji miti mikubwa kwa ajili ya kwenda juu.

Naye afisa Utalii, kutoa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Pemba Khalid Kombo Khamis, amesema Wizara inachukuwa jukumu kubwa sana la kuhamasisha wakulima wa Viungo, vilimo vyote vinahitaji uhifadhi wa mazingira.

Alisema kilimo kinacholimwa ni kilimo hai kwa 100% kinasaidia uhifadhi wa mazingira, kwani hakihitaji kemikali na kwenya mashamba hata hakuhitaji hata mifuko ya plastiki na kulinda afya ya mtumiaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa chama cha waandishi wa habari za Mazingira Tanzania (JET) John Chikomo, alisema baada ya mafunzo sasa ni wakati kwa waandishi kuandika habari kwa wingi zinazohusiana na masuala ya uhifadhi wa malia asili, ikiwemo uhifadhi wa mazingira, wanyama na kilimo cha viungo.

MWISHO

Abdi Juma Suleiman

Journalist/Photographer

Zanzibarleo newspaper
Chake Chake -Pemba
+255774565947 or +255718968355