MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mama Maryam Mwinyi amesema kundi la wajane ni sehemu ya jamii lilosahaulika sana na kulifanya kukosa haki zake.
Mama Maryam aliyasema hayo katika hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Riziki Pembe Juma katika maadhimisho ya siku ya wajane duniani katika ukumbi wa Shekh Idrissa Abdul Wakil Kikwajuni.
Alisema kutokuwepo kwa takwimu sahihi za wajane na kukosa msukumo wa kuzifanyia kazi Tafiti hizo nchini ni moja ya changamoto.
Aidha alisema hali hiyo inasahabisha suala la wajane kuwa lisiloeleweka na kutambulika bayana katika Jamii kubwa zinazoishi na makundi hayo.
Mama Maryam alibainisha kuwa hilo linadhihirisha na ukweli kuwa vitendo vya unyanyasaji na ukiukwaji wa haki za wajane na Watoto wao vimekuwa vikiendelea katika Jamii bila kukemewa wala kuonywa kuwa ni tatizo linalohotaji kupatiwa ufumbuzi.
Hata hivyo alisema uzoefu unaonesha kuwa mara nyingi wajane wamekuwa wakifukuzwa kutoka katika nyumba zao walizokuwa wanaoishi na familia zao baada ya waumme zao kufariki ama kupewa talaka.
Aidha amewataka kina mama kwa nguvu na sauti moja kukemea vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa watoto na wanawake na kuendelea kujikinga ili vitendo hivyo visiendelee kutokea ili watoto na wazazi waweze kuishi kwa Amani bila ya khofu yoyote.
Pia mama Maryam ametoa wito kuzitumia fursa ambazo serikali imekuwa ikizitoa ili kuwanufaisha wanawake wajane waweze kunyanyuka kiuchumi ikiwemo fursa za mkopo wa fedha zinazotokana na Ahueni ya Uviko 19 ambazo zitawasaidia kuanzisha shughuli mbalimbali na kukuza pato la kiuchumi.
Alipongeza jumuiya ya wajane Zanzibar (ZAWIO) kwa kuadhimisha siku hiyo na kuwakweka pamoja wajane ili kuwasaidia katika shughuli mbalimbali za kujikwamua na umasikini.
Mama Maryam amesema kuwa tarehe 23 August ni siku ya sensa hivyo basi ameiomba jamii kukubali kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kukubali kuhesabiwa ili kusaidia Mipango ya Maendeleo ya Serikali na kupatikana kwa takwimu sahihi za wajane ndani ya Nchi.
Naye Mkurugenzi wa Tasisi hiyo Tabia Makame aliiomba serikali kuwaondeshea vikwazo mbalimbali vinavyokwamisha wanawake wajane kupata mikopo na badala yake wapatiwe mikopo hiyo waweze kujiendeleza kimaisha.
MWISHO