Thursday, January 16

Masheha serikali imepiga marufuku risiti za mkono -RC Mattar

NA HANIFA SALIM, PEMBA

MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud amesema, serikali inaendelea kupiga marufuku utoaji wa risiti zinazoandikwa kwa njia ya mkono dhamira yake ikiwa ni kuhakikisha mapato halisi yanapatikana.

Aliyasema hayo katika mkutano wa kuhamashishana na kukumbushana utoaji na upokeaji wa risiti za kieletroniki uliowashirikisha masheha wa shehia mbali mbali Kisiwani Pemba, uliofanyika katika ukumbi wa Bodi ya mapato Zanzibar (ZRB) Gombani Chake chake.

Alisema, risiti zinazoandikwa kwa njia ya mkono ni mfumo wa muda mrefu ambao sio njia sahihi kwani wafanyabiashara wamekua wakiumiza serikali kupitia mfumo huo katika suala la ukusanyaji wa mapato.

“Mfanyabiashara anaweza kuuza 20,000/= akaandika risiti 10,000/= unaweza kukuta mfanyabiashara ana mauzo ya millioni 30,000,000/= kwa mwezi akalipa (ZRB) 80,000/= kwaio wanatuumiza sote serikali na jamii,” alisema.

Alieleza, serikali zote Duniani zinatekeleza miradi yake kupitia kodi hivyo aliwataka wananchi waelewe kwamba kodi zinazokusanywa ndio inayoendesha nchi kupitia miradi mbali mbali ikiwemo, afya, elimu na barabara.

“Masheha munafahamu changamoto zinazowakabili wananchi bila ya kusimamia imara matatizo yataendelea kubakia, tukiimarisha wenzetu wa ndani wa makusanyo basi uwezo wa serikali wa kupanga mipago yake na kutekeleza utakua mkubwa,” alisema.

Aidha alisema, kuna baadhi ya wageni wanalala katika nyumba za hoteli bubu jambo ambalo sio sahihi hivyo aliwaagiza masheha hao wakasimamie suala hilo kwenye shehia zao na kwa mtu ambae atakua na nyumba hizo atalazimika kuirasimisha ili seikali ifaidike na kodi.

Mapema, Mkurugenzi wa Bodi ya mapato Zanzibar (ZRB) Pemba Jamal Hassan Jamal alisema, suala la kusimamia kodi sio la bodi pekee lazima washirikiane na viongozi wa aina mbali mbali kwenye jamii wakiwemo masheha.

“Serikali imeshapiga marufuku utoaji wa risiti mkononi masheha tukaihamasishe jamii tuipeleke taaluma hii wananchi wadai risiti zitakazotolewa kwa mashine maalumu za kieletroniki,” alisema.

Hata hivyo alisema ni kweli kuna ukodishwaji wa nyumba wa hoteli bubu zinazokodishwa na baadhi ya watu kwenye jamii hivyo aliwataka masheha hao wahakikishe nafasi hiyo haipo kwani sio njia sahihi na haifai.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Chake chake Abdalla Rashid Ali alisema, masheha wanajukumu kubwa kwani wao wanashehia zenye wananchi wengi hivyo aliwataka wakasimamie maagizo ambayo wamepatiwa katika kikao hicho.

Sheha wa shehia ya Vitongoji Ali Suleiman Khamis alisema, wafanyabiashara waliowengi hawapo tayari kulipa kodi na wakati mwengine hupunguza bei ya kitu kwa mnunuaji ili wasitoe risiti hivyo aliishauri ZRB kutoa elimu kwa jamii ili iweze kutambua umuhimu wa kupewa risiti.

Sheha wa shehia ya Mkoroshoni Khamis Iddi Songoro aliishauri ZRB kuweka watu kwenye maduka wataochunguza baada ya mtu kupewa huduma akaacha kudai risiti, endapo hatokua na risiti apelekwe kituo cha polisi kulipa faini alisema, tatizo hilo litasaidia serikali kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.

                                      MWISHO.