Thursday, November 14

Mtambwe wa hamasishwa utunzaji wa Amani-PPC

 

WANANCHI wa shehia ya Mtambwe Kinazini Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, wametakiwa kutambua kuwa suala la utunzaji wa amani na Utulivu ni jambo muhimu katika shehia zao.

Hayo yameelezwa na katibu wa klabu ya waandishi wa Habari Pemba (PPC) Ali Mbarouk Omar, wakati wa mkutano wa shehia juu ya umuhimu wa kudumisha Amani na utulivu ya nchi, ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa SAUTI YANGU, AMANI YANGU, HATMA YANGU, unaotekelezwa na wakishirikiana na Foundation for civil society na Search for common groud, kwa ufadhili wa umoja wa nchi za ulaya PPC.

Alisema Amani ndio msingi wa maisha ya kila siku, kwani bila ya amani hakuna linaloweza kufanyika, hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kuitunza na kuithamini amani hiyo.

“Amani inaanza hata majumbani kwetu kwenye familia, kunakochafuka au kuwepo kwa hali ya sito fahamu kila kitu kinakwama na kufanyika nishida, vizuri tukawa watunzaji wazuri wa amani hii tulionayo,”alisema.

Hata hivyo aliwataka vijana kutokukubali kushawishika na kuwa mtari wambele katika vurugu, badala yake wanapaswa kuwa wa kwanza kuelimisha jamii.

Naye mjumbe kutoka PPC Khadija Kombo, alisema sasa Zanzibar inaongozwa na Serikali ya Umoja wa kitaifa, baada ya viongozi wakuu kukubalia na kwa maslahi ya wazanzibari wote.

“Yaliopita yamepita sasa ni wakati wa maendeleo, viongozi wamekua mstari wambele katika kuhimiza maendeleo na kuachana na mambo ya siasa yasio kua na manufaa kwa umma,”alisema.

Kwa upande wake Mchanga Haroub kutoka PPC, alisema katika misingi ya utunzaji wa amani, dosari ndogo ndogo zilizojitokeza zinapaswa zisijirudie tena, hivyo wananchi wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika utunzajihuo.

Aidha alisema wananchi wanapaswa kutumia njia sahihi za utatuzi wa migogoro pale inapotokea katika jamii, na sio kutumia mivutano ambayo mwisho wake inapelekea kubaya.

Seif Salum Abdalla mkaazi wa Kinazini Mtambwe, aliwaomba watendaji wa serikali kuacha kubagua wananchi pale panapotokea miradi mikubwa ya maendeleo badalaya yake kuipeleka katika shehia zote.

Naye Fatma Hamad mkaazi wa Kinazini Mtambwe Kusini, alisema bado wananchi wanaendelea kuwa na hofu juu ya mambo yaliyotokea katika uchaguzi, hivyo aliwaomba viongozi kuachana kutumia nguvu wakati wanapohudimia wananchi, ikizingatiwa zanzibar ina serikali ya umoja wa kitaifa.

Klabu ya waandishi wa habari Pemba (PPC), kwa sasa inatekeleza inatekelezaji wa mradi wa SAUTI YANGU, AMANI YANGU, HATMA YANGU, unaotekelezwa na wakishirikiana na Foundation for civil society na Search for common groud, kwa ufadhili wa umoja wa nchi za ulaya PPC.

MWISHO