NA ABDI SULEIMAN.
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema kuwa inajali na kuthamini nguvu na juhudi zinazotolewa na wadau wa maendeleo, wakiwemo shirika la UNDP kupitia mradi wa LEAP na kuwaomba kuendelea kuwaunga mkono kwa maslahi ya taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Mdhamini Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi na Utawala Bora Pemba, Halima Khamis Ali wakati alipokua akihairisha mafunzo ya siku tatu kwa wasaidizi wa sheria Pemba, juu ya kuwakumbusha sheria mbali mbali ambazo zimefanyiwa marekebisho.
Alisema mradi wa LEAP imeelezwa kuwa unamalizika muda wake, hivyo ipo haja kwa wadau hao wa maendeleo kuendelea kuwashika mkono, kwa maslahi ya jamii kwani bado inahitaji elimu ya sheria kwa kiasi kikubwa.
Alisema taswira ya nzima ya utoaji wa msaada wa kisheria imebadilika, hizo sio juhudi tu za serikali kutambua uwepo wao wasaidizi wa sheria, lakini mashirikiano ndio yaliopelekea kuwepo kwa mabadiliko ya utoaji wa huduma katika fani hiyo.
“Bado serikali inahisi inasababu ya kuendelea kuekeza kwa wasaidizi wa Sheria kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa jamii,”alisema.
Alisema wasaidizi wa sheria ni watu muhimu sana katika jamii, kila kitu ni utaratibu hakuna kitu bila ya utaratibu, kitu kitakacho kwenda kinyume na utaratibu kitafeli.
Mdhamini Halima aliwasihi wasaidizi hao kutii sheria ipasavyo, hakuna utetezi sheria sameheki sheria ni jambo kubwa sana, lazima wasaidizi hao kuwa makini katika nchi watu wote wapo.
Aidha alisema uwepo wao katika jamii utapelekea wananchi wengi kupata haki zao stahiki, hivyo wanapaswa kwenda kusaidia jamii kwa kutumia taaluma walionayo.
Hata hivyo aliwataka wasaidizi hao wa sheria Pemba, kuendelea kufanya kazi kila mmoja kwa eneo lake, kuendelea kushirikiana, kufanya kazi kwa pamoja na kuachana na ufanyaji wa kazi kimazowea.
Kwa upande wake afisa sheria kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar Ali Haji, alisema kutoka kwa mafunzo hayo kwa wasaidizi wa sheria wakongwe, yataweza kuwajengea uwezo na kuwakumbusha mabadiliko ya sheria mbali mbali, ili kuweza kutoa huduma bora za kisasa zaidi.
Naye afisa Sheria kutoka idara hiyo upande wa Pemba Bakar Omar Ali, alisema mafunzo hayo yamejumuisha wasaidizi wa sheria 25 kisiwani Pemba na jumla ya mada tisa zimewasilishwa na wanasheria, huku akiishukuru skuli ya sheria Zanzibar kwa kujuhudi zao za kusaidia wasaidizi wa Sheria Pemba.
Akitoa neno la shukurani Msaidizi wa sheria kutoka Wete Hamad Ali Hamad, aliahidi mafunzo na elimu hiyo waliopatiwa watahakikisha wanaitumia ipasavyo kwa lengo la kusaidia jamii ambayo inahitaji msaada huo.
MWISHO