Thursday, January 16

SITO kubali kuona dereva bajaji au bodaboda anavunja sheria za barabarani-MDHAMINI

NA HANIFA SALIM, PEMBA.

OFISA Mdhamini wizara ya ujenzi, mawasiliano na uchukuzi Pemba Ibrahim Saleh Juma amesema, hatokubali kuona dereva yoyote wa bodaboda na bajaji anavunja sheria zilizowekwa ndani ya nchi.

Alisema, kumekuwa na makosa mengi yanayofanywa kwa baadhi ya waendesha bodaboda ikiwemo kupakia abiria zaidi ya mmoja jambo ambalo hata kanuni imeruhusu kupakia abiria mmoja kwenye chombo hicho.

Aliyaeleza hayo alipokuwa akizungumza na viongozi wa jumuiya za bodaboda na Bajaji Kisiwani Pemba katika mkutano wa kujadili na kuhamasiha madereva kujisajili uliofanyika Ofisini kwake Tibirinzi Chake chake.

Alifahamisha, ni kipindi cha muda mrefu sasa tangu Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi kulirasimisha suala la bodaboda kuwa biashara halali na ndipo Serikali ikaandaa kanuni inayohusiana na masuala hayo.

“Wizara yetu ipo tayari kila siku kuelimisha na kusajili bodaboda kwa sasa tayari tumesajili boda boda 762 kwa Pemba, Mkoa wa kusini madereva wamehamasika sana tunaomba na Kaskazini mufanye ushindani kwenye hili”, alisema.

Alieleza, kwa sasa waendesha bodaboda wanatakiwa kuvaa vikoti maalumu vyenye namba za kuwatambua jambo ambalo ni utaratibu uliowekwa ndani ya kanuni yao.

Hata hivyo alimuagiza Mkuu wa usalama barabarani kufanya doria ya kuwakagua ambao wanakiuka sheria zilizowekwa ili wawachukulie hatua kwa watakaobainika kuvunja utaratibu uliowekwa.

Aidha alisema, waendesha bodaboda wengi wao ni vijana hivyo aliwataka viongozi wa jumuiya za bodaboda watumie busara zao katika kuwafahamisha na kuwaelimisha ili kuonesha mabadiliko makubwa kwenye vituo wanavyovisimamia.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya usafiri na usalama barabarani Pemba Khamis Ali Khatib alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi kwa kuona kuna haja ya kulirasimisha suala la boda boda kuwa halali.

Alisema, mamlaka yao kwa sasa imejipanga vizuri katika utoaji wa taaluma kwa madereva wa bodaboda na ni matumaini yao faida kubwa itapatikana kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Mkuu wa usalama barabarani wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Mkoani Mustafa Mbarouk Hamad alisema, bado madereva wa bodaboda hawajawa tayari kujifunza lakini aliwataka waelewe kwamba sheria yao ni ngumu na lazima wakubaliane nayo.

“Mimi binafsi nilipita kila kituo cha waendesha bodaboda kwa Wilaya ya Mkoani na hakuna dereva aliejitokeza kujisajili, lakini nataka mutambue kuwa mimi kazi yangu ni kukamata na sio kutoa taaluma ya usajili”, alisema.

Hata hivyo Mwenyekiti wa jumuiya ya wandesha bodaboda Mkoa wa Kusini Pemba Kassim Juma Khamis alisema, kikao hicho kitasaidia zaidi nguvu kazi kwa viongozi hao kwani kimeweza kutilia mkazo katika kuendesha shughuli zao.

                                   MWISHO.