NA ZUHURA JUMA, PEMBA
KIJANA Said Ali Nassor mwenye umri wa miaka 28 mkaazi wa Vitongoji Chake Chake, amehukumiwa kwenda kutumikia chuo cha mafunzo kwa muda miaka saba (7) au kulipa faini ya shilingi milioni tano baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kupatikana na unga wa madawa ya kulevya aina ya heroin, yenye uzito wa gramu 17.045
Hukumu hiyo imetolewa katika mahakama ya Mkoa Wete, ambapo hukumu Abdalla Yahya Shamhu alisema mshitakiwa huyo wamemtia hatiani baada kuthibitika kuwa ni mkosa.
Alisema kuwa, baada ya kusikiliza mashahidi wa pande zote mbili, mahakama hiyo imemuona mshitakiwa ana kosa na kumtaka kwenda kutumikia chuo cha mafunzo kwa miaka saba au alipe faini ya shilingi milioni tano.
‘’Baada ya mahakama kupitia ushahidi wa pande zote mbili, imeona kuwa upande wa mashitaka umethibitisha kosa kwa mshitakiwa bila ya kuacha chembe ya shaka, hivyo mahakama inamtia hatiani mshitakiwa huyu’’ alisema hakimu Shamhun.
Kabla ya kusomwa hukumu hiyo mwendesha mashitaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Zanzibar Mohamed Ali Said aliiomba mahakama hiyo izingatie vifungu vya Sheria na adhabu ambavyo vinaendana na kosa hilo, sambamba na kuangatia athari zinazotokea kutokana na matumizi ya dawa za kulevya kwa jamii na Taifa.
Kwa upande wake mshitakiwa alipopewa nafasi ya kujitetea aliiomba mahakama impunguzie adhabu au imfunge kifungo cha nje kwani ana familia inategemea, ombi ambalo limekataliwa na mahakama.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa May 10, mwaka jana majira ya saa 12:00 za jioni huko Mtemani Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, bila ya halali mshitakiwa alipatikana na madawa ya kulevya aina ya heroine yenye uzito wa gramu 17.045, jambo ambalo ni kosa kisheria.
Kufanya hivyo ni kosa kinyume na kifunfu cha 15 (1) (a) cha Sheria ya udhibiti wa madawa ya kulevya nambari 9 ya mwaka 2009 Sheria ya Zanzibar kama ilivyorekebishwa na Sheria nambari 12 ya mwaka 2011 na kifungu cha 24 (a) cha Sheria nambari 1 ya mwaka 2019 Sheria ya Zanzibar.
Kesi hiyo yenye kumbu kumbu namba RM 40 ya mwaka 2021 kwa mara ya kwanza ilianza kusikilizwa Juni 17 mwaka jana katika Mahakama ya Mkoa Wete.