Wednesday, January 15

SERIKALI kupitia Wizara ya Utalii Zanzibar imeanza kuyafanyia ukarabati majengo ya kihistoria kwa lengo la kurejesha uasili wake.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

SERIKALI kupitia Wizara ya Utalii Zanzibar imeanza kuyafanyia ukarabati majengo ya kihistoria kwa lengo la kurejesha uasili wake, jambo ambalo litasaidia kuimarisha utalii kisiwani Pemba.

Akizungumza Chwaka Tumbe Wilaya ya Micheweni, Matibu wa Idara ya Makumbusho Pemba Khamis Ali Juma alisema kuwa, majengo ya kihistoria yamekuja na sura mpya ya utalii, hivyo yakifanyiwa maboresho yatarudi katika uasili wake.

Alisema kuwa, Idara yao ina dhamira ya kurejesha uasili wa majengo ya kihistori kwa lengo la kuimarisha utalii na kurudisha historia kamili, ili vizaji vijavyo viweze kujua.

“Tunafanya ukarabati lakini tunafuata vile vile yalivyo majengo haya na tunatumia zana zile zile, ili yawepo katika uasili wake, hivyo tunaamini kwamba wataimarisha utalii kwani majengo ya historia yamekuja na sura mpya ya kiutalii”, alisema Mratibu huyo.

Alifahamisha kuwa, tayari wameshaukarabati msikiti chooko (msikiti wivu) uliopo Chwaka Tumbe na sasa wanaendelea na msikiti wa ijumaa, ambao kihistoria ndio uliosababisha kujengwa kwa msikiti wivu.

“Msikiti Wivu ni msikiti mdogo ambao tayari tumeshaufanyia ukarabati kwa kuurejesha katika uasili wake na sasa tunaendelea na huu msikiti wa ijumaa na tutahakikisha tunafuata kama ulivyo na tunatumai utakapomalizika watu wataweza kuuswalia”, alisema.

Kwa upande wake Mhandisi Mkuu Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Ali Mbarouk Juma alisema kuwa, lengo ni kurejesha majengo hayo katika hali ya awali bila kuharibu uasili wake.

“Tupo katika hatua ya awali amayo ni ya kuchukua mawazo tofauti kutoka kwa watu wazima wenye umri mrefu ambao wanaufahamu msikiti huu ulivyokuwa, ili kuuweka katika uasili wake”, alisema Mhandisi huyo.

Aidha alimtaka mkandarasi aliekabidhiwa jengo hilo wavunje taratibu sehemu za milango ambayo ilizibwa na watu wa kawaida, ili kuuweka msikiti huo katika sura ile ile ya zamani.

“Huu msikiti ulikuwa na milango lakini imezibwa, kuna alama zinaonesha hapa, hivyo ili uweze kurudi katika uasili wake inabidi itolewe, lakini wajitahidi kufanya pole pole”, alifahamisha.

Nae Afisa Mdhamini Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Pemba Zuhura Mgeni Othman alisema kuwa, wafanyakazi wa Wizara hiyo wanaunga juhudi hizo za kuyarejesha majengo ya kihistoria katika uasili wake na ndio maana wanafanya kazi ya kuondoa kifusi ambacho kilifunika msikiti huo.

“Kile kifusi ambacho kilikuwa kinaanguka chini kiliweza kufunika jengo kidogo, lakini tunafanya kazi ya kukiondosha ili mkandarasi apate kulifanyia maboresho”, alisema Mdamini huyo.

Alieleza kuwa, Wizara imejipanga kurejesha haiba ya maeneo yao ya kihistoria ili kujipatia mapato, kwani watalii watakuja kwa wingi na kujionea majengo hayo.

Aliwaomba wanajamii kushirikiana pamoja katika kuyalinda maeneo ya kihistoria huku wakiepuka kufunga mifugo yao kwani wamekuwa wakiharibu.

Mapema mzee Mwinyi Hassan Shoka mwenye umri wa miaka 95 mkaazi wa Tumbe alisema kuwa, alihadithiwa na wazazi wake kwamba msikiti huo uliezekwa kwa mfumo wa mwamvuli, ambapo ndani ulipambwa kwa vitu vya thamani yakiwemo mabakuli yaliyosarifiwa.

“Ulijengwa kwa mawe, chokaa na mchanga lakini ulikuwa mzima sana kwa sababu huu upo zaidi ya miaka 500 iliyopita na watu waliokuwa wakiishi maeneo hayo wengi wao walihamia Shumba Mjini Micheweni”, alisema.

Alisema kuwa, wanajivunia sana kuwepo kwa majengo ya kihistoria na Serikali imefanya jambo zuri la kurejesha uasili wake, wanaamini kuwa wageni wataongezeka na uchumi utaimarika.

Aliwataka vijana kuhoji historia katika maeneo yao ili waijue vizuri, jambo ambalo litawasaidia wao na vizaji vijavyo.

Msikiti wa kihistoria wa Ijumaa Chwaka Tumbe unafanyiwa maboresho ya kurejesha uasili wake kama ulivyofanyiwa maboresho msikiti chooko ambao ulijengwa baada ya mke mdogo kuona siku zote mume wake anachelewa kurudi na kufikiri kwamba anakuwepo kwa mke mkubwa, jambo ambalo halikuwa sahihi kwani alikuwa na darsa ya usiku katika msikiti huo wa Ijumaa.

MWISHO.