Thursday, January 16

USHIRIKIANO unahitajika zaidi katika kuhakikisha kunakuwa na ukondoishwaji wa masuala ya watu wenye ulemavu, ili wapate haki zao za msingi.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA
USHIRIKIANO unahitajika zaidi katika kuhakikisha kunakuwa na ukondoishwaji wa masuala ya watu wenye ulemavu, ili wapate haki zao za msingi.
Akiwasilisha mada katika mkutano wa Mtandao wa Wilaya wa Mpango Jumuishi wa Maendeleo katika Jamii (CBID), Mshauri kutoka Shirika la watu wenye ulemavu la Norwey (NAD) Christine Cornick alisema, wamekuwa wakifanya kazi na mtandao huo, ili kuisaidia kuleta mabadiliko katika jamii.
Alisema kuwa, ushirikiano wa pamoja ndio utakaoleta nguvu ya kufanya kazi na kuleta mabadiliko ya haraka katika ukondoishaji wa masuala ya watu wenye ulemavu katika nchi mbali mbali.
“Katika mtandao huu tumeshirikisha watu mbali mbali, wanakuwa na sehemu ama mahala ambapo wanakutana na kubadilishana uzoefu katika ngazi mbali mbali na kutoa maamuzi ya kujenga jamii iliyobora”, alisema Mshauri huyo.
Alifahamisha kuwa, watu wenye ulemavu wamekuwa wakikosa huduma zao za msingi, jambo ambalo linasababisha kudharaulika na kudhalilika, hivyo mtandao huo wanaamini utasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto zilizopo.
Mapema Mkurugenzi wa Baraza la watu wenye ulemavu Zanzibar Ussi Khamis Debe alisema kuwa, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ipo pamoja na watu wenye ulemavu kutumia mtandao huo katika kuhakikisha wanafikisha changamoto zinazowakabili sehemu husika, ili ziweze kupatiwa ufumbuzi unaofaa.
“Tunaamini kwamba lengo la taasisi ya malezi na makuzi Bora ya watoto (MECP-Z) ina lengo la kutusaidia na kupata haki zetu sawa na watu wengine, hivyo tushirikiane kwa pamoja ili kufanikisha”, alisema Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi huo Saida Amour alieleza kuwa, watu wenye ulemavu wanakosa usaidizi katika sehemu za kutoa huduma, wanalipishwa nauli mara tatu wakati wanapokwenda safari na pia kuna ushirikishwaji mdogo katika masuala ya michezo.
“Hizi ni changamoto kubwa zinazowakabili watu wenye ulemavu ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi na kuondoshwa kabisa ili wajisikie huru ndani ya jamii”, alieleza Mratibu huyo.
Nae muwasilishaji kutoka SHIJUWAZA Ali Khamis Machano alisema kuwa, watu wenye ulemavu wamekosa elimu ya watu wazima pamoja na ya utunzaji wa fedha, jambo ambalo linasababisha kutoendeleza biashara zao wanazonzisha kwa lengo la kujikwamua kimaisha .
“Watu wenye ulemavu unakuta mara nyingi miradi yao inakwama na hawaendelei mbele, jambo hili linawakwaza sana, hivyo kuna haja ya kupewa elimu ya utunzaji wa fedha”, alifafanua.
Washiriki wa Mkutano huo walisema kuwa, mtandao huo ni mzuri sana, kwani unaunganisha wadau mbali mbali, jambo hilo litasaidia kwa kiasi kikubwa katika kipendekeza na kutatua changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu.
Mkutano huo umeandaliwa na MECP-Z kupitia mradi wa Mpango Jumuishi wa Maendeleo katika Jamii (CBID) kwa ufadhili NAD ambao umefanyika katika Ukumbi wa Kiwanda cha Mafuta ya Makonyo Wawi Chake Chake.