Thursday, November 14

KWA SHERIA HII LINI UHURU WA HABARI UTAHESHIMIWA

MTAALAMU wa uchambuzi wa masuala ya sheria, kwenye mradi wa kuhamasisha mabadiliko ya sheria ya habari Zanzibar Hawra Mohamed Shamte, akiwasilisha juu ya mabadiliko ya sheria hiyo kwa waandishi wa habari Pemba, mkutano uliofanyika katika ofisi za TAMWA Mkanjuni
MWEZESHAJI wa kutoka TAMWA shifaa Said Hassan, akitoa maelezo juu ya sheria hiyo ya habari kwa waandishi wa habari Pemba, mkutano uliofanyika katika ofisi za TAMWA.
BAADHI ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali vya habari Pemba, wakifuatilia kwa makini uwasilishaji wa mada juu ya mabadiliko ya sheria ya habari Zanzibar, mkutano uliofanyika katika ofisi za TAMWA Mkanjuni

KWA SHERIA HII LINI UHURU WA HABARI UTAHESHIMIWA ZANZIBAR

  • WAPAZA SAUTI SHERIA KUFANYIWA MAREKEBISHO

NA ABDI SULEIMAN.

MASUALA ya haki za binadamu yalianza kuingizwa katika mikataba mbalimbali ya kitaifa mwaka 1950, huku Azimio la kulinda Haki za Binadamu Ulimwenguni lilifikiwa mwaka 1984 na Afrika mwaka 1981.

Baada ya hapo mikataba mbalimbali ya kikanda ilipitishwa, kwa dhamira ya kutoa ulinzi wa haki za kiraia na kisiasa, haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, kwa ufanisi zaidi.

Maazimio mbali mbali yaligusia juu ya suala la uhuru wa maoni na kujieleza, likiwemo azimio la UDHR, katiba ya Zanzibar ibara ya 18(1)na(2) kama nayo imeeleza:

18(1)“Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta kupokea na kutoa habari na dhana kupitia chombo chochote, bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati”

(2)kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbali mbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shuhuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii”

Zipo sheria nyingi kwa namna moja ama nyingine zinaathiri uhuru wa habari na haki ya kujieleza kwa mfano sheria ya Usalama wa Taifa, Sheria ya Baraza la Wawakilishi, Sheria ya Takwimu, Sheria ya Makosa ya Mtandaoni.

Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988 kama ilivyorekebishwa na sheria namba 8 ya mwaka 1997

Sheria hii licha ya kuwa kongwe na imekua na mapungufu mengi, yanayokwamisha haki ya uhuru wa vyombo vya habari na uandishi wa habari Zanzibar.

Kifungu cha 27(1)(2)(4), Uwezo wa kukamata magazeti na kupekua majengo.

Kifungu kidogo (1)Ofisa yeyete wa Polisi anaweza kukamata gazeti lolote, popote litakapoonekana, lililochapwa au kuchapishwa, au ambalo kwa maoni yake atalituhumu kwamba limechapwa au kuchapishwa, kinyume na sheria hii.

Kifungu kidogo(2) Hakimu yoyote anaweza kwa hati, kumruhusu ofisa yoyote wa polisi wa cheo cha Mkaguzi au cheo cha juu yake, akiwa na msaada au bila ya msaada, kuingia na kuepuka sehemu yoyote ambayo kwa maoni yake anadhani kwamba limo gazeti lililochapwa au limechapishwa kinyume na sheria hii, limewekwa ndani yake, au kuna kosa limefanywa, linafanywa chini ya sheria hii au kanuni yoyote iliyotungwa chini yake na kukamata gazeti lolote lililokutwa ndani yake, pamoja na ushahidi mwengine wowote wa kosa chini ya sheria hii au kanuni zozote zilizotungwa chini yake unaoweza  kuonekana.

 Aidha kifungu kidogo (4)Gazeti lolote lililokamatwa chini ya kifungu litapelekwa haraka iwezekanavyo kwa hakimu, ambaye anaweza, ikiwa atajitosheleza kwamba gazeti lilichapwa au kuchapishwa kinyume na sheria hii au kanuni zozote zilizotungwa chini yake, au kitu chengine kilitumika katika utendaji wa kosa chini ya sheria hii au kanuni zilizotungwa chini yake kuamuru lichukuliwe au liaangamizwe.

 Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar kwa ufadhili wa Shirika la Internews, kwa sasa wapo katika kufanyia uchechemuzi wa sheria hiyo, katika vifungu mbali mbali ambavyo kandamizi, ili kuweze kupatikana kwa sheria mpya.

WAANDISHI WANAYEPI JUU YA KIFUNGU HICHI?

 Amina Ahmed kutoka Zenj Tv Online, anasema kifungu hicho kinapaswa kufanyiwa marekebisho, kwani kinampa mamlaka makubwa polisi wakati zipo taasisi za kihabari zinazopaswa kusimamia kitu hicho.

Kuwepo kwa mamlaka hayo kutapelekea waandishi, wauzaji, wasambazaji na makampuni kuwatia hofu kila wakati kuhofia kukamatwa.

Naye Asha Mussa ni Mjumbe kutoka PPC, Amesema tasnia ya habari inaenda kuwa mhimili wa nne, kumpa mamlaka polisi au chombo chengine sheria kwenda kufanya upekuzi au kuwaharasi waandishi ni kosa na kuvunja uhuru wa habari.

“Kama kuna mamlaka inahisi gazeti limeaandika vibaya au limekwenda kinyume na sheria za habari, vizuri kufuata taratibu za kisheria na sio kuwakamata moja kwa moja au kuwavamia.

Mwandishi wa habari kutoka Gazeti la Zanzibarleo Pemba Hanifa Salim, anasema Mamlaka hayo  kwa Ofisa wa Polisi anaweza kukamata gazeti atakapojisikia tu kukamata na sio kwa kufanya kosa.

Meneja wa radio Jamii Micheweni Ali Massoud Kombo, anasema sio sahihi kwa Ofisa Polisi kupewa Mamlaka hayo, kwani Uhuru wa habari utakuwa bado haujakuwepo nchini.

“Kama mwandishi amegombana na afisa wa polisi, mitaani na ubarabarani si anaweza kuutumia ugomvi huo kuja kufanya upekuzi na kusababisha sito fahamu kwa waandishi na chombo cha habari.”amesema.

WADAU WA HABARI WAO WANAMTAZAMO GANI JUU YA SHERIA HIYO?

Katibu wa Jumuiya ya PECEO Pemba Juma Said Ali, vifungu vya sheria hiyo haviko sawa na viko kandamizi kwa tasnia ya habari, kwa kutoa mamlaka ya moja kwa moja kwa vyombo vya sheria jambo hilo ni kinyume na katiba ya nchi.

Juma amewashauri waandishi wa habari, vilabu vya habari Zanzibar kuhakikisha wanapaza sauti zao na kuhakikisha sheria hiyo inafanyiwa mabadiliko katika vifungu vyake ikiwemo kifungu cha 27 kifungu kidogo (1),(2) na (4).

Mkurugenzi wa Jumuiya ya Community Forest Pemba Mbarouk Mussa, anasema uwezo uliopo katika kifungu ni mkubwa na unanyima uhuru wa waandishi wa habari na taasisi zao kufanya kazi zao ipasavyo.

“Hii sheria inaonekana ni kongwe sana na imeshapitwa na wakati, sasa ni wakati wa maendeleo lazima sheria hii ifanyiwe mabadiliko makubwa ili iweze kuendana na mabadiliko yaliyopo,”amefahamisha.

Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said, anasema Mamlaka ya Polisi ni kulinda raia na mali zao na amani ya nchi, hivyo mamlaka yaliomo katika kifungu 27 kifungu kidogo (1)(2) na (4) yanapaswa kufanyiwa maboresho.

“Kitakapoboreshwa kifungu hicho, waandishi watakuwa huru kufanya kazi zao za kihabari na wananchi watapata habari, uhuru wa kutoa maoni na kujieleza”, anasema.

MWANASHERIA WANAMTAZAMO GANI JUU YA SHERIA HIYO?

 Ali Amour Makame kutoka Osifi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, anasema kifungu cha 27 kifungu kidogo (1) hakipo sawa na kinanyima uhuru wa habari kwa waandishi na taasisi ya kihabari.

“Kichekesho zaidi anaposema “KWA MAONI YAKE” neno hili halitakiwi liwepo kisheria na kupewa mamlaka makubwa Polisi kama hayo, elimu za Polisi zinajulikana, iweje apewe mamlaka kama hayo mbele ya taaluma nyengine,”amesema.

“habari inaweza kuwa sahihi kutokana kwa mujibu wa Maadili ya waandishi, Polisi huyo isimfurahishe sio sahihi kabisa kumpa mamlaka hayo,”amefahamisha.

Kifungu kidogo(2)kinaenda kinyume na vifungu vya sheria nyengine, ambazo zinaelekeza namna ya kufanya upekuzi na ukamataji wa vitu vinavyodhaniwa kuwa ni makosa, ikiwa ndani ya nyumba, ofisi au kiwanda au sehemu yoyote inadhaniwa kuwepo kitu kama hicho.

Sheria ya Mwenendo wa makosa ya jinai Zanzibar namba 7 ya mwaka 2018, na Sheria ya Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na madawa ya kulevya Zanzibar, zimeweka utaratibu wa kufanyika upekuzi na itambulike sheria yoyote itakayoenda kinyume na sheria nyengine, katika jambo linalofanana itakuwa ni makosa kwa sheria hiyo.

 Sheria hizo zinaelekeza unapofanyika upekuzi na ukamataji wa maeneo kama hayo, ni lazima askari polisi awe na shahidi wawili raia wanaofahamika na kuheshimika katika eneo hilo na washuhudia upekeuzi huo mwanzo_mwisho na lazima wawe wawili sio mmoja.

Anasema askari huyo anatakiwa awe na fomu/Hati maalum ya upekuzi, ambayo ataorodhesha vitu vilivyokamatwa na kuweka saini yake, mashahidi wawili wataweka saini na majina yao pamoja na aliyekamatwa katika fomu au hati hiyo.

“Serikali imepitisha hilo ili kuondoa ukamataji kiholela na uonevu kwa jamii, pia kuwepo kwa shahidi wawili inaondoa ile dhana ya askari kuiba vitu vyengine walivyovikuta ndani humo,”amesema.

Naye Mwanasheria kutoka idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar Ofisi ya Pemba Bakar Omar Ali, anasema kifungu hicho hakipo sawa na kinahitaji kufanyiwa marekebisho, kwani kinaenda kinyume na sheria nyengine za nchi.

Amesema sheria hiyo haiyendani na wakati wa sasa, kwani kuna mabadiliko mengi kwenye masuala ya habari yametokea,tafauti na miaka 25 iliyopita.

“Gazeti kama lina kosa vizuri kusubiriwe litoke kama linapotoka tu ndio pakulikamata, ingekua gazeti limepigwa marufuku nchini na likatoka hapo munaweza kuja kunipekua,”alisema.

VIONGOZI WA VYOMBO VYA HABARI WANAMTAZAMO UPI?

 Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar Ali Haji Mwadini, anasema sheria inanyima uhuru wa waandishi wa habari kufanya kazi zao vizuri na kikamilifu.

“Ukamataji na upekuzi wowote lazima kwanza ufuate taratibu na sio mtu au kiongozi kukurupuka na kuvamia, sheria hiyo sasa vizuri nayo ikafanyiwa mabadiliko ili iendane na wakati.

Afisa Mdhamini Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Pemba Mfamau Lali Mfamau, anasema kifungu cha 27 kifungu kidogo cha (1)(2) kuwa kiko sawa kwa sawa, mwenye mamkala ya kukamata ni jeshi la polisi, ila watu wa habari vinawapa ukakasi na ni vyema kuweka wazi hilo tatizo na kwenda kushauri sherikalini.

“Kwa sasa Wizara ipo katika mchakato wa sheria ya waandishi wa habari, iko jikoni inapika ikitoka mapungufu mengi yanayojitokeza yanaweza kuwa muarubaini wa matataizo hayo,”amesema.

TAASISI ZA KIHABARI ZINASEMAJE JUU YA SHERIA HIYO?

Mjumbe wa Kamati tendaji kutoka Pemba Press Club Gaspary Chales, amesema Shria kumpa nguvu ofisa wa polisi uwezo wa kukamata na kufanya upekuzi, ni kipimo kikubwa cha ukiukwaji wa uhuru wa habari nchini.

“Sheria haijaweka wazi vigezo gani ambavyo vinaingia kwenye orodha ya makosa ya uvunjifu wa sheria, ila imesema anaweza kutumia mamlaka ya kisheria kukamata gazeti kwa

maoni yake binafsi bila kujali ni kweli au laa na pasipo kishauriana na mtu yeyote,”amesema.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania(MCT) Kajubi Mukajanga, anasema waandishi wasipozielewa sheria zao, mchakato wa kupitisha utakuwa kwenye mikono ya wanasheria na wanasiasa na hivyo watapendekeza wanavyotaka.

MKATABA WA HAKI ZA BINAADAMU WA DISEMBA 10/1948 UNASEMAJE

katika mkataba huo ibara ya 19 inasema, kila mtu ana haki na uhuru wa kutoa maoni na kujieleza, haki hii inajumuisha uhuru wa kuwa na maoni bila kuingiliwa na kutafuta, kupokea na kutoa habari na mawazo kupitia chombo cha habari bila kujali mipaka.

NINI KIFANYIKE

Juma Omar Khamis anasema ni wakati sasa kwa sheria hiyo kufanyiwa marekebisho, katika vifungu vyote vinavyoonekana vinakandamiza waandishi wa habari na uhuru wao.

“Kutokana na baadhi ya vifungu kukinzana, tunasema bado uhuru wa habari umebanwa vizuri waandishi kuwa huru na kufanya kazi zao na vyombo vyao bila ya kuingiliwa,”amesema.

Salma Khamis Juma anasema kifungu kieleze ufasaha wa vitu ambavyo vikitokea gazeti linapaswa kupekuliwa au kuvamiwa, na sio kuficha jambo linalowatia hofu waandishi.

Shaban Ali kutoka Redio jamii Micheweni amesema, kuwepo kwa sheria hiyo imekua ni changamoto kwa waandishi, sheria kuibadilisha na badala yake afisa wa polisi kama kuna jambo kuomba kwa maandishi ili kuhakikisha anapewa anachokitaka.

MWISHO