NA MARYAM SALUM, PEMBA
WAZIRI wa Biashara , Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Omar Saidi Shaaban alieleza kuwa siku ya Ushirika duniani ni moja ya tukio muhimu sana kwani inakwenda sambamba na mikakati ambayo Serikali imejiwekea kwakuwasikiliza Wananchi kupitia makundi yao na hasa wanaushirika.
Hayo yalielezwa na Waziri huyo kwa niaba ya Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Mudrik Ramadhan Soraga, kwenye hafla ya maadhimisho siku ya kilele cha siku ya Ushirika Dunianai katika Uwanaja wa Michezo Gombani Chake Chake, iliyowashirikisha Viongozi mbali mbali wa Serikali pamoja na wanaushirika kutoka kwenye mikoa miwili ya Pemba.
Alisema kuwa siku ya kilele cha Ushirika duniani ni tukio kubwa kwani inatoa fursa yakuwakutanisha pamoja wananchi na wanaushirika kwa ujumla katika kujadili mafanikio, kutatua changamoto zao katika vyama vyao na kupeana elimu zaidi juu ya shuhuli zao zinazowakabili .
“Nawapongeza wanaushirika kwakuungana na wanaushirika wenzenu duniani, katika kufanikisha kilele cha siku ya Ushirika duniani kwani mikusanyiko hii hutoa fursa ya kupeana elimu, ushauri kwa jinsi ya kuimarisha utendaji wa vyama vyao na kuleta ufanisi sio tu kwenye vyama vyenu bali pia kuchochea maendeleo ya vyama na jamii kwa ujumla,” alisema Waziri Omar.
Alieleza kuwa vyama vya ushirika ni taasisi muhimu sana na ni vya hiari vyenye uwezo wa kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii kuleta ustawi wa maisha yenye neema, kwani vyama hivi vinatoa fursa kwa wanachama kujiajiri na kutoa fursa kwa wengine.
“Vyama hivi vinaouwezo mkubwa sana wakuongeza wazalishaji mali, kwa bidhaa, pia kutoa huduma kama vile za fedha, makaazi, na usafiri, kupitia vyama hivi ni rahisi kuzalisha bidhaa zenye viwango bora kwa matumizi ya watu, pia ni vyama vikuu vinavyorahisisha katika upatikanaji wa mitaji, elimu na matumizi ya teknolojia yakisasa pamoja na kufaidika ununuzi na mauzo ya jumla,” alieleza.
Alifahamisha hii inamaana kwamba kupitia vyama vya ushirika tutaongeza nguvu zaidi ya ushindani wa masoko ya ndani ya kikanda kama vile SADEC na KOMESA hadi masoko ya kimataifa.
Alifahamisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayodhamira ya dhati ya kuimarisha uchumi wa buluu, hii inamaana kwamba kwakutumia rasilimali zilizopo baharini huleta Mapinduzi ya kiuchumi nchini.
Wazir Omar alieleza, kuwa Vyama vya Ushirika vinanafasi na fursa kubwa sana kushiriki katika kutekeleza shuhuli za kiuchumi zinazoambatana na uchumi wa buluu, kama vile uvuvi wakati na wa bahari kuu ufugaji wa mazao ya baharini, usarifu wa mazao ya baharini na Kilimo cha mwani.
Aidha alieleza kuwa vyama vya ushirika vinaouwezo mkubwa wakuendeleza uzalishaji wa mazao mbali mbali ya Kilimo kama vile mboga, matunda maziwa, na mazao ya mizizi na mifugo mengine, ni dhahiri kuwa vinachangia kwa kiwango kikubwa kuilisha jamii na wawekezaji wanaokuja kuwekeza katika Miradi ya shuhuli mbali mbali nchini.
Hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi, ambapo SACCOS zinamchango mkubwa wa kusambaza na kuimarisha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi kwa urahisi na unafuu zaidi.
Alisema Serikali inathamini sana mchango wa wanaushirika katika kuimarisha hali ya maisha ya wananchi kiuchumi na kijamii,hivyo ni matumaini yao kuwa kupitia mikusanyiko hiyo, elimu na mafunzo yanayotolewa yatasaidia kuimarisha uendeshaji wa vyama na kuona kwamba vyama vya ushirika vipo imara kimuundo na uendeshaji vyenye kuhimili hali ya ushindani uliopo katika soko huria.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Ali kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa huo Mattar Zahor Massoud alisema kuwa wanaushirika ipo haja kuendelea kuwa na imani na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, katika kuendeleza vyama vyao Kiuchumi.
“Vyama vya Ushirika vifahamu kwamba Serikali imejijengea imani yakutosha na wanaushirika katika kujikwamua kwenye masuala mbali mbali hususan yakiuchumi, kwani Serikali imetenga shilingi Bilioni Thelathini na mbili kwa ajili ya wanaushirika, hivyo fedha hizo ziweze kutumika vizuri ili kufikia malengo yaliyokusudiwa,” aliseleza .
Hivyo kwa vile ni ushirika, ni umoja basi wanaimani watayafikia malengo yote yaliyokusudiwa juu ya fedha hizo.
Nae Katibu Mkuu Ofisi ya Rais aliekuwa wizara ya kazi uwezeshaji Khadija Khamis Rajab alifahamisha kuwa lengo kuu la maadhimisho ya ushirika duniani ni kuwapa fursa zaidi wanaushirika kukutana pamoja kubadilishana mawazo na kupeana elimu zaidi ya shuhuli zao.
Alieleza kuwa kuwepo kwa mikusanyiko hiyo wanaushirika hupata nafasi nzuri ya kujadili changamoto zao zinazowakabili, na kufikia yale malengo waliyojipangia.
Mapema akisoma risala ya wanaushirika Katibu mtendaji Muungano wa vyama vya ushirika Zanzibar (CUZA), Suleiman Ame Mbarouk alieleza kuwa wanaushirika wanaimani kubwa na Serikali, hivyo kuunga mkono Serikali kwenye dhana ya Uchumi Buluu kwa upande wauzalishaji wa baharini.
Alisema ipo haja kwa wanaushirika kushirikishwa kwenye uchumi wa buluu, kwani bado hawajaona kushirikishwa kwenye uchumi huo katika utekelezaji Mradi huo ingawa si mara ya kwanza kupelekea kilio hicho.
Hivyo aliishukuru Serikali kwa kuwasaidia wanachama wa Ushirika Zanzibar, ambapo sasa Ushirika wa Kilimo cha mihogo kimeshasajiliwa Pemba.
Siku ya kilele cha Ushirika Duniani hufanyika kila ifikapo July 2 ya kila mwaka, ambapo Ujumbe wamaka huu ni USHIRIKA HUJENGA DUNIA ILIYOBORA ZAIDI”.