Thursday, January 16

MWAKILISHI AKABIDHI VIFAA KWA MASKANI TONDOONI

MWAKILISHI wa Jimbo la Wawi Bakar Hamad Bakar, akizungumza na wananchi wa tawi la CCM Mvumoni jimbo la Wawi, mara baada ya kukabidhi mifuko 20 ya saruji, madirisha nane na milango kwa ajili ya maskani ya CCM Mvumoni.(PICHA NA ABDI SULEIMAN)
MWAKILISHI wa Jimbo la Wawi Kisiwani Pemba Bakar Hamad Bakar, akimkabidhi madirisha nane katibu wa Tawi la CCM Mvumoni Zena Ali Hamad, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa kwa wananchi wa tawi hilo wakati akiomba kura 2020.(PICHA NA ABDI SULEIMAN)
MWAKILISHI wa Jimbo la Wawi Kisiwani Pemba Bakar Hamad Bakar, akimkabidhi mifuko ya saruji kwa katibu wa wa Tawi CCM Mvumoni Zena Ali Hamad, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa kwa wananchi wa tawi hilo wakati akiomba kura 2020.(PICHA NA ABDI SULEIMAN)

 

NA HANIFA SALIM.

 

MWAKILISHI wa jimbo la Wawi Bakar Hamad Bakar, amekabidhi vifaa vya kukamilisha ujenzi wa tawi la CCM shehia ya Mvumoni, ikiwemo saruji mifuko 20, mchanga, madirisha nane na milango ikiwa ni utekelezaji wa ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni mwaka 2020.

 

Akikabidhi vifaa hivyo kwa wanachama wa chama cha Mapinduzi CCM shehia ya Mvumoni Mwakilishi huyo amesema, vifaa hivyo ni kutekeleza ahadi ambayo aliieka kwa wanachama hao endapo watamchagua.

 

Alieleza, wananchi wa shehia ya mvumoni ni mashahidi wa kuwa jengo hilo si ahadi yake ya kwanza, kuitekeleza bali ni muendelezo kwani kuna baadhi ya kazi zimeshatangulia kufanywa na mengine yataendelea kama ambavyo aliawaahidi.

 

“Ndugu wanachama katika uchaguzi wa mwaka 2020, nilipita kuomba kura zenu niliahidi mambo mingi ikiwemo ujenzi huu wa tawi la Mvumoni, na nyinyi kwa imani yenu mulinichagua kutokana na ahadi zangu nilizozitoa kuwa munazihitaji,” alisema.

 

Alisema, aliahidi kuling’arisha tawi la CCM shehia ya Mvumoni kwa kulitia madirisha, milango, kulipiga plasta nje na ndani, kupakwa rangi, ili liweze kukalika vizuri na wanachama wa chama cha Mapinduzi wafanye shughuli zao katika mazingira yanayoridhisha.

 

“Barabara yetu haikua vizuri sote tunalijua hili, ilikua na mashimo makubwa ni changamoto hata kwa wagonjwa wanaokimbilia hospitali, lakini sasaivi iko kwenye kiwango, skuli yetu ya furaha tayari tumefikia hatua ya kuezeka banda la watoto la kuwapikia uji na hata msikiti wetu tulikua na shida ya maji tumejenga tangi la kuhifadhia,” alisema.

 

Aidha, aliwasisitiza wananchi wa Mvumoni waendelee kumuunga mkono, ili aweze kutekeleza ahadi zake alizozieka kwa wananchi na kuwataka pale ambapo hawamuoni, katika shehiya hiyo watambue kuwa anatekeleza ahadi kwenye shehia nyengine.

 

Aidha aliwanasihi wananchi waendelee kumuunga Mkono Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwani anapambana kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo sambamba na kuwataka wanamvumoni kujitokeza kuhesabiwa katika sensa.

 

Katibu wa umoja wa vijana UVCCM Wilaya ya Chake chake Changarawe Makaranga, alimpongeza Mwakilishi wa jimbo la wawi kwa kutekeleza ahadi zake, ambazo alizieka kwa wananchi wakati akiomba kuchaguliwa kuwa mwakilishi wa jimbo hilo.

 

“Wanachama wa CCM wasikivu ndio maana wanafanya ambayo wanahitaji wananchi wao, tumepata kiongozi bora anaetimiza ahadi kwa wakati hivyo tumuunge mkono ili aendelee kufanya kazi zake zaidi,” alisema.

 

Kwa upande wake Katibu wa Wadi ya Kibokoni Khamis Mohamed Abdalla alisema, mvumoni ya sasa ni ya maendeleo wanachama wa chama cha Mapinduzi CCM wapo imara, wasikivu na wenye kujituma.

 

Nae Mwenyekiti wa Tawi la CCM Mvumoni Mohamed Abdi Said alisema, wanachama wapo imara, wapo tayari kukitumikia chama chao kwa kila hali ili kiweze kusonga mbele.

 

Mwakilishi wa jimbo la Wawi amekabidhi milango 2, madirisha 8, saruji mifuko 20, mchanga, pesa kwa ajili ya kuwalipa mafundi kwa lengo la kuing’arisha tawi la chama cha Mapinduzi CCM shehia ya Mvumoni Chake chake Kisiwani Pemba.

 

                            MWISHO.