Wednesday, January 15

‘Khamis’ kisiwa kidogo kilichobeba historia ya Pemba

MOJA ya kisiwa kidogo kilichopo Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, kiitwacho kisiwa Ndege (Kisiwa Khamis) ambacho mwanzoni mwa mwaka huu kimetangazwa kama ni kivutio kipya cha kiutalii
BOTI aina ya mashua iliyobeba watendaji wa wizara ya utalii na ambo ya kale akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya wakielekea kisiwa ndege kwa ajili ya kukitangaza rasmi kuwa ni kivutio kipya cha utalii.

‘Khamis’ kisiwa kidogo kilichobeba historia ya Pemba

  • Utalii yakiibua kama kivutio kipya, kina ndege aina 12

NA HANIFA SALIM, PEMBA

Ni takribani dakika 25, kutoka katika ufukwe kwa bandari ya Tumbe, hadi kufikia kwenye kisiwa cha Ndege ‘Khamis’ kilichopo katika eneo la Tumbe ndani ya bahari ya Hindi.

Ilikuwa majira ya saa 3:00 asubuhi, boti iliyobeba maafisa wa wizara ya utalii na mambo ya kale, ikiwasili katika kisiwa Ndege kinachojulikana kwa jina la (kisiwa khamis).

Hali ya hewa ilikuwa ni ya mawingu mawingu, kutokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku mzima wa kuamkia siku hiyo, boti hiyo aina ya mashua, ilibeba takribani ya watu 30.

Katika msafara huo, jemedari wa Wilaya hiyo Mgeni Khatib Yahya amekiongozana na mwenye dhamana ya Wizara ya utalii na Mambo ya Kale Pemba Zuhura Mgeni Othman, na maafisa wengine.

Safari hiyo, haikubeba maafisa hao, tu bali ilikua na watu ambao wanaipasha jamii habari, kutoka vyombo mbali mbali vya habari.

Ziara hiyo, iliyofanywa na Wizara ya Utalii, ilikua na lengo la kutembelea kisiwa hicho, kukitangaza rasmi kiutalii, kikiwa ni kivutio kipya.

Kwani, kwa miaka zaidi ya miaka 70 iliyopita, hakikuwemo kwenye orodha ya vivutio, ambavyo vimetambuliwa Kisiwani Pemba.

Kilipo kisiwa ‘Khamis’ ni takribani ya kilomita 3, hadi ilipo bandari ya Tumbe Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Kisiwa hicho chenye urefu wa wastani wa viwanja viwili vya mpira wa miguu ‘mita 230’ kikiwa na upana wa kiwanja kimoja na nusu cha mpira wa miguu ‘mita 160’.

Miti mirefu mchanganyiko, iliyotawala ubichi iliyojengeka kwa vichaka na hali ya hewa mwanana, huku ukikaribishwa na miito ya ndege aina 12, ndio mandhari inayowavutia wageni na wenyeji.

AINA YA NDEGE WALIOPO KISIWA KHAMIS

Kisiwa Khamis, umaarufu kisiwa ndege, kimechota aina 12 ya ndege 12 wakiwemo Yangeyange, Makoho, Vijafara, Membe, Chozi, Mwewe, Jimbi msitu, Visengenya na Chozi jabiri.

Aina hii ya ndege 12 waliopo katika kisiwa hicho, wala sio rahisi hata kidogo kuwakuta ndani eneo jengine pasi na kisiwa hicho.

IDARA YA MAKUMBUSHO NA MAMBO YA KALE PEMBA

Khamis Ali Juma, ambae ndie Mratibu wa Idara hiyo, anakiri kuwa, upya wa ugunduzi wa kisiwa hicho, bado ni mapema kuelezea sababu ya kuitwa kisiwa ‘Khamis’.

Ijapo kuwa wakaazi wa eneo la Tumbe na hasa wavuvi walikipachika jina la ‘Kisiwa ndege’ kutokana na kuzagaa kwa idadi kubwa ya ndege.

Mratibu Khamis anasema, ugunduzi wa kisiwa hicho ni kuelekea kuengeza idadi ya vivutio vya utalii Kisiwani Pemba.

‘’Ni mwaka huu wa 2022 tu, ndio tumekigundua kisiwa hichi, na rasmi sasa tumeshakiingiza kama ni kivutio kipya cha kiutalii Kisiwa Pemba,’’ anasema.

Anaainisha kuwa, kuwa juhudi zikiendelea za ugunduzi wa vivutio vya utalii kama ‘kisiwa ndege’ ni ile dhana ya kuongeza idadi ya utalii Pemba, haitokua mbadala.

Historia ya Pemba, imeanza kukatika kutoka kisiwa cha Bara zaidi ya miaka milioni 5 iliyopita, ilijigawa na kupatikana visiwa vidogo vidogo ikiwemo cha Pemba.

Kisiwa cha Pemba nacho, kimeanza kukatika na kutengeneza visiwa vidogo vidogo kama vile Mkumbuu.

Ingawa kuna nguvu iliyotumika ya kujengwa daraja la kuungaisha mto uliopita, vyenginevyo eneo hilo lingekua tayari ni kisiwa.

“Licha ya daraja na mto uliopo, lakini kutokana na mazingira yaliyopo baada ya miaka kadhaa, Mkumbuu wilaya ya Chake chake, itakuwa kisiwa ambacho kitajitegemea,’’anasema.

Hili Mratibu huyo anasema, kwani sasa hivi tayari kuna mito miwili inayoingiliana baina ya upande mmoja na mwengine.

ASILI YA KISIWA NDEGE

Ni ndege wa aina tofauti, ambao wanaingia na kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Eneo moja ni kama vile Ulaya na kwenda kuishi kwa muda ndani ya kisiwa hicho na kuondoka.

“Kuna ndege wa pwani, wao wanatumia bahari kwa kutafuta chakula chao, kuna ndege aina ya Yangeyange, Makoho, Kunguru, Vijafara, Membe pamoja na Njiwa ambao wanakipamba kisiwa hichi”, anasema.

Ndege aina ya Membe ni ndege ambao wanalia kuashiria maji kutoka na kuingia, na mara nyingi wavuvi wanawatumia kujua maji yanapoingia au kutoka.

WIZARA YA UTALII NA MAMBO YA KALE

Mwenye dhamana ya ofisi hiyo Pemba, Zuhura Mgeni Othamn anasema, ndege waliopo ndani ya kisiwa hicho pekee ni utalii wa kutosha, achia mbali kisiwa hicho.

‘’Ndege ni sehemu ya utalii, wapo wageni ambao ni wanafanya utafiti, ambao hupenda kuona ndege au kuwinja, ndipo wizara ilipoamua kutembelea, ili kukitangaza kisiwa hicho,’’ anasema.

Anasema kuwa, ndege waliopo katika kisiwa hicho hawapatikani kwengine popote duniani, ambapo hilo ni jambo la kujivunia.

Licha ya rasilimali ya ndege iliyopo kwenye kisiwa hicho, lakini pia ardhi yake ni ya mwamba wa mawe na udongo wa aina ya tifu tifu.

 

Kwa upande wa wizara, imejipanga vyema kwa kukiimarisha  kisiwa hicho, ili kiweze kuleta faida kubwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

MKUU WA WILAYA

Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya, aliwataka wananchi kukitunza kisiwa hicho, kwa kurejesha msitu ambao ulikuwepo awali.

Anasema, kisiwa hicho ni moja kati ya vivutio muhimu cha utalii kwa Wilaya hiyo, hivyo aliwataka wananchi ambao wanafanya shughuli za kilimo, kulima kilimo kinachoendana na mabadiliko ya tabia nchi.

Anaeleza, kisiwa hicho endapo jamii itashindwa kukitunza, kitaathirika na ndege ambao wanaishi humo, wataondoka na kupoteza historia.

‘’Mandhari, uzuri na utamu wa kisiwa ndege ni kuwepo kwa ndege aina 12, kama ilivyo sasa, endapo shughuli za binaadamu zitawakimbiza ni kupunguza utamu wa historia,’’ anaeleza.

Binafis alifarajika kukitembelea kisiwa hicho, ambacho kina mandhari nzuri na haiba ya kuvutia, na kina mazalio ya ndege tofauti.

Mkuu huyo, aliwataka wananchi wa Pemba kujenga utamaduni wa kutembelea maeneo ya kihistoria, ili kujifunza na kujionea utalii ambao upo ndani ya kisiwa chao.

AFISA MAZINGIRA WILAYA YA MICHEWENI

Afisa Mazingira Wilaya ya Micheweni Salum Mjaka Ali anasema, kisiwa hicho kwa sasa, kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kimeathiriwa na shughuli za kibinaadamu.

“Hichi kisiwa kama tutaendelea kukitunza kitaendelea kubakia kutumika kwa shughuli za kiutalii, tutakapofanya uharibifu tunajiharibia maisha yetu,’’ anaeleza.

Aliwashauri wananchi ambao wanafanya shughuli za kilimo ndani ya kisiwa hicho, kufanya kilimo endelevu ambacho kitaimarisha hali ya kisiwa hicho kwa kupanda miti itakayodumu kwa muda mrefu.

Kisiwa Khamis (kisiwa ndege) kipo upande wa Mashariki wa bandari ya Tumbe, kikiwa ni moja ya visiwa vidogo vidogo vinavyomegeka siku hadi siku kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kwa zaidi ya miaka milioni 5 iliyopita.

                                            MWISHO.