NA ABDI SULEIMAN.
NAIBU Mrajisi wa mahakama kuu Pemba Faraji Shomar, amewataka watendaji wa Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Pemba, kuendelea kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi hususan vijijini, kwani waliowengi uwezo wao ni mdogo wa kuwapata wanasheria.
Alisema watendaji wa idara hiyo, wanapaswa kuwelekeza nguvu zao maeneo mengine ya wananchi kuwa kuwafikisha elimu hiyo, ili waweze kupata haki zao mahakamani au uraiyani kwa wale waliokosa.
Naibu huyo aliyaeleza hayo wakati alipokua akizungumza na wananchi wa shehia ya Ndagoni Wilaya ya Chake Chake, mara baada ya kufungua kambi ya siku mbili ya msaada wa kisheria.
Alisema lengo la kambi hiyo, ni kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi hao, kwani wananchi wa wengi ni wanyonge, masikini na uwezo wao wa kupata huduma za kisheria kupitia kwa mawakili ni mdogo, na wana mambo mengi ikiwemo migogoro ya ardhi, mirathi, udhalilioshaji na madawa ya kulevya.
“Tumekua tukishuhudia wananchi wengi wa kawaida wanashindwa kupata huduma ya sheria, kwa sababu ya uwezo wao mdogo wa kupata elimu hiyo ya sheria,”alisema.
Aidha aliwataka wanasheria hao, kuwasaidia wananchi wenye makundi maalumu, huku akiwasihi wananchi kuitumia fursa hiyo kuelezea matatizo yao, wakitambua kua serikali bado inaendelea kuwa na nia njema na wananchi wake.
Kadhi wa Rufaa Pemba Shekh Daudi Khamis Salum, aliwataka wananchi wa shehia hiyo kuitumia kamisheni ya wakuf na malia ya amana Zanzibar, kila wanapohitaji kurithishana.
Afisa Mipango kutoka kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar Ofisi ya Pemba Safia Saleh Sultani, aliwaomba wananchi wa shehia ya ndagoni kuitumia fursa hiyo adhimu kwa kutoa matatizo yao yanayowakabili na kupatia msaada wa kisheria.
“Leo hapa wanasheria wamewafuata nyinyi na wameacha kazi zao, kuna siku mutawafuata wao na mutalipia, kuitumia fursa hii adhimu kwenu,”alisema.
Naye Adamu Abdalla kutoka Mahakamani, alisema wananchi wa Ndagoni wanachangamoto mbali mbali ikiwemo masuala ya ardhi, udhalilishaji na barabara, hivyo wanapaswa kuwa wawazi ili kupatiwa ufumbuzi wa changamoto zao.
Mwanasheria kutoka kamisheni ya Wakfu na Malia ya Amana Zanzibar Ofisi ya Pemba, Mussa Ali mussa alisema migogoro ya mirathi imekua ikitokea kwa wingi, sababu kubwa wananchi kushindwa kurithishana baada ya mmoja ya wanafamilia kufariki dunia.
Kwa upande wake Afisa Dawati jinsia la watoto Mkoa wa Kusini Pemba Zuwena Hamad Ali, alisema wanawake wanakabiliwa na kesi nyingi za udhalilishaji wa wanawake na watoto.
“Vizuri kuitumia siku yale kwani matukio ya udhalilishaji yapo mengi huku, wanaume kwenda dago na kuwacha wake zao muda wanaorudi wanaujuwa wao,”alisema.
Nao wananchi wa shehia hiyo, wamesema changamoto kubwa ni migogoro ya ardhi, kwa kuvamiwa ardhi yao na kushindwa kupatiwa fidia yoyote.
Fatma Suleiman Khamsi alisema wanaume wamekuwa wakiwadhalilisha kwa kuwaacha na watoto huku wakishindwa hata kuwahudumia, jambo ambalo husababisha migogoro kwenye familia.
MWISHO