NA ABDI SULEIMAN
MTU mmoja amefariki dunia na mmoja kunusurika kufa, baada ya chombo chao aina ya ngalawa ya waliokuwa wakivulia samaki baharini kuzama kutokana na upepo mkali.
Aliyefariki dunia ametambuliwa kwa jina la Mohamad Ali Mohamad (40) mkaazi wa kisiwa cha Makoongwe na alienusurika kufa ni Ali Shaaban Khamis wote wakaazi wa Kisiwa cha Makoongwe.
Mwili wa marehemu huyo ulilazimika kuzikwa huko huko Ndagoni, kutokana na kutokubebeka kufuatia kukaa baharini tokea Julai 8 mwaka huu.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, baadhi ya mashuhuda wamesema taarifa ya kuonekana kwa mwili huo wamewasikia watoto ambao walikua wakiongelea baharini hapo.
“Baada ya kusikia hizo tuliweza kwenda kushuhudia na kuuona mwili wa mtu, ndipo tulipotoa taarifa kwa viongozi wa shehia na serikali,”alisema mmoja ya mashuhuda.
Akizungumza na Waandishi wa habari manusura wa tukio hilo, Ali Shaban Khamis alisema sababu iliyopelekea kutokea kwa tukio hilo ni uupepo mkali uliopelekea chombo chao kuzama.
Alisema baada ya kuzama waliweza kukaa juu ya chombo chao kwa muda mrefu, kabla ya kuanza harakati za kujiokoa kwa kuogolewa hali iliyopelekea mwenzake kupotea na kuonekana akiwa ameshafariki.
“baada ya kuzama tulikuwa na madumu matupu ndani ya chombo, tulikamata kila mtu lake, ila baadae anakanambia kuwa amechoka mimi nikakimbilia juu niliporudi na wasamaria wema hatukumuona,”alisema.
Sheha wa shehia ya Ndagoni Massoud Ali Mohamed, alisema taarifa ya kupotea kwa Mohamed Ali, alipata siku nne nyuma baada ya ndugu zake kufika kumtafuta katika maeneo yao lakini ilishindikana mpaka alipoonekana jana akiwa amefariki.
Alisema tayari miili ya watu sita imeshaokotwa katika eneo la Ndagoni, kwa mwaka huu ukiwa ni mwili wa kwanza kuzikwa katika eneo hilo la mbuyuni.
Naye baba mdogo wa marehemu huyo, Juma Mohamed Ali aliwashukuru wananchi wa shehia ya ndagoni kwa umoja na upendo wao waliouwonyesha kipindi chote walichokuwa akiutafuta mwili wa mtoto wao.
Afisa mdhamini Ofisi ya Makamu wa Pili Pemba Ali Salum Matta, alizishukuru taasisi za serikali zilizojitokeza katika kusaidia kupatikana kwa mwili huo, pamoja na wananchi wa shehia ya ndagoni na Makoongwe.
Aidha mdhamini huyo aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa viongozi wa shehia pale panapotokea matukio au majanga ya moto, ili serikali iweze kutambua haraka na kutoa msaada wa hali ya juu.
“Sisi kama serikali taarifa rasmi hatukupata watu wetu wa kamisheni ya kukabiliana na maafa wamepeta leo baada ya mwili kuonekan, kama ingetoka zamani basi hata siku ya tukio tungeweza kusaidia na kama kupatika akiwa mzima au amefariki angepatikana,”alisema.
Hata hivyo mdhamini huyo aliwataka wananchi ambao wanajishuhulisha na shuhuli za uvuvi kuhakikisha wanafuatilia taarifa za hali ya hewa muda wote katika vyombo vya habari ili kuepukana na majanga yanayotokea baharini.
MWISHO