NA ABDI SULEIMAN.
KATIBU wa Itikadi na Uenezi CCM Taifa Shaka Hamdu Shaka, amesema Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa ni mtu mwenye upendo na uvumilivu uliopitiliza katika kuendesha siasa za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Shaka alisema nyakati zote, hata pale Chama cha Mapinduzi kilipofungua milango ya maridhiano na mazungumzo, Maalimu Seif Sharif Hamadi alitanguliza maslahi mapana sana ya Watanzania na Wazanzibari na kuwaunganisha.
Katibu huyo, aliyaeleza hayo katika ziara yake ya kuzuru makaburi ya viongozi wakuu wa kitaifa Kisiwani Pemba, wakiwemo aliyekua makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania marehemu Dkt.Omar Ali Juma kijijini kwao wawi Wilaya ya Chake Chake na Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad kijijini kwao Mtambwe Nyali Wilaya ya Wete.
Alisema jambo hilo ni funzo kubwa sana kkwao na kizazi kilichopo, hivyo tunaweza kuisha na kutembea nyao badala ya kuongozwa na uhafidhia na chuki na jazba na mpasuko ndani ya jamii.
“Nivyema ni vyema tukarudi tukafuata nyayo za waliotutangulia katika miaka 30 hii ya kuendesha siasa za nchi, kweli walifanya mambo makubwa kwa wananchi wake,”alisema.
Aidha alisema bado kunanafasi ya kujenga leo yetu na kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya vizazi vinavyokuja, kwani maalim Seif amefariki lakini amewacha funzo kubwa na deni kubwa, deni ambalo ndilo lililowapatia amani, umoja na mshikamano ndani ya nchi.
“Mimi naweza kusema bila ya busara subra na hekima za viongozi waliotutangulia, akiwemo maalimu seif sharif Hamad, matunda haya tulionayo ya amani, umoja na mshikamano kupitia serikali ya umoja wa kitaifa yasingekuwepo kwa upande wa Zanzibar,”alisema.
Alifahamisha kuwa Dunia leo hii imepata funzo kubwa sana, kutoka Zanzibar na Tanzania, uwepo wa serikali ya Umoja wa Kitaifa imeleta upendo umoja na mshikamano ndani ya taifa.
“Hebu tizameni leo hii tumefika mtambwe tukiwa wamoja, bila ya kujali tafuti zetu na itikadi zetu za chama siasa, wala madhehebu mengine ya dini wote tumesimama wamoja, kumkumbuka na kumuenzi alipanda mbengu njema kwa wazaznibari,”alisema.
Akizungumzia juu ya marehemu Dkt.Omar Ali Juma, alisema ni miaka 21 sasa na amekuwa funzo kubwa kwa Taifa, kwani alikua ni kiongozi wa mfano kwa Zanzibar.
Alisema alitimiza wajibu wake kwa nchi na taifa kwa ujumla, katika kuhakikisha nchi inaendelea kupiga hatua, bado mawazo yake na michango inaendelea kukumbukwa.
Sheha wa shehia ya Mtambwe Kaskazini Saleh Khamis, alimuomba katibu huyo kuhakikisha wanawatengenezea barabara yao, kwani imekua ikitumiwa na watu mbali mbali kufika kumuombea dua kiongozi huyo.
Naye mwana wa familia ya Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, Mzee Bakari Sharif Hamad aliishukuru serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua walizozichukua, pamoja na viongozi wengine kutokuchoka kufika kumuombea dua kiongozi huyo.
Naye Zubeir Ali Juma mwana familia ya marehemu Dkt.Omar Ali Juma, alimtaka katibu wa Itikadi na uenezi, kuhakikisha wanawatilia fusi katika barabara inaingia katika kaburi la kiongozi huyo, pamoja na kuwawekea umeme katika kituo cha ulinzi kilichomo kaburini hapo.
MWISHO