Friday, November 15

UTPC yawanoa waandishi wa habari juu ya usalama wao

NA ZUHURA JUMA, DODOMA.

WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kuzingatia usalama wao wakati wanapofanya kazi ya kuandika habari, kwani ni maisha yao ni muhimu zaidi kuliko habari hizo.

Akifungua mafunzo ya siku mbili juu ya ulinzi na usalama kwa waandishi huko Dodoma, Mjumbe wa Bodi ya UTPC Yussuf Mussa alisema, mafunzo hayo yatawajengea uwezo waandishi katika kujitambua na kujua thamani yao katika utendaji wa kazi zao za kihabari.

Alisema kuwa, waandishi wa habari wamekuwa na jukumu kubwa la kuwapasha wananchi habari mbali mbali, ingawa sayansi na teknolojia inawaweka wanahabari hao katika hali hatarishi, hivyo ipo haja ya kujua jinsi ya kujilinda ili kuwa katika hali ya usalama.

“Naamini kwamba baada ya mafunzo haya mtajua namna ya kujilinda, hivyo nawaomba musipende kukaa na watu msiowafahamu na mnapopigiwa simu tuwe makini, ili tusije tukaingia katika matatizo”, alisema Mjumbe huyo.

Kwa upande wake Afisa Program Machapisho, Utafiti na Mafunzo kutoka UTPC Victor Maleko, alieleza kuwa suala la usalama na ulinzi wa waandishi ni muhimu sana, hivyo ni vyema wakazingatia wanachofundishwa katika mafunzo hayo kwa ajili ya usalama wao.

“Tunajitahidi kupigania haki za watu lakini sisi wenyewe hatupiganii zetu, kwa hiyo tuwe makini wakati tunapofanya kazi zetu za kihabari, maisha yetu ni bora zaidi”, alifahamisha Afisa huyo.

Aidha alisema kuwa, UTPC inatekeleza mradi wa miaka miwili unaolenga kuzijengea uwezo taasisi za kihabari nchini, ambapo moja ya shughuli zake ni kutoa mafunzo kwa wanachama wa klabu kuhusu ulinzi na usalama kwa waandishi wa habari.

“Mradi huu utakapomalizika tunatakiwa tuwe tumeshawapatia mafunzo hayo wanachama 100, tunatumai kwamba na hawa watawafikishia waandishi wengine ambao hawakupata nafasi ya kushiriki”, alifahamisha.

Nae mkufunzi wa mafunzo hayo, Mtaalamu wa Mawasiliano ya Umma Dr Joyce Bazira, alisema sio vyombo vyote ambavyo vinamsaidia mwandishi wa habari anapofikwa na matatizo, na kuwataka kuwa makini wakati wanapotekeleza majukumu yao.

“Migongano inaendelea kila siku katika jamii zetu, kwa hiyo tunapoandika habari tuhakikishe kwanza tunajilinda na tunakuwa salama” alisema dr Joyce.

Akiwasilisha mada ya namna ya kujilinda katika mitandao wanayotumia waandishi hao, Mkurugenzi Mkuu wa TMF Dastan Kamanzi aliwataka waandishi kuacha tabia ya kuweka taarifa zao binafsi kwenye mitandao, kwani zinaweza kuwarahisishia wahalifu wenye lengo la kuwadhuru.

“Ni wakati sasa tujielewe isiwe kila kitu tunaweka mtandaoni hata taarifa zetu binafsi kwani ni hatari sana, pia tutengeneze programu ambazo zitawasaidia kuficha kazi zetu,” alifahamisha Mkurugenzi huyo.

Kwa upande wao waandishi walieleza kuwa, wamekuwa wakitishiwa usalama wa maisha yao hasa pale wanapoandika habari ambazo zinawagusa watu ambao hawatakii mema maslahi ya jamii yao, jambo ambalo linarudisha nyuma tasnia ya habari nchini.

Mafunzo hayo yameandaliwa na UTPC chini ya ufadhili wa Shirika la IMS (International Media Support) ambalo linapewa fedha kutoka Umoja wa Ulaya (EU).

MWISHO.