WAANDISHI wa habari, vyama vya habari vishajihishe upatikanaji sheria ya Habari
- Itaongeza upatikanaji uhuru wa habar
- Ni zao la katiba zote mbili za Tanzania
NA ABDI SULEIMAN.
KWA mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kifungu cha 18 kifungu kidogo(1)“Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutatuta kupokea na kutoa habari na dhana kupitia chombo chochote, bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati”
Nacho kifungu kidogo (2)kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbali mbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shuhuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii”
Kifungu hichi kimeeleza umuhimu wa upatikanaji na utoaji wa habari kwa raia, bila ya kuathiri sheria za nchi na kutokuingiliwa mawasiliano yao.
Ikiwa katiba ya nchi inaeleza hivyo, lakini hali halisi kwenye baadhi ya sheria zilizopo nchini haziko wazi kama ilivyoeleza katiba hiyo.
Juu ya hilo tunapaswa kuangalia sheria ya usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988 kama ilivyofanyiwa na sheria namba 8 ya mwaka 1997, ni sheria ya kwanza baada ya uhuru, lakini kwa bahati Sheria hii sasa imekua na mapungufu yanayokwamisha haki ya uhuru wa vyombo vya habari na uandishi wa habari Zanzibar.
Sheria hii inasura 10 na vifungu 80 ndani yake, huku baadhi ya vifungu ikionekana kuwa na mafungufu, ikiwemo kifungu cha 14 (1)na (2).
Kifungu kidogo (1)Mchapishaji wa gazeti lililochapishwa Zanzibar atawajibika kwa kila siku ambayo gazeti linachapishwa, kwa gharama zake kuwasilisha, kulipeleka kwa njia ya posta, kwa Mrajis nakala mbili za gazeti hilo na nakala mbili za kila toleo la ziada la gazeti hilo kama zipo.
Kifungu kidogo (2)Nakala hizo zitakuwa kwenye aina ya karatasi ambazo kiasi kikubwa cha nakala za gazeti hilo kitakuwa kimechapwa na kuchapishwa na zitakua katika hali sawa na nakala zilizotayarishwa kwa kuuzwa na kusambazwa.
WAANDISHI WA HABARI WANASEMAJE
Khadija Kombo Khamis kutoka ZBC anasema kifungu cha 14(1)(2) hakiko sawa na katika utaratibu huo hakuna uhuru wa habari na wala hauwezi kuwa kutokana na kifungu hicho.
Anasema kutokana na harakati za kimaendeleo yaliyopo kazi za sasa zote ni za harakati, kinakazwa “uchapishe gazeti halafu gazeti mbili upeleke kwa mrajis, wakati huo kunagharama za nakala mbili hizo” kifungu kimekaa kama kuna adhabu ndani yake.
Mwandishi Gaspary Charles, anasema kifungu hicho kinanyima uhuru wa habari na hakiko sawa, kwani kinazoretesha utendaji wa kazi wa mlazalishaji kufanya kazi kwa kuhofia kufanya makosa yatakayoathiri uchapishaji wa gazeti husika.
“Ili kuweka mazingira sawa ya magazeti kufanya kazi zake kwa uhuru bila hofu, ni vizuri kama kifungu hiki kingebadilishwa na kuwa jukumu la mrajis mwenyewe, kutafuta nakala za kopi kumbukumbu na simkumbebesha mzigo mchapishaji,”amesema.
Naye Amina Ahmed kutoka Zenj FM, anasema kifungu kinabana uhuru wa mmiliki gazeti, bali mrajisi anapaswa kununua gazeti wakati mzalishaji amesajiliwa kwa gharama.
Mwandshi Omar Haji yeye amekuwa na mtazamo tafuti, amesema nijambo zuri kuwasilisha kopi mbili za gazeti, kwani taasisi husika ya kihabari itakuwa makini katika uzalishaji wa habari ambazo zipo sahihi.
“Tumekua tukishuhudia baadhi ya magazeti kufungiwa kutokana na kuandika habari za uongo au uchochozi, kutokana na kutokuwa makini na habari wanazozizalisha,”amesema.
WAANDISHI WA MAGAZETI WANAYAPI YA KUSEMA
Grace Paulo kutoka gazeti la Sauti, anasema kifungu hicho kinaondosha uhuru wa mwandishi na taasisi yake katika uwandishi wa habari.
“Sasa hapa kama unataka kufanya habari za uchunguzi na ikatoka, siku moja hao wafanyakazi wa mrajisi si wataweza kukuweka hadharani, kama habari imeandikwa na nani na unaweza kupoteza hata maisha,”amefahamisha.
Mwandishi Bakari Mussa kutoka Gazeti la Zanzibarleo Ofisi ya Pemba, anasema kifungu hicho hakina ulazima kutokana na mabadiliko ya kimtandao, kwani anaweza kupelekea kwa njia mtandao kuliona na kujiridhisha.
Anasema kulepeleka hivyo ni kuitia hasara taasisi, kwani hali hiyo inapelekea makampuni kushindwa kuanzisha magazeti Zanzibar kutokana na kifungu hichi kunyima uhuru.
“Hivi sasa utandawazi umekua tuendane na mabadiliko ya kidunia, gazeti linalotumwa mitamboni kuchapishwa na mrajisi kutumia kwenye mtandao na sio kupeleka kama ilivyo sasa,”alisema.
WADAU WA HABARI HAWAKUSITA KUSEMA YAO JUU YA SHERIA HIYO
Meneja wa Redio Jamii Micheweni Ali Massoud Kombo amesema kifungu hichi ni kunyima uhuru wa gazeti, kwani kila siku baada ya kushuhulikia gazeti mzalishaji anawaza mrajisi atalipata vipi au wapi kumpelekea gazeti.
Anasema waandishi wanatakiwa kupiga kelele ili sheria na kifungu hicho kiweze kubadilika, ukeshasajili iwe basi umeshasajili, kilichobakia ni kufuata taratibu, sheria na kanuni na sio kila siku unahangaikia mengine kwenda ofisi ya msajili.
“Kama kifungu hichi kitaendelea kuwepo kitakua bado kinakandamiza uhuru wa habari, sasa itakua uwajiri mtu kila siku kupeleka magazeti kwa msajili, hili ndilo linalopelekea Zanzibar watu kushindwa kufungua vyombo vya habari au magazeti,”amesema.
Mkurugenzi kutoka Jumuiya ya KUKHAWA Pemba Hafidhi Abdi Said, amesema kifungu hichi kitapelekea waandishi wa habari na vyombo vya habari vya magazeti, kushindwa kufanya kazi zao ipasavyo, kwa kutokuwa huru na kutokuaminiwa na mrajis huyo.
Anasema “sasa dunia imebadilika kutoka analogi kwenda kidijitali, hivyo ni wakati wakutumia mabadiliko hayo baada ya kupelekewa kopi mbili sasa ni kutumiwa kwa kutumia mtandao,”.
Fatma Abrahmana kutoka JICHOLETU ONLINE TV, anasema kifungu cha 14(1) na (2) kinapaswa kubadilishwa, kwani hakiwezi kuipa habari uhuru na badala yake kinadumaza uhuru wa habari.
WANASHERIA WANAMTAZAMO GANI WAO
Mwanasheria wa Serikali kutoka Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar ofisi ya Pemba, Ali Amour Makame anasema kifungu cha 14 na vifunbgu vyake vidogo, vinaondoa uhuru wa habari na kutia hofu kwa vyombo vya habari.
“Chombo cha habari kikishindwa kupeleka nakala ya gazeti adhabu yake ipi, ni vizuri ingejulikana au kutajwa katika vifungu hivyo, sambamba na mrajis kununua kopi hizo mbili kila siku kama ilivyo wateja wengine,”amesema.
Anasema “wamiliki wanalipa kodi zote zinazotakiwa na serikali au mrajis, wakati wa kusajili kampuni au chombo hicho cha habari, pamoja na kuridhia kanuni, sheria na taratibu zote,”.
Naye mwanasheria kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, bakar Ali Omar anasema kuwa shehria inaoneka imeshapitiwa na wakati, hivyo ipo haja kwa sheria hiyo kufanyiwa marekebisho.
Amesema kifungu hicho lazima kifanyiwe marekebisho, ili nakala za gazeti kuwasilishwa kwa mrajisi kwa kutumia njia za mtandao ambazo zinawekana kutokana na utandawazi uliopo.
WATENDAJI WA VYOMBO VYA HABARI NAO WANASEMAJE
Mhariri Mtendaji kutoka shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar Ali Haji Mwadini, anasema vifungu vinahitaji kufanyiwa marekebisho, ili kutoa uhuru zaidi wa habari.
Anasema kuwasilisha nakala mbili kwa marjisi kifungu chi kinapaswa kuwepo, kwani mrajisi anatakiwa kuangalia utoaji wa habari na pamoja na kuwa msimamizi.
Naye afisa mdhamini Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Pemba, Mfamau Lali Mfamau amesema malengo ya sheria ni mrajirsi kutaka kuahkiki maudhuwi anayopatiwa mlaji ni sahihi na hayatoa ukakasi.
Amesema kutokana na maendeleo ya sasa ya sayansi na teknolojia, mchapishaji anapaswa kukutana na mrajisi kujadiliana na kutumia njia mbadala na kuwasilisha kwa kutumia njia ya mtano.
“Hapa watu wanakimbia gharama au shida mtu kutoka sehemu moja kwenda nyengine, ila wakati huu ni vizuri kutumia mitandao ili kufikisha kopi hizo kwa urahisi,”amesema.
NAVYO VYAMA VYA KIHABARI HAVIKUSITA KUSEMA YAO
Katibu wa Pemba Press Club Ali Mbarouk Omar, amesema ni wakati sasa kwa sheria hiyo kufanyiwa marekebisho, ili kuondosha ukakasi kwa wamiliki wa vyombo vya habari na kutoa fursa kwa magazeti mengine kusajiliwa Zanzibar.
Amesema kwa sasa kuna njia mbali mbali za uwasilishaji wa nakala za magazeti kwa mrajis, kinachopaswa ni makubaliano baina ya mrajisi na mzalishaji wa gazeti, kwani hata njia ya utandawazi kwa mitandao inaweza kutumika.
Afisa kutoka baraza la habari Zanzibar (MCT) Shifaa Said Hassan, amesema sheria ijamaa vipengele ambavyo ni ndamizi kwa uhuru wa habari, ndio maana wadau wanavifanyia uchechemuzi ili kubadilishwa na kwenda na wakati wa mabadiliko ya dunia kiutandawazi.
Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar kwa ufadhili wa Shirika la Internews, kwa sasa wapo katika kufanyia uchechemuzi wa sheria hiyo, katika vifungu mbali mbali ambavyo kandamizi, ili kuweze kupatikana kwa sheria mpya.
NINI KIFANYIKE?
Mratib wa TAMWA-Zanzibar Ofisi ya Pemba, Fathiya Mussa Said amsema ujio wa sheria mpya ya wakala wa habari, Magazeti na Vitabu Zanzibar, itapelekea baadhi ya vifungu kubadilisha ili viendane na tansia ya habari.
“katika sheria hii iliyopo sasa ambayo tunaifanyia uchechemu, muna vifungu kadhaa vimekua vikinyima uhuru wa habari ikiwemo kifungu cha 14(1)na (2),”amesema.
Mwandishi wa habari Gaspa, anasema ili kuweka mazingira sawa ya magazeti, kufanya kazi zake kwa uhuru bila hofu, ni vizuri kifungu hiki kingebadilishwa na kuwajukumu la mrajis mwenyewe kutafuta nakala za kopi, ili kuliweka kumbukumbu na simkumbebesha mzigo mchapishaji.
Naye Is-haka Mohamed Rubea meneja ZENJ FM Radio, anasema ni wakati wakutumia mitandao kama vile email kwa kutumiwa kopi za gazeti na kuondosha kupelekewa moja kwa moja kama ilivyo sasa,
MWISHO