Thursday, January 16

WANANCHI 5674 kunufaika na huduma ya maji safi na salama

MAELEZO YA PICHA. katibu wa CCM jimbo la Chonga Massoud Juma Khamis, kimkabidhi mipira 10 ya maji shehsa wa shehia ya Kilindi Nassor Mohamed Khamis, mipira hiyo iliyotolewa na Mwakilishi wa Jimbo la Chonga ambae ni Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar Suleiman Massoud Makame.(PICHA NA ABDI SULEIMAN,PEMBA)

NA ABDI SULEIMAN.

ZAIDI ya wananchi wa 5674 wa shehia ya Kilindi jimbo la Chonga Wilaya ya Chake Chake, wanatarajia kuondokana na tatizo la ukosefu wa maji safi na salama, ambalo lilidumu kwa miaka mitatu katika shehia yao baada ya kupatiwa roli 10 za mipira ya usambazaji wa maji.

Awali wananchi hao walikuwa wakisumbuka katika suala la upatikanaji wa huduma hiyo, wakati wemngine hutumia maji ya visima mabondeni.

Hayo yameelezwa na katibu wa CCM jimbo la Chonga Massoud Juma Khamis, kwa niaba ya mwakilishi wa jimbo hilo ambaye pia ni Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Suleiman Massoud Makame, huko Mgogoni Wilaya ya Chake Chake.

Alisema baada ya kuona wananchi wanatatizo la maji, mwakilishi wa Jimbo hilo amelazimika kuwatatulia wananchi shida hiyo, ili kupata maji safi na salama.

Alisema utoaji wa mipira hiyo ni kufuatia maombi ya wananchi wa shehia hiyo, kuyafikisha kwa viongozi wa jimbo, huku mwakilishi akiahidi kuwatatulia.

“Hii ni utekelezaji wa ahadi za wananchi ambao walifika kumuelezea mwakilishi wao, leo ndio tumekuja kiutekeleza ahadi hiyo kwa vitendo,”alisema.

Sheha wa shehia ya Kilindi Nassor Mohamed Khamis, alimshukuru mwakilishi huyo, kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi zake, kwa kuwatatulia wananchi tatizo la maji kwa kuwapatia mipira hiyo.

Aidha aliahidi mipira hiyo kutumika ipasavyo katika vijiji  vyote ambavyo vinatatizo la maji, ili kuona wananchi wanapatia msaada mwengine na sio maji tena.

“Baada ya maji kukamilika na kuanza kutoka tutatafuta kitu chengine ili mwakilishi wetu aweze kutusaidia, lengo ni kuona yale matatizo yetu yatatuliwa ipasavyo,”alisema.

Kwa upande wake Khatib Juma Khatib mkaazi wa Pujini, alisema mwakilishi huyo amekua mstari wambele katika utatuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo.

Hata hivyo aliwataka wananchi wa jimbo hilo, kuendelea kumuamini mwakilishi wao, kwani amekua na dhamira ya dhati katika kusaidia huduma mbali mbali zinazowakabilia.

Naye Abdalla Juma Feruzi, aliwataka viongozi wengine wa majimbo kuiga mfano utaoonyeshwa na mwakilishi wajimbo la Chonga, katika kuwatatulia changamoto wananchi, sambamba na kuthamini maoni ya wananchi yanayotolewa katika vikao vya jimbo.

MWISHO