NA HANIFA SALIM, PEMBA
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi, amewahakikishia wajasiriamali wa Wilaya ya Micheweni kwamba serikali itarahisisha upatikanaji wa kupata mikopo sambamba na kuunda timu zitakatoa huduma ili kuacha kufuata huduma Chake Chake.
Dk, Hussein Mwinyi alisema, watatafuta njia ya kuwapunguzia wananchi kutembea masafa marefu kufuata utaratibu wa upatikanaji mikopo kwani imeonekana ni changamoto kubwa kwa wajasiriamali waliopo katika Wilaya nyengine.
Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi mara baada ya kutembelea miradi mbali mbali ya wajasiriamali waliopewa fedha za mkopo wa UVIKO 19 huko katika viwanja vya Shaame mata Micheweni Pemba.
“Tutahakikisha yale yote ambayo wajasiriamali yamekuwa ni changamoto kwao kuwa yanafanyiwa kazi ili muweze kufanya biashara zenu kwa uhakika, nataka muelewe mkopo huu ni mwanzo mtakaporudisha mutapata mkubwa zaidi “, alisema.
Alieleza, Ilani ya Uchaguzi imekuwa ikitekelezwa kwa vitendo kwani mikopo imeanza kutolewa, mazingira mazuri yameanza ya kufanyia biashara kwa kujenga masoko ya kisasa ya wajasiriamali wa mboga mboga, samaki na mengineyo, elimu na zana pia kutolewa.
“Tulisema hapa tunataka kuwapa elimu wajasiriamali kilingana na biashara wanazozifanya wawe na weledi nazo, kuwapatia mikopo, kuwapatia zana za kisasa za kufanyia biashara zao na kutengeneza mazingira mazuri ya kufanyia kazi zao”, alisema.
Aidha Dk, Hussein aliipongeza benki ya CRDB kwa kazi kubwa wanazozifanya ya kuendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha wajasiriamali wanapata mikopo isiyokuwa na riba ya kuwawezesha kufanya shughuli zao na kutoa elimu.
Wakati huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi aliweka jiwe la msingi katika ujenzi Hospitali ya Wilaya ya Micheweni ambapo majengo hayo ni utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi 2020-2025 kwa vitendo.
Alieleza, Wilaya zote za Unguja na Pemba zitakuwa na Hospitali kubwa za kisasa ambazo zitakuwa na zana za matibabu sambamba na kutoa kibali cha ajira ambacho kitaajiri wafanyakazi wa afya watakaohudumia Hospitali hizo.
“Wahudumu wa Afya wa kujitolea msiwe na wasi wasi wakati wa ajira tutakupeni kipaumbele katika hospitali zetu hizi zinazojengwa kila Wilaya”, alisema.
Akizungumzia sekta ya elimu alisema, kutokana na kukuwa kwa idadi ya wanafunzi waliopo Micheweni serikali itajenga skuli ya msingi ya gorofa ambayo itawawezesha wanafunzi watajisomea vizuri na kuepusha misongamano ya watoto madarasani.
Dk, Hussein akizungumzia suala la barabara alisema, serikali itajenga kilomita 275 barabara za ndani katika vijiji vya Unguja na Pemba kwa hatua ya lami na sio kwa kuweka kifusi kama ilivyozoeleka hapo zamani.
Mapema, Waziri wa kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar Mudrik Ramadhan Soraga alisema, hali ya uwezeshaji wananchi kiujumla kwa upande wa Kaskazini Pemba inaendelea vizuri kupitia Wilaya zote mbili ikiwemo Micheweni na Wete.
Alifahamisha hadi kufika Julai 22 mwaka huu wizara imeshatoa fedha kwa vikundi 58 kwa Wilaya ya Micheweni na 58 kwa Wete ambapo zaidi ya milioni 500 zimetolewa kwa Wilaya ya Wete na zaidi ya milioni 700 Micheweni.
Alisema, wizara inafahamu changamoto kubwa ya ucheleweshaji wa kutoa mikopo lakini jambo hilo lina sababu ya msingi ambayo ni uhakiki wa vikundi na kujiridhisha wao na kwa upande wa benk ndipo kukajitokeza tatizo hilo.
Aidha aliwapongeza wajasiriamali wa kisiwa cha Pemba kuwa ni wasikivu, wamehamasika na wanatoa mashirikiano makubwa wakati wanapohitaji kukutana nao kuwapa miongozo mbali mbali ya utekelezaji hufanya vizuri sana.
Mkuu wa Wilayaya Micheweni Mgeni Khatib Yahya alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza laMapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi kwa maendeleo ambayo anaendelea kuwapatia wananchi wake wa Wilaya hiyo.
Mmoja ya wajasiriamali Riziki Yassir Hamad kutoka Kizimbani Wete, alisema hali halisi ya upatikanaji wa mikopo ya wajasiriamali wanapofikia benk hukumbana na usumbufu mkubwa kwao.
“Wanaweza kukupigia simu ufike benk unapokwenda wanatutaka radhi turudi ukiangalia uhalisia wa masafa ya kutoka Wete hadi Chake ni usumbufu kwetu na nauli, tunakuomba Rais wetu uzidi kutuongezea nguvu hususani sisi wanawake kuyafikia maendeleo” ,alisema.
Hiyo ni miongoni mwa ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi , Dk, Hussein Ali Mwinyi aliianza kisiwani Pemba kwa mkoa wa Kaskazini Pemba.
MWISHO.
Abdi Juma Suleiman
Journalist/Photographer