PEMBA.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu ili wanafunzi wapate mazingira mazuri ya kusoma na kufanya vyema katika mitihani yao.
Dk. Mwinyi alisema hayo leo huko katika Ikulundogo ya Pagali Kisiwani Pemba, katika hafla ya kuwapongeza wanafunzi wa Kidato cha Nne 2021 na Sita waliofanya vizuri katika mitihani yao ya Kitaifa ya mwaka 2022 sambamba na kula nao chakula kwa pamoja alichowaandalia.
Sambamba na hilo alieleza kuwa Serikali itaekeza katika vyuo vya mafunzo ya amali kwa wale wanafunzi ambao hawakupata nafasi ya kuendelea pamoja na kuwapatia mikopo ya elimu ya juu katika bodi zote mbili ikiwemo ile ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jambo ambalo litawawezesha kujiendeleza kielimu.
Katika kuzithamini juhudi za wanafunzi hao Rais Dk. Mwinyi ametoa nafasi za udhamini wa masomo “Scholaship” kwa wanafunzi 30 waliofanya vizuri katika mitihani yao ili kuendelea na masomo katika vyuo mbali mbali.
“Kupata Division one kwa mwanafunzi sio jambo rahisi sisi tuliosoma Tanzania tunajua lazima afanye kazi ya ziada hivyo, Serikali imeona haja ya kuwapongeza kwa kuwapatia nafasi hizo pamoja na kuwapatia zawadi ikiwemo Kompyuta mpakato (Lop top) kwa wanafunzi wote waliofanya vyema katika mitihani yao wakiwemo wale wa kidato cha Sita 2022 na kidato cha Nne 2021”, alisema.
Alifahamisha kuwa kulingana na takwimu zilizotolewana ufaulu wa wanafunzi ni dalili njema kuwa Zanzibar itafikia malengo ya kufanya Mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu na kuhakikisha wanafunzi wanafaulu vizuri katika madaraja ya juu.
Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa kutokana na hilo ni wazi kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imeweza kutimiza kwa vitendo maagizo yake aliowapatia juu kukuza kiwango cha juu cha ufaulu kwa wanafunzi wa Zanzibar.
Alisema kuwa Wizara ya Elimu imekuwa ikifanya kazi kubwa na maandalizi mazuri kwa siku za usoni kwa sababu alikaa nao na kuwaambia haridhiki na matokeo ya wanafunzi wanaofaulu katika mitihani yao kwa sasa na lazima watafute njia mbadala.
“ Mimi binafsi nilikaa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali nikawambia mimi siridhiki natambuwa na nyinyi hamridhiki na matokeo tunayoyapata sasa lazima tutafute njia ya kuyafanya matokeo yanakuwa mazuri zaidi bahati nzuri wamechukuwa juhudi hizo nawapongeza sana”, alisema Dk. Mwinyi.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa pamoja na Wizara kuunda timu ya wadau kufanya maboresho ya elimu na Serikali inayasubiri na itahakikisha inayatekeleza yale ambayo yanapendekezwa katika ripoti hiyo ili hatimae Elimu ya Zanzibar inakuwa bora zaidi na ufaulu unakuwa mkubwa zaidi.
Hata hivyo, aliwashukuru walimu wengine wote pamoja na walimu wakuu kwa kufanya kazi nzuri licha ya mazingira magumu waliokuwa nayo sambamba na wazazi na walezi kwa kuwasimamia vijana wao wasome vizuri jambo ambalo matokeo yake wamejumuika pamoja katika hafla hiyo.
Dk. Mwinyi alisema kuwa iwapo wadau wa elimu wataendeleza mwenendo huo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itafanikiwa kwani asilimia hizo zilizotajwa 2.8 mpaka asilimia 18 hiyo ni hatuwa nzuri zaidi kwani kuna mwanga unaonekana na kuahidi yeye na wenzake watahakikisha kuwa hilo wanalikamata vyema ili huko mbele ya safari wazungumze lugha nyengine ili asilimia hiyo iwe kubwa zaidi.
Aidha, aliwapongeza wadau wengine wa elimu wakiwemo wamiliki wa Skuli binafsi ambao ni sehemu ya mafanikio yao ambao walionesha dhahiri kama watashajiishwa basi wataweza kufanya vizuri zaidi kwa vijana.
Alisema wakati Serikali inajenga mfumo wadau wengine wote wanayo nafasi ya kushirikiana nao ili waweze kufanya vizuri na wakati anafanya ziara ya kuangalia miradi mbali mbali kisiwani Pemba ameanza kuona mabadiliko makubwa kwani kumekuwa na uwekezaji katika sekta ya elimu kwa kuwepo ujenzi wa skuli mpya za Msingi na Sekondari na ujenzi wa madarasa mapya yanjengwa kila upande.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi Serikali itaendelea kuwekeza kwa kuwa na skuli nyingi zaidi ikiwemo za ghorofa sambamba na kuajiri walimu wapya ili kupunguza uhaba wa walimu wa masomo mbali mbali ikiwemo wa Sayansi ambazo zimeshaanza kutangazwa ili kuweza kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu.
“Serikali inachangamoto kubwa ya kielimu wapo idadi kubwa ya wanafunzi katika madarasa , uhaba wa maabara , maktaba , Kompyuta na uchache wa walimu wa Sayansi na Hisabati lakini haya yote yako katika mpango wa maendeleo wa elimu ili kuhakikisha tunakabiliana na changamoto ya elimu na sio muda mrefu tutaona matokeo,”alisema Rais Dk. Mwinyi.
Alifahamisha kuwa uwekezaji katika elimu ni wa muda mrefu na ukianza kuekeza sasa unaweza kupata matokeo baadae sana lakini matokeo yake imeshaanza kuonekana kwa hivyo hukuna sababu kwanini wasiendeleze hapo hapo badala ya kusubiri matokeo miaka kumi ijayo.
Hata hivyo, Dk. Mwinyi aliwapongeza wadau mbali mbali wamekuwa msaada mkubwa wa kuunga mkono serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika safari yake ya kielimu .
Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Leila Mohammed Mussa alieleza hatua zitakazoendelea kuwekwa na Wizara hiyo katika kuhakikisha ufaulu unaongezeka hasa kwa kidato cha Nne.
Nae Katibu mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ali Khamis Juma akitowa Takwimu za uafaulu wa wanafunzi alisema Mtihani ya kidato cha nne ulifanyika mwezi Novemba 2021 na matokeo yake yalitoka January 2022 ambao jumla ya wanafunzi 15,569 walifanya mtihani huo na wanafunzi 4,403 wamefanikiwa kuendelea namasomo ya kidato cha tano Julai 2022.
Alifahamisha kuwa ufaulu wao ni kati ya daraja la kwanza hadi la tatu na ni sawa na asilimia 28.3, kati ya wanafunzi hao ,wanafunzi 445 walipata daraja la kwanza ambapo nisawa na asilimia2.8 tu,ambao hawa wa hapa Pemba 137 ni miongoni mwao.
Alisema takwimu hizo zinaonesha mwenendo na mabadiliko ya kila daraja ila tunakuahidi watahiniwa wakidato cha nne 2022 watakuja na matokeo mazuri zaidi.
“Uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na watendaji wote tutasimamia utekelezaji wake na Inshaallah matokeo yatakuridhisha kwani kwetu sisi hii ni vita na hakuna sababu ya kurudi nyuma”,alieleza.
Aliendelea kueleza kuwa Mtihani ya kidato cha sita ulifanyika mwezi Mei 2022 na matokeo yake yalitoka Julai 2022 ambao jumla ya wanafunzi 3,683 walifanya mtihani huo na wanafunzi 3,644 wamefanikiwa kuendelea na masomo elimu ya juu katika vyuo vya ndani na nje kwafani zozote ambazo Serikali zitaweka kipaumbele kulingana na mahitaji yaSerikali.
“Kati ya wanafunzi hao,wanafunzi 693 waliopata daraja la kwanza, ambao 151 ni miongoni mwao wapo hapaleo’, alisema.
Alisema Takwimu alizozisoma zinaonesha mabadiliko ya ufaulu mwaka hadi mwaka mfano mwaka 2020 daraja la kwanza ni 124 na mwaka 2022 ni 693, mwaka huo huo 2020 daraja sifurini 99 na mwaka 2022 ni .
Katibu mkuu huyo aliwashukuru wanafunzi, walimu,wazazi,walezi na wadau wa elimu mbalimbali ambao wako pamoja nao katika kusaidia utoaji na upatikanaji wa elimu bora, ambao miongoni mwao ni MIF,UNICEF,GPE,SIDA,KOICA,MILELE FOUNDATION, TANZANIA CENTRE FOR EDUCATION,FAWE,UNESCO, GOOD NEIGHBOURS, WORLD BANK, EARLY CHILHOOD MAADRASA na wengine wengi.
Kwa upande wake Mfanyabiashara maarufu Zanzibar, Said Nassor (Bopar) aliahidi kuwapatia zawadi za Kompyuta aina ya Laptop wanafunzi hao wote kwa kushirikiana na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi pamoja na Makamo wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdullah.
Pamoja na hayo, wanafunzi hao waliipongeza hatuwa hiyo iliochukuliwa na Serikali ya kuwakutanisha na Rais kwa ajili ya kuwapongeza na kula nao pamoja.
Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,
Ikulu Zanzibar.