NA ABDI SULEIMAN.
WADAU wa Habari Kisiwani Pemba, Wamesema licha ya waandishi wa habari kulindwa na maadili ya habari na kanuni, lakini bado waandishi hawajawa salama hivo lazima sheria mpya ya habari ionyeshe uasalama wake.
Walisema hata kama mwandishi atafanya kosa, sio kukamtwa moja kwa moja na kupokonywa vifaa vyake, bali uchungu upanaswa kufanyika na ikithibitika ndio kutiwa hatiani kisheria.
Wadau hao wa habari waliyaeleza hayo, katika kikao cha utoaji maoni juu ya Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988 kama ilivyorekebishwa na sheria namba 8 ya mwaka 1997 na Mapungufu yaliyomo katika Sheria ya Tume ya Utangazaji ya Zanzibar namba 7 ya mwaka 1997 kama ilivyorekebishwa na sheria namba 1 ya mwaka 2010
Said Rashid Hassan kutoka kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar Tawi la Pemba, alisema ifike wakati sheria hiyo inayokuja iweze kuonyesha inamlinda vipi mwandishi wa habari wakati anapokua katika kazi na sio kumpana na kumtia matatizoni.
Alisema kifungu cha 27 cha sheria hiyo, kifungu hicho kinahatarisha usalama wa mwandishi, hivyo kifungu hicho kinapaswa kubadilishwa au kiondoshwe kabisa ili kuwapanafasi waandishi kufanya kazi zao.
“Sheria zote zimezungumzia suala la adhabu, hakuna sehemu iliyozungumzia kuwalinda waandishi, vizuri sheria ikaonyesha wazi vifungu au kifungu cha kuwalinda waandishi,”alisema.
Bakari Mussa kutoka Gazeti la Zanzibarleo, alisema sheria isitowe nafasi kubwa kwa viongozi, pamoja na hao wajumbe watakaoteuliwa wasiwe miongoni mwa wakuu wa vyombo vya habari.
Aidha alishauri baada ya kupatikana kwa sheria hiyo mpya, ipo haja kwa sheria hizo kugaiwa au kupatiwa kwa taasisi za kihabari ili waandishi wa habari waweze kuisoma na kuijua sheria yao.
Naye meneja wa sheria jamii micheweni Ali Massoud Kombo, alisema kanuni ya vyombo vya habari vya mtandaoni Zanzibar 2019, inapaswa kufanyiwa marekebisho kwani imekua ikikandamiza vyombo hivyo katika suala la ulipaji wa ada.
“serikali inahimiza vijana kujiajiri wenye, baadhi ya vijana wameitikia wito kwa kuanzisha mitandao ya kijamii, ikiwemo blog, online TV na mitandao mengine lakini sasa ajira zao zinaelekea ukingoni kutokana na gharama za ulipaji kupanda kupitia kiasi,”alisema.
Kwa upande wake afisa ufuatiliaji na Tathmini kutoka TAMWA Zanzibar Mohamed Khatib, alisema kuna baadhi ya vifungu katika sheria ya hiyo vimekua sio rafiki kwa waandishi wa habari, hali inayopelekea baadhi ya waandishi kufanya kazi kwa woga.
Alisema TAMWA imekua ikikutana na wadau mbali mbali wa habari kujadili, mapungufu yaliyomo ndani ya sheria hiyo na kutoa maoni yao, ili mwisho wasiku maoni hayo yawasilishwe na kuwa na sheria rafiki kwa waandishi.
Naye Mjumbe wa Bodi wa Tamwa Zanzibar Shifaa Said Hassan, alisema kuna baadhi ya vifungu katika shehia hiyo, vinaminya uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza, hali inayofanya vifungu hivyo vifanyiwe marekebisho ili kufikia huko wadau ni kupaza sauti zao.
Alifahamisha kuwa tayari serikali ipo katika mchakato wa kurekebisha sheria ya habari na sheria ya tume ya utangazaji, hivyo wadau wanapaswa kushirikia katika utoaji wa maoni yao wakati utakapofika.
MWISHO