NA ABDI SULEIMAN.
WATAALAMU kutoka kitengo cha Maradhi yasiyoambukiza Zanzibar (NCD UNIT), wamesema maradhi hayo yamekuwa ni hatari na kupoteza maisha ya watu kimnya kimnya kuliko maradhi mengine.
Kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya duniani(WHO), zinaonyesha kuwa maradhi hayo yanauwa watu milioni 41 kila mwaka sawa na 71% ya vifo vyote duniani kote mwaka 2021.
Hayo yameelezwa na afisa kutoka kitengo hicho Rabia Ali Makame, wakati wa mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari Kisiwani Pemba, katika ukumbi wa maabara ya afya ya jamii Wawi Wilaya ya Chake Chake.
Afisa huyo alisema Kila mwaka zaidi ya watu milioni 15 wanakufa kutokana na maradhi yasiyoambukiza, kati ya umri wa miaka 30 mpaka 69 sawa na 85%, ambapo vifo hivo vya mapema hutokea kwa nchi yenye vipato vya chini na vya kati.
Alisema utafiti uliofanywa na wizara ya afya Zanzibar mwaka 2011, umeonesha kuwa watu wenye umri wa miaka 25-65, sawa na asilimia 33% wanaishi na shinikizo la damu, wakati asilimia 3.7% wanaishi na ugonjwa wa kisukari.
Kwa upande wa Takuwimu za Saratani zimeripotiwa katika hospitali zetu za Unguja na Pemba, kwa wagonjwa wapya zinaonyesha Saratani ya matiti 2019 ni wagonjwa 62, 2020 ni wagonjwa 39 na 2021 ni wagonjwa 63, kwa mwaka 2022 Januari mpaka Juni ni wagonjwa 19.
Kwa upande wa Saratani ya shingo ya kizazi 2019 waligundulika wagonjwa wapya 70, 2020 wagonjwa wapya 48, 2021 wagonjwa 31 na Januari mpaka Juni wamegundulika wagonjwa 10
Nayo Saratani ya tezi dume 2019 wagonjwa 49, 2020 wagonjwa 23, 2021 wagonjwa 30 na 2022 Januari mpaka Juni wagonjwa 12, huku akiwataka wananchi kuacha kutumia tumbaku, Pombe, uzito mwingi, msongo wa mawazo, kutokufanya mazoezi na ulaji usiofaa kama Vyakula vya uwanga kwa wingi, mafuta, sukari, chumvi na Ulaji wa nyama nyekundu kwa wingi.
Kwa upande wake mratib wa kitengo hicho Zanzibar Dk.Omar Abdalla Ali, alisema lengo ni kuwafundisha wanahabari nini maradhi yasiyoambukiza yakiwemo kisukari, shinikizo la juu la damu na saratani, ili waweze kutumia taaluma hiyo kwa kuelimisha na kuhamasisha jamii jinsi ya kupambana na maradhi hayo.
Alisema waandishi wa habari wananafasi kubwa ya kuelimisha jamii kupitia vyombo vyao vya habari, ili jamii iweze kufahamu na kupunguza kabisa kwani magonjwa hayo yamekua tishio kubwa.
“Iwapo jamii itaweza kubadilika katika ulaji wa vyakula, basi kutaweza kupunguza maradhi hayo kwa kiasi kikubwa sambamba na kufuata ushauri wa madaktari,”alisema.
Nao washiriki wa mafunzo hayo wamesema watahakikisha wanatumia taaluma zao katika kuelimisha jamii, juu ya madhara ya maradhi hayo sambamba na jamii kuchukua tahadhari kubwa.
MWISHO
Abdi Juma Suleiman