Wednesday, January 1

RC azipongeza NGOs kuhamasisha sensa kwa wananchi

NA ABDI SULEIMAN.

MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, amesema uwamuzi uliobunia na taasisi ya Nasimama na Dk.Mwinyi Foundation, kuhamasisha zeozi la Sensa kwa wananchi ushajihishaji wa wananchi kudai risiti za kieletroniki ni jambo la kuungwa mkono na wananchi wote.

Alisema taasisi hiyo imeonesha mfano mzuri, kwani elimu hiyo ya sensa ya Watu na Makaazi itaweza kuwafikia wananchi wengi kupitia mabonanza mbali mbali yanayotarajiwa kufanyika.

Mkuu huyo aliyaeleza hayo mara baada ya kumalizika kwa zoezi la ufanyaji wa usafi katika hospitali ya Chake Chake, zeozi lililowashirikisha viongozi mbali mbali na kuratibiwa na taasisi hiyo.

Alisema zoezi la Sensa litaisaidia serikali kujua idadi halisi ya watu wake, idadi ambayo itasaidia katika kupanga mipango ya maendeleo, kwani wananchi wanahitaji majengo, barabara na lazima idadi halisi ijulikane.

“Lazima kila mmoja wetu akubali kuhesabiwa muda na siku itakapofika, idadi kamili yetu ndio itakayosaidia mambo mengi muhimu kwa serikali, lazima tukubali kuhesabiwa kwa manufaa ya taifa letu,”alisema.

Akizungumzia suala la usafi, mkuu huyo alisema suala la afya linahitaji kuwa na mazingira mazuri, kwani tiba ya kwanza spitali ni usafi hivyo aliwataka kuendelea kuhamasishana juu ya suala hilo.

Aidha alizitaka taasisi nyengine na wadau kujitokeza na kusaidia hospitali, katika suala zima la usafi kuwa katika mazingira bora ikizingatiwa idadi ya wafanyakazi waliopo ni wachache.

Kwa upande wa Risiti za kieletroniki, Mkuu huyo aliwataka wananchi kudai risiti kila wanaponunua bidhaa, kwani serikali iweze kupata mapato yake ili kuwafikishia wananchi maendeleo.

“Barabara, maji, mishahara, walimu, madaktari vyote hivyo vinahitaji fedha, tusipodai risiti basi serikali haitopata fedha za kutekeleza mambo yote hayo, hakuna serikali yoyote dunaini inayoendeshwa bila ya kodi,”alisema.

Mkurugenzi wa taasisi ya Nasimama na Dk.Mwinyi Foundation Zanzibar, Othman Haji Hamad, alisema lengo la zoezi hilo ni kuwaunga mkono juhudi za viongozi wa SMT na SMZ katika kushajihisha wananchi kujitokeza kuhesebaiwa wakati utakapofika.

Alisema hospitali ni sehemu muhimu sana kwa wananchi, wagonjwa mbali mbali hufika kupata matibabu, ikizingatiwa watu wazima, vijana, watoto hufika na kupatiwa tiba.

Hata hivyo aliwataka wananchi kuendelea kudai risiti wanapofanya miamala madukani, kwani fedha za serikali hazipotoweza kupotea na serikali iatapata mapato yake.

Kwa upande wake Dktari dhamana wa Hospitali ya Chake Chake, Dk Abrahman Mselem, aliishukuru taasisi hiyo kwa uwamuzi wake wa kufanya mazoezi katika sehemu hiyo muhimu kwa jamii.

Hata hivyo alizitaka taasisi nyengine kujitokeza kwa hali na mali kusaidia suala la usafi kwa hospitali hiyo, kwani ndio sehemu muhimu na inayohitaji kuwa safi muda wote.

MWISHO