Sunday, November 24

VYAMA VYA SIASA VINAPASWA KUWA NA MIFUMO IMARA YA KUWAPA NAFASI WANAWAKE,

NA ABDI SULEIMAN.

IMEELEZWA kuwa kukosekana kwa mifumo imara, inayowajengea wanawake misingi bora ya uongozi katika ngazi mbalimbali, ndio kikwazo kikuu kinachokwamisha ufikiaji wa usawa wa kijinsia katika vyombo vya maamzi nchini.

Hayo yameelezwa na viongozi wa vyama vya siasa katika ukumbi wa Maktaba Kuu Kisiwani Pemba, katika mkutano wa kujadili mbinu na hatua ambazo zinatakiwa kuchukuliwa na vyama hivyo, ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi.

Walisema bado katika baadhi ya vyama vya siasa, hakujawa na mifumo imara inayoweza kuwajengea wanawake misingi bora ya uongozi ili waweze kufikia usawa wa kijinsia katika ngazi za maamuzi.

Aidha viongozi hao walisema, bado kuna ufinyu wa elimu kwa wanawake katika kuzielewa na kuzitambua haki zao za msingi, na wajibu wao wa kushika nafasi katika vyombo tofauti vya maamuzi nchini.

Katibu wa Chama cha ACT-Wazalendo Mkoa wa Chake Chake Pemba Saleh Nassor Juma, alishauri serikali na wadau wa elimu kuingiza somo la jinsia katika mtaala wa elimu, ili kuafundisha wanafunzi umuhimu na haki za usawa wa kijinsia katika ngazi za msingi.

Alisema elimu hiyo inapswa kutolewa tokea ngazi ya msingi, kwani wanafunzi wanapokuwa wadogo wanakumbana na mambo mbali mbali majumbani mwao na mitaani, hivyo somo hilo litakuwa mkombozi kwao kupinga mfumo dume unaoanza tokea utotoni.

“Lazima kuwepo kwa mtaala maalum wa somo la usawa wa kijinsia kwenye sikuli kuanzia ngazi za msingi, hii itasaidia kuwaandaa watoto wetu hasa wakike, kukua na wakitambua misingi ya uongozi kuanzia ngazi za chini kabisa,” alieleza.

Naye Riziki Mgeni Juma Kutoka Chadema Wilaya ya Chake Chake,  alishauri kuanzishwa kwa mfuko maalum wa kuwawezesha wanawake utakao wapatia pesa, ili kumudu changamoto za kiuchumi zinazokwaza ushiriki wao kwenye kugombea nafasi za uongozi.

“Tunahitaji sasa bajeti ya nchi iweke kipengele cha mfuko wa uwezeshaji wanawake, ili mfuko huo uwawezeshe kuwa na uwezo na nguvu za kwenda majimboni kupambana na wanaume, kwani ukosefu wa nguvu za kiuchumi kwa wanawawake ni tatizo kubwa linalowakwamisha kutokana na vyama vingi kukosa ruzuku,”alisema.

Aidha alisema wakati umefika kwa wanawake kuondosha udhaifu wao kwa kupendana ili wanaume nao waweze kuwaunga mkono ikiwemo waume zao majumbani.

Kwa upande wake Mwenyeki wa Wanawake chama cha ADC Mkoa wakusini Pemba Shekha Ali Yussuf, alisema wanawake wanapaswa kuwa na umoja na mstari wambele, wakati wanapoamua kuingia katika majimbo kugombani nafasi mbali mbali za uongozi.

Mapema mratib wa mradi mradi wa kuwawezesha wanawake katika nafasi za uongozi(SWIL), unaotekelezwa na PEGAO na kufadhiliwa na ubalozi wa Norway, Dina Juma, alisema katika utekelezaji wa mradi huo tayari wamefanya shuhuli mbali mbali, ikiwemo kupita katika shehia kuhamasisha jamiijuu ya suala hilo na wamefikia shehia 44 kati ya shehia 133.

Alisema tayari wameshafanya mikutano mbali mbali na kuibuliwa changamoto kadhaa, zinazogusa moja kwa moka katiba na miongozo hali iliyopelekea kukutana na viongozi wa vyama vya siasakujadili kwa pamoja na kutoka na maazimio ili wanawake nao wapate nafasi za kutosha katika vyombo vya maamuzi kuanzia ngazi za chini hadi Taifa.

Akiwasilisha mada ya jinsi Mratib wa TAMWA Pemba Fathiya Mussa Said, alisema uchambuzi wa kijinsia unaonyesha kuwa kundi kubwa la wanawake linachangamoto za kijinsia, ambapo wanawake kudhulumiwa haki zao mara baada ya talaka,wanaachiwa watoto bila ya kupatiwa matunzo na wanaume na haki za mirathi zinazoachwa na wazazi kufariki.

Alisema kiwango cha uelewa kwa wanawak, Demokrasia na uongozi umeongezeka, ambapo Jumla ya wanawake 216 kati ya 939 wanaume sawa na asilimia 20%, walipitishwa na vyama vyao kuwa wagombea kwa nafasi tofauti wakiwemo 61 kugombea nafasi za Wawakilishi, 74 Madiwani, 81 kwa nafasi za Ubunge. Walioshinda mchakato huu ni 37 tu.

“Tunataka tujipange ili kufikia 2025 wanawake tujitokeze kwa wingi kugombea nafasi za uongozi, ili kufikia lengo la 50/50 uchaguzi utakapofika,” alisema mtarib Fat-hiya.

Akiwasilisha mada juu ya Mapungufu katika shehia za vyama vya siasa, mwanasheria kutoka kituo cha huduma za sheria Pemba Safia Saleh Sultan, alisema bado sheria mbali mbali Zanzibar hazijaonyesha kuwepo kwa uwiano wa usawa wa kijinsia kati ya wanawake na wanaume katika ngazi mbali mbali za maamuzi.

MWISHO