Monday, November 25

VANILA NI ZAO LA KIUTALII LINALOHIFADHI MAZINGIRA

MKULIMA wa Vanila katika kijiji cha Daya Mtambwe Kusini Bakari Mataka Bakari, akiwaonyesha waandishi wa habari kutoka wa JET, mti unaojulikana kwa jina la Oll spaisi, unaopatikana katika shamba la viungo huko Daya, wakati walipofanya ziara Kisiwani Pemba ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa tuhifadhi maliasili Tanzania unaofadhiliwa na USAID.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

 

VANILA NI ZAO LA KIUTALII LINALOHIFADHI MAZINGIRA.

  • Wakulima waahidi kuendelea kulima kwa kutumia kilimo hai.

NA ABDI SULEIMAN.

SUALA la uhifadhi wa Mazingira ni kitu ambacho hakiepukiki kwa kila mwananchi, ikiwa shambani, mtaani, njiani, barabarani hata majumbani.

Sote tunaelewa kuwa mazingira ni kitu muhimu kwa mustakbali mzuri wa maisha ya mwanadamu, mimea, wanyama na viumbe vilivyoko chini ya bahari.

Vanilla (Vanila Fragrans) ni moja ya mazao yanayohifadhi mazingira, tokea upandaji wake, ukuaji, uotaji hadi ustawi wake.

HISTORIA YA VANILLA.

Asili yake ni Amerika ya kati huko Mexico, Guatemala na Costa Rica, ilianza kutumika tangu karne ya 15, barani ulaya ilifika karne ya 16 katika visiwa vya Reunion, Mauritius, Madagasqa, Shelisheli, Tahit na Comoro kati ya karne ya 18 na 19 na sasa linazalishwa kwa wingi Madagasca,Comoro na Reunion.

Tanzania liliingizwa Mkoani Kagera mwaka 1962 kutoka nchini Uganda, Mkoa wa Kagera unazalisha katika Wilaya ya Bukoba na Muleba, Zanzibar Vania inaleta fedha za kigeni na ajira kwa wananchi.

TABIA YA VANILA(MMEA)

Ni mmea ambao hutambaa kwenye mti na huzaa matunda yanayofanana na maharage, mmea hukua kufikia urefu wa mita 10 hadi 15, maua yake ni makubwa manene na yananukia, rangi ya kijani isiyokolea na njano, ukubwa wa harage ni kiasi cha sentimita 10-25 na unene wa 1.5cm.

MAENEO YANAYOFAA KWA UZALISHAJI

Zao hili kama ilivyo mazao mengine mengi hustawi vizuri kwenye udongo wenye kupitisha maji, rutba na mboji ya kutosha kiasi huhitajika kwani ni mme ambao haupendi jua kali.

HALI YA HEWA INAYOFAA

Zao hili huhitaji hali ya hewa yenye wastani wa nyuzi joto za sentigradi 28, inaweza kuhimia nyuzi joto za sentigradi 21 hadi 30.

Huhitaji mvua zenye mtawanyiko mzuri wa milimita kati ya 1,500 na 3,000, na inaweza kustawi vizuri katika mvua za wastani wa milimita 2,000, Vanila ya porini inaweza kustawi zaidi maeneo yenye unyevunyevu yalio usawa wa bahari hadi mita 600.

Katika kisiwa cha Pemba zao hili zaidi linalimwa katika kijiji Daya shehia ya Mtambwe Kusini Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, ikiwa ni kilimo kilichoajiri watu wengi ikiwa ni zao la utalii.

 WAKULIMA WA VANILA

Bakari Mataka Bakari mkulima wa Vania Daya Mtambwe, amesema  wataendelea kutumia kilimo hai, kwa ajili ya kuhifadhi mazingira katika mashamba yao na kupata vanilla zilizokuwa bora na zenye kuvutia wageni.

Amesema bidhaa za viungo wanavyolima, lazima viwe katika hali ya mazingira mazuri, hivyo suala la uharibifu wa mazingira katika mashamba yao ni marufuku kufanyika.

“Sisi tunalizama biashara za viungo kama vile Vanila, Hiliki, Mdalasini, Mchaichai, Pilipili Manga na karafuu zinahitaji mazingira mazuri, muda wote vinapokuwa shambani,”amesema.

Mkulima mwengine Amina Ali Mmanga, amesema wageni wangi wanaofika katika mashamba yao, huvutiwa na mazingira mazuri ambayo yanapatikana.

Amesema wamekuwa wakali pale wanapoona wananchi wanaharibu mazingira, kwani mazingira mazuri ya misitu yanapelekea hata vilimo vyao kunawiri ipasavyo.

“kilimo hiki kimetusaidia sana katika kuhudumia familia zetu, yapo mambo mengi tunahudumia familia na wala hatuwaombi pesa waume zetu, ikiwemo baadhi ya vitu vya skuli kwa watoto,” alisema.

Naye Safia Ali Mmanga amesema kabla ya kuingia katika kilimo cha viungo hali za maisha zilikua ngumu, lakini sasa riski yake anapata na kuhudumia watoto wake.

“Kwa sasa natengeneza madogo ya karafuu kwa ajili ya kusafishia mwili, sabuni za karafuu na viungo vyengine hulazimika kuvisaga na kuvichanganya pamoja,”anasema.

Fatma Yussuf Said mkulima wa viungo Mtambwe, akizungumza na waandishi wa habari kutoka Chama cha Waandishi wa habari za Mazingira Tanzania (JET), juu ya kilimo cha Viungo kinavyolimwa ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa tuhifadhi maliasili Tanzania unaofadhiliwa na USAID.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

Hata hivyo ameiyomba serikali kuwawekea kiwanda cha kusarifu bidhaa zao, ikiwemo vanilla na karafuu kwani wanaweza kutengeneza vitu vingi kwa ajili ya jamii.

Fatma Yussuf Said mkulima wa viungo Mtambwe, ameiyomba serikali kutokuwaacha nyuma wanawake, waliojikita katika kilimo cha Vanila kinacholimwa kwa kuhifadhi mazingira.

“Tutakapo wezeshwa kwa kupatiwa mikopo na masoko, basi kilimo cha vanilla, mdalasini na michaichai tutaweza kuzisarifu ipasavyo na kuongeza thamani,amesema.

USHIRIKA WA VANILA DAYA

Katibu wa kikundi cha Daya Cooperative Society Mohamed Ali Mmanga, ansema walianza kulima mwaka 1992 hadi sasa bado wanaendelea na kilimo hicho.

Kilimo cha vanilia kina faida kubwa kuanzia mti, mazao wenyewe na mpaka mbegu zake kwao ni biashara, kilo moja ya vanilla kavu ni shilling Milioni 1,000,000/= hadi laki 900,000/=.

Anasema mpaka sasa bado wanaendelea kutumia kilimo hai, ambacho hakiharibu mazingira kwa ajili ya kulinda mazingira yaliyozunguka vilimo vyao.

“Sisi hapa miti muda wote ipo katika hali nzuri, kilimo hichi cha viunguo kinahitaji mazingira ya ubaridi baridi na kuvutia ndio maana hapa watalii wakija huvutiwa na mazingira husika,”alisema.

Aidha amesema kilimo chao ni kilimo msitu, hawawezi kukata miti kutokana na vanilla na mikarafuu huhitaji miti mikubwa kwa ajili ya kwenda juu.

ASASI ZA MAZINGIRA

Mkurugenzi Mtendaji wa chama cha waandishi wa habari za Mazingira Tanzania (JET) John Chikomo, amesema baada ya mafunzo sasa ni wakati kwa waandishi kuandika habari kwa wingi zinazohusiana na masuala ya uhifadhi wa malia asili, ikiwemo uhifadhi wa mazingira, wanyama na kilimo cha viungo.

Amesema kilimo cha Viungo kinahitaji uhifadhi mzuri wa mazingira, katika uotaji wake hadi ukuaji kwani kinastawi wizuri na kua na harufu inayovuti wageni.

“Kilimo cha viungo ni moja ya vivutio vikubwa kwa wageni kutembelea, zaidi huvutiwa na mazingira ya eneo husika lilivyo tunzawa,”amesema.

Mkurugenzi wa Community Forest Pemba Mbarouk Mussa, amesema kilimo cha Vanila lazima kinahitaji mazingira mazuri ya Upandaji na ukuaji wake, unapelekea vanilla inayozaliwa kuwa na harufu nzuri.

Amesema vanilla za Pemba ni za kipekee kutokana ladha yake, tafuti na Vanila zinazopandwa katika nchi nyengine hata uzuri wake.

“Tunahamasisha wakulima kuhifadhi mazingira katika mashamba yao, Vanila haihitaji jua kali bali inahitaji kivuli na mwanga hafifu,”alisema.

MTI wa Vanila Ukiwa umepatandwa katika moja ya mashamba ya maonyesho Chanamangwe hivi karibuni, jinsi ya kilimo hai kinavyolimwa na hakiharibu Mazingira.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

TAASISI ZINAZOHUSIKA NA MASUALA LA KITALII

Afisa Utalii Mkoa wa Kaskazini Pemba Saleh Malik Abdi, amesema wanachukua jukumu la kuhamasisha wakulima wa Viungo kuhifadhi mazingira, zao la Vanila ni moja ya vivutio vya kiutalii nchini.

Amesema kilimo kinacholimwa ni kilimo hai kwa 100% kinasaidia uhifadhi wa mazingira, hakihitaji kemikali na kwenya mashamba hakuhitaji mifuko ya plastiki kwa lengo la kulinda afya.

“Tunawashauri wakulima kutengeneza mazingira yao kiutalii, mashamba mengi yako lakini hayako kiutalii na yako kibiashara kulima na kuvuna na kuuza, linapokuwa kiutalii wanaweza kupata fedha muda wote,”alisema.

Amesema kijani ya Pemba ni kimoja ya vivutio vya utalii, ikiwemo miti ya asili na ukitia moto mashamba inaua bayonuai, huku akiwataka wakulima kuendelea kuhifadhi mazingira katika mashamba yao.

TAASISI ZA SERIKALI

Afisa Mdhamini Wizara ya Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo Idrisa Hassan Abdullah, amesema Pemba wanawakulima wa kilimo cha viungo zaidi ya 584, wanaolima vitu mbali mbali ikiwemo Vanila, Hiliki, Mdalasini, Manjano na Tangawizi.

Amesema wanavuna vanilla kavu kilo 500 hadi 700 kwa msimu mmoja na Mwaka wanavuna marambili, na kwa sasa bei elekezi iliyopo  sokoni ni shilingi laki tatu (300,000) kwa kilo, kwani bei inapanda na kushuka inategemea soko la dunia lilivo.

“Wakulima wanapaswa kuendelea na kilimo hai, kilimo ambacho hakiharibu mazingira nirafiki mkubwa wa mazingira na kuvutia wageni,”amesema.

Aidha amefahamisha kwamba kilimo kinaweza kuwapatia ajira watu, ikizingatiwa mikakati ni kuzalisha kwa wingi na chenye ubora ili kulikamata soko la bidhaa hizo.

NINI KIFANYIKE

Ashura Kombo Ali anasema wataendelea kutumia kilimo hai katika suala zima la kilimo cha viungo, ikiwemo kilimo cha vanilla, hiliki na mazao mengine, kwani yamekuwa mtunzaji mkubwa wa mazingira.

Kombo Khamis Juma ameiyomba Serikali kutilia mkazo katika suala la uhifadhi wa mazingira, kwani watalii wamekuwa wakivutiwa na mazingira yanayotunza katika kilimo cha viungo.

Afisa Mdhamini Wizara ya Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo Idrisa Hassan Abdullah, amesema serikali itaendelea kuthamini juhudi zinazochukuliwa na wakulima wa vanilla pemba katika kuendeleza uhifadhi wa mazingira.

MWISHO