Friday, November 15

MAJAJI WAMALIZA KAMBI KUSIKILIZA RUFAA ZA MWAKA 2018 PEMBA

NA ZUHURA JUMA, PEMBA.

MAJAJI wawili wa mahkama kuu Zanzibar, wamemaliza kambi ya mwezi mmoja kisiwani Pemba, iliyokuwa na lengo la kusikiliza kesi za rufaa, zikiwemo za jinai ambazo zimefikishwa mahakamani kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka 2021.

Akizungumza na waandishi wa habari hizi, Naibu Mrajisi wa Mahkama kuu Pemba Faraji Shomari Juma alisema, baada ya uchunguzi mdogo uliofanywa na mahkama, uligundua kuwa kuna mrundikano mkubwa wa kesi za rufaa za mahkama kuu kisiwani humo.

Alisema, licha ya majaji kuwa na utamaduni wa kwenda Pemba kwa ratiba zao za kawaida kufuatilia kesi, lakini Jaji mkuu ameona ni vyema, kuwapeleka Pemba majaji wawili kwa muda wa mwezi mmoja, ili kupunguza kesi.

“Baada ya kuonekana kuna kesi nyingi ndipo Jaji Mkuu amewaleta majaji wawili, ambao walipiga kambi kwa muda wa mwezi mmoja, tunashukuru kesi nyingi zimeshatolewa maamuzi”, alisema.

Alieleza kuwa, wameona zipo rufaa zaidi ya 25 ambazo nyingine ni tangu mwaka 2018, jambo ambalo lilikuwa likiwatesa wananchi kutokana na kukaa kwa muda mrefu bila ya kupata haki zao.

“Kwa wananchi sasa wamekuwa na imani kubwa na mahkama kwa sababu kesi nyingi zimepatiwa hatia, hii ni mafanikio kwetu”, alisema.

Naibu huyo mrajisi wa mahkama kuu Pemba alisema, moja ya sababu zilizopelekea kuwepo kwa mrundikano huo, ni janga la corona, lililopelekea majaji kutofika kisiwani Pemba kuendelea na kesi zao.

“Lakini hata ufinyu wa bajeti wa kuwasafirisha majaji Pemba, nao ulikuwa sehemu ya kusababisha mrundikano huo, ambapo kwa sasa hali ya fedha imeruhusu, ndio maana wameletwa majaji hao”, alifafanua.

Katika hatua nyingine, aliwapongeza mawakili kwa ushirikiano waliouonesha kwa mahkama katika kupunguza kesi hizo licha ya kuwa ni za muda mrefu.

Hata hivyo amewashukuru wananchi kwa ushirikiano wao waliouonesha kwa kufika kwa wingi mahkamani, jambo ambalo limesaidia kesi hizo kupata hatia kwa haraka.

“Awali katika kipindi cha kuanzia Septemba 8 hadi 21 mwaka huu majaji hao walikuwepo kisiwani hapa kwa lengo la kushughulikia rufaa 47, ambapo walifanikiwa kumaliza kesi 35 na kubakia 12 tu”, alifafanua.

Akizungumza kwa njia ya simu, wakili wa kujitegemea Pemba Zahran Mohamed Yussuf, alisema kuja kwa majaji hao imekuwa ni faraja kwao, kwani haki inapocheleweshwa ni sawa na kukosekana.

‘’Haki inapocheleweshwa huwa kama iliyokosekana, kwani hata wananchi wanakata tamaa, lakini sasa kama majaji watakuwa na tabia hii ya kupiga kambi kama hii iliyofanyika, kwetu sisi mawakili wa kujitegemea itatusaidia kwa kiasi kikubwa,’’alieleza.

Mwanasheria dhamana wa Ofisi ya Mkurugenzi mashataka Mkoa wa kaskazini Pemba, Mohamed Ali Juma alisema, kuja kwa majaji hao kumezaa faraja, kwani mrudikano wa kesi mahakamani umepungua kwa kiasi kikubwa.

“Sisi ujio wa majaji wa kupiga kambi kwa muda mwezi mmoja Pemba, umesaidia kupunguza mrundikano wa kesi za rufaa, maana zipo nyingine tangu mwaka 2018 hazijaguswa,’’alisema.

Baadhi ya wananchi kisiwani Pemba, wamesema uamuzi uliofanywa Mahkama kuu ya kuwasafirisha majaji wawili kwa lengo la kusikiliza kesi ni jambo jema.

Majaji waliokuja kisiwani Pemba kuweka kambi kwa muda wa mwezi mmoja ni Abdull-hakim Ameir Issa na George Joseph Kazi, huku ikiwa tayari mwezi Disemba mwaka 2021, kisiwa hiki kilipata Jaji mkaazi Ibrahim Mzee Ibrahim.

                             MWISHO.